Watu 10,262 wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi mkoani Mwanza, hawajulikani waliko kwa zaidi ya miezi mitatu sasa baada ya kutohudhuria kliniki ya kutoa dawa hizo.
Hatua hiyo imekuja huku baadhi ya watu wanaoishi na maradhi hayo nchini wakiendelea kutafakari juu ya ama waendelee au wasiendelee kutumia dawa za kuongeza muda wa kuishi (ARV), kutokana na madai ya kuwapo kwa uchakachuaji wa dawa hizo.
Mratibu wa Ukimwi mkoani Mwanza, Dk. Pius Masele, alitoa taarifa hiyo jijini hapa wiki iliyopita wakati akitoa mada kwenye kikao kilichoandaliwa na Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (SCCS) kwa wadau mbalimbali.
Lengo lilikuwa SCCS kuwataarifu wananchi matarajio yake ya kuzindua mradi unaolenga kuuwarejesha wagonjwa waliokwepa kuhudhuria kliniki kwa ajili ya kupatiwa ARV, kwani dosari zilizokuwapo zimesharekebishwa.
Dk. Masele alisema watu hao 10,262 hawajulikani waliko na kwamba maendeleo ya afya zao hayajulikani, kwa vile hawajafika kliniki kwa zaidi ya miezi mitatu sasa pasipo taarifa zozote.
Alibainisha kuwa idadi hiyo ni sehemu ya watu 34,422 waliojitokeza kupimwa afya zao tangu mwaka 2004 kupitia maeneo yaliyotengwa na Serikali, ambapo ilibainika kuwa wanatakiwa kutumia ARV.
Katika hatua nyingine, Dk. Masele alisema watu 4,455 wameripotiwa kufa mkoani hapa kutokana na Ukimwi, tangu Serikali ilipoanzisha huduma ya kutoa ARV mwaka 2004.
Alifafanua kuwa watu hao ama wamefariki kutokana na kushindwa kuzingatia masharti ya matumizi ya dawa hizo, au kuchelewa kupima afya zao. Hata hivyo, alisema idadi ya maambukuzi mapya ya VVU na vifo vinavyotokana na Ukimwi imepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Kwa mujibu wa Dk. Masele, takwimu hizo zimekusanywa hadi kufikia Machi mwaka huu, na kwamba zinajumuisha Wilaya ya Busega mkoani Simiyu na Wilaya ya Geita mkoani Geita.
Kwa upande wake, Meneja wa SCCS Kanda ya Ziwa, Richard Mbwambo, alisema tume hiyo inatarajiwa kuzindua mradi utakaowezesha kurejesha watu wote waliokwepa kuendelea na matumizi ya ARV.
Pamoja na sababu nyingine, Mbwambo alisema lengo la mradi huo ni kupunguza vifo miongoni mwa watu wenye VVU/Ukimwi.
Alisema mradi huo utazinduliwa mwishoni mwa mwezi huu katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, ambapo Mkuu wa Mkoa huu, Mhandisi Evarist Ndekilo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.