Takribani watu 241 wameuawa ndani ya saa 24 zilizopita na wengine 382 kujeruhiwa wakati oparesheni ya kijeshi ya Israel ikiendelea dhidi ya kundi la Hamas huko Gaza, Wizara ya Afya ya Gaza ilifafanua katika taarifa yake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na mtandao wa ‘Business Standard’ ikiinukuu wizara hiyo imeeleza Wapalestina wasiopungua 20,915 wameuawa wengi wao wakiwa watoto na wanawake katika zaidi ya wiki 11 za mapigano.
Israel ilisema ilipiga zaidi ya maeneo 100 siku ya Jumanne, huku kukiwa na ripoti za oparesheni za ardhini katikati ya Gaza.
Milipuko mikubwa ilisikika kutoka Ukanda wa Gaza katika eneo la jirani na Israel mapema leo. Vita vilianza tarehe 7 Oktoba baada ya Hamas kuongoza wimbi la mashambulizi Israel.
Watu wapatao 1,200 waliuawa. Takriban watu 240 walirudishwa Gaza kama mateka, na baadhi yao waliachiliwa baadaye.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alivitaja vita hivyo kuwa ni “uhalifu mkubwa” dhidi ya watu wake, na kuvitaja kuwa “zaidi ya janga” na “zaidi ya vita vya maangamizi”.