Takriban watu 18 wamekufa na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea kwenye kituo cha reli cha New Delhi.

Maelfu ya watu waliripotiwa kujaa kwenye kituo cha treni Jumamosi usiku walipokuwa wakijaribu kupanda treni zilizochelewa.

Wanne kati ya waathiriwa walikuwa watoto, huku 10 wakiwa wanawake, kulingana na orodha iliyotolewa na maafisa.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alisema alikuwa pamoja “na wale wote ambao wamepoteza wapendwa wao” kupitia ujumbe wake wa X.

Mkanyagano kwenye umati kunaripotiwa kutokea mara kwa mara nchini India ambapo kila wakati kuna msongamano ama kwenye hafla za kidini, sherehe na maeneo ya umma.

Tukio hilo linatokea wiki kadhaa baada ya watu 30 kuuawa katika mkanyagano uliotokea alfajiri katika tamasha la kidini, Kumbh Mela, kaskazini mwa India, ambapo makumi ya mamilioni ya Wahindu walikuwa wamekusanyika kuoga katika maji matakatifu ya mto katika moja ya siku takatifu za tukio hilo la wiki sita.