
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar
TAKWIMU zinaonyesha kati ya watu 6,000 hadi elfu 12,000 wanahofiwa kuugua ugonjwa wa himofilia nchini huku idadi ya watu waliogundulika kuwa na ugonjwa huo hadi sasa wakiwa ni 451 pekee.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Himofilia Duniani iliyofanyika pamoja na uzinduzi wa Kliniki ya Himofilia, katika Hospitali ya Wilaya ya Ijitimai, Visiwani humo jana.
Hafla hiyo iliandaliwa na Chama cha Himofilia Tanzania (HST), kwa uwezeshaji kutoka Taasisi ya himofilia ya novo nordisk na Chama cha Himofilia Duniani kwa ushirikiano kutoka Serikali ya Tanzania na ya Zanzibar, wizara za afya kutoka pande zote mbili, Hospitali ya Taifa Muhimbili na wadau wengine.

Mheshimiwa waziri alisema takwimu za kidunia zinaonesha mtu mmoja kati ya 10 anapatikana na ugonjwa huo, hii ikimanisha kuwa Tanzania yenye watu takribani milioni 61 inaweza kuwa na wagonjwa elfu 6 hadi elfu 12, huku ikielezwa 97% ya watu wenye ugonjwa huu duniani kote hawajagundulika, ambapo kwa upande wa Tanzania waliogundulika mpaka sasa ni 451 tu.
“Kama tunavyofahamu himofilia ni ugonjwa wa damu kukosa uwezo wa kuganda unaosababishwa na ukosefu wa kiwango cha chembechembe za protini zinazotakiwa kugandisha damu hivyo kusababisha damu kuvuja kwa mda mrefu pindi mtu anavyopata jeraha hivyo kuhatarisha maisha yake.
“Maisha ya watu wenye matatizo haya yanahitaji uangalizi mkubwa na tahadhari kubwa ili kuzuia uvujaji wa damu, ulemavu na vifo hivyo kuwepo na hitaji la kubaini aina ya himofilia na kupata matibabu ya kuchomwa sindano yenye chembechembe za protini zinazokosekana mwilini ili kusaidia kuzalisha damu”, alisema Waziri Mazrui.
Alisema Mwaka 2020 Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikishirikiana na Taasisi ya himofilia ya novo nordisk ilianzisha mradi wa kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma kwa watu wenye magonjwa ya damu lengo kuu ikiwa ni kuunga mkono serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya afya katika kupunguza madhara ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyo ambukiza ikiwemo himofilia na selimundu.
Pamoja na hayo alisema, lengo kubwa la mradi huu ni kuwezesha upatikanaji wa vipimo vya wagonjwa wa damu, seli mundu, na himofilia katika hospitali za rufaa nchini sambamba na kuanzisha kliniki za magonjwa hayo, kuwezesha mafunzo na upatikanaji wataalamu wa afya waliobobea kwenye hospitali hizo pamoja na upatikanaji wa miundo mbinu sahihi, vipimo na dawa ili wagonjwa wahudumiwe mahali popote nchini bila kulazimika kufika Muhimbili.
“Katika maadhimisho haya leo nina furaha kubwa kuwaambia kuwa mradi huu katika kipindi cha uhai wake kuanzia kipindi cha kwanza hadi kipindi cha pili tayari umefanikisha kukamilisha ukarabati wa kliniki za himofilia katika hospitali 13 zikiwemo hospitali za Muhimbili, KCMC, mbeya na Bugando.
“Tunawashukuru pia wafadhili wetu kwa msaada wa dawa zenye thamani ya shs milioni 500, kwa kweli mmetusaidia sana na vifaa nyenye gharama kubwa, chini ya uongozi wa maraisi wetu, Samia Suluhu Hassan na Hussein Ali Mwinyi, tunaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kila mtanzania anapata matibabu kwa usahihi na kwa wakati, hivyo juhudi zenu hizi zinatufanya twende sambamba na juhudi za viongozi wetu hawa”, aliongeza waziri huyo.

Akizungumzia zaidi kuhusu himofilia, Mwenyekiti wa Chama cha Himofilia Tanzania (HST), Dk. Stella Rwezaura alisema, asilimia 70 ya wagonjwa wa himofilia wanarithi na inabebwa katika kinasaba cha kike, kwani mwanamke ana ‘x’ mbili na mwanaume ana ‘xy’, hivyo endapo mwanamke ana ‘x’ yenye vinasaba vya himofilia, asilimia 50 ya watoto wake wa kiume watakuwa na tatizo hilo hivyo kufanya asilimia 99 ya wagonjwa wa himofilia kuwa wanaume.
“Tunaposherehea Siku ya Himofilia Duniani, sambamba na Kauli Mbiu ya Mwaka 2025 isemayo, ‘Wanawake na Wasichana pia wanakumbwa na tatizo la kuvuja damu, licha ya himofilia kuwapata zaidi wanaume, tuwaite wanawake waje kupima, waweze kutambulika mapema hivyo kupata matibabu sahihi.
“ Lengo la mradi huu ni kuwatambua wagonjwa wengi zaidi na kupata huduma kwani wapo wengi wenye tatizo hili na hii ilitokana na changamoto ya uhaba wa vifaa, mashine na vitendanishi vya kutambua ugonjwa huu, hivyo kwa msaada wa wafadhili, vyama vya wagonjwa pamoja na serikali yetu sikivu ya Tanzania, ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, wizara yake ya afya na wadau wengine, huduma hizi sasa zinafika karibu kwa wananchi kwa usahihi zaidi”, aliongeza Dk. Stella.
Naye mmoja wa wagonjwa wa Himofilia ambaye pia anauguza watoto wawili wenye ugonjwa huo, Regina Shirima alisema anakabiliwa na changamoto kubwa ya hali duni ya kiuchumi baada ya kutumia muda wake mwingi katika kuhudumia watoto hivyo kutokuwa na muda kabisa wa kujishughulisha na kazi za kujitafutia kipato.
“Changamoto nyingine ni kwa watoto wenyewe hawapati muda wa kusoma, kucheza na wenzao ama kuwa na furaha kwani muda mwingi wanakuwa wagonjwa, lakini ni ukweli kuwa wanawake ndio wanabeba vinasaba vya himofilia, lawama nyingi zinakuja kwetu kwa kuzaa watoto wenye changamoto hii, hivyo unajikuta familia imekuacha”. Akiongeza kuwa kuna wakati kulikuwa na changamoo ya upatikanaji wa dawa ukizingatia kuwa mgonjwa wa himofilia akikosa dawa tu anaweza uhai wake unakuwa hatarini.
“Natoa wito kwa jamii kuwa gonjwa hili la himofilia lipo na mama sio anayesababisha mtoto kuzaliwa na ugonjwa huu, kwani huwezi kupata mtoto bila ya baba”, aliongeza Bi. Regina kwa mshangao.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Himofilia Tanzania (HST), Dk. Lawrence Museru alisema HST imekuwa sauti ya wenye ugonjwa wa himofilia katika kuangalia changamoto wanazopitia katika kutafuta tiba, moja ya changaoto ni utambuzi wa ugonjwa huu katika jamii.
“Wagojwa wamekuja kutambulika baada ya kupoteza maisha ama kupata ulemavu wa kudumu kwasababu ugonjwa huo haukutambulika hivyo tunaokoa sauti yao kuona jamii na watoa huduma za afya wanatambua ugonjwa huo na wagonjwa wanapata tiba sahihi.
“Tiba sahihi ni ghali sana na serikali haiwezi peke yake, hivyo lazima uwepo ushirikiano kutoka kwa sisi chama ambacho kina wataalamu na wadau wengine ili kuusemea ugonjwa huu, na tunaimani uwepo wako mheshimiwa waziri unafanya ugonjwa huu usemeke katika vyombo vya maaumuzi”, alisema Prof. Museru.
Akimkaribisha Mheshimiwa Waziri, Mkurugenzi wa Tiba na Elimu ya Afya Zanzibar, Dk. Marijani Msafiri alisema katika kipindi cha miaka minne, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dr. Hussein Ali Mwinyi imefanya mapinduzi makubwa katika kuboresha huduma za afya, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa hospitali 10 za wilaya na hospitali moja kubwa ya kisasa ya mkoa ya Lumumba.
“Ndani ya hospitali hizi sasa tumeimarisha miundombinu na huduma, serikali yetu ya awamu na nane pia imeamua kufanya kazi na sekta binafsi ili kutoa huduma bora kwa wagonjwa wote ikiwa ni pamoja na wagonjwa wa himofilia, zikiwemo huduma za maabara, utoaji wa dawa na uendeshaji wa hospitali”, alisema Dk. Msafiri.

