Ndege iliyokuwa imebeba abiria 181 imeanguka katika uwanja wa ndege kusini magharibi mwa Korea Kusini.

Ajali hiyo ilitokea muda mfupi baada ya 09:00 saa za eneo – 00:00 GMT – wakati ilipokuwa ikitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Muan.

Picha zinaonekana kuonyesha ndege hiyo ikiteleza kutoka kwenye njia ya kurukia na kuangukia ukuta, kabla ya baadhi ya sehemu zake kuwaka moto.

Shirika la Kitaifa la Zimamoto sasa linasema kuwa limepata miili 124 kutoka kwenye ajali hiyo.

Kati ya hao, 54 wametambuliwa kuwa wanaume na 57 ni wanawake. Miili 13 ya ziada haikuweza kutambuliwa jinsia yake.

Kufikia sasa, wafanyikazi 1,562 wametumwa kusaidia katika juhudi za uokoaji, wakiwemo wafanyikazi 490 wa idara ya zima moto na maafisa wa polisi 455, kulingana na shirika hilo.

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Muan wa ukubwa wa kati ulifunguliwa mwaka wa 2007, na una njia za kwenda nchi kadhaa za Asia.