Takriban watu 10,000 wanakisiwa kupotea kufuatia mafuriko makubwa nchini Libya kulingana na afisa kutoka Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC).
“Tunaweza kuthibitisha kutoka kwa vyanzo vyetu huru vya habari kwamba idadi ya watu waliopotea inafikia 10,000 hadi sasa,” alisema Tamer Ramadan, mkuu wa ujumbe wa IFRC nchini Libya.
Mafuriko na maporomoko ya udongo yanayosababishwa na mvua kubwa yameharibu barabara na nyumba nyingi.
Mahali palipoathirika zaidi ni bandari ya Derna, ambayo sehemu kubwa iko chini ya maji baada ya mabwawa mawili na madaraja manne kuporomoka.
“Idadi ya vifo ni kubwa na huenda ikafikia maelfu,” aliongeza Bw Ramadan.
IFRC inaweza hivi karibuni kuwasilisha ombi la ufadhili wa dharura kusaidia wahanga wa mafuriko nchini Libya.