Zaidi ya watu 25 wamepoteza maisha baada ya boti yenye abiria zaidi ya 100 kuzama katika mto Fimi, katika jimbo la Mai-Ndombe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ajali hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa matukio ya aina yake kutokea ndani ya mwaka huu kwenye eneo hili linalozungukwa na mito mingi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na maafisa wa serikali na mashuhuda wa tukio hilo wamesema boti hiyo iliondoka kutoka mji wa Inongo, kaskazini mashariki mwa mji mkuu wa Kinshasa.

Inadaiwa kuwa boti ilizama mita chache tu baada ya kuondoka kwenye bandari ya Fimi, na mpaka sasa, juhudi za uokoaji zinaendelea huku idadi ya watu waliopoteza maisha ikitarajiwa kuongezeka.

Wakaazi wa maeneo hayo wamesema kuwa ajali hii ni miongoni mwa ajali nyingi za usafiri wa majini katika jimbo la Mai-Ndombe, ambalo linategemea usafiri wa majini kutokana na mitaa yake ya miji na vijiji vilivyozungukwa na mito mingi.

Hii ni ajali ya nne kutokea mwaka huu, na hali hiyo imezua hofu kubwa kuhusu usalama wa usafiri wa majini katika eneo hilo.

Serikali inaendelea na shughuli za uokoaji na inawataka wananchi kuwa makini zaidi wakati wanapochukua usafiri wa majini ili kuepuka maafa zaidi.