Takriban watu 10 wamekufa na idadi ya wengine isiyojulikana hawajulikani walipo baada ya mgodi kuporomoka katikati mwa Zambia.

Mamlaka nchini Zambia imesema shughuli ya uokoaji inaendelea japo haijabainika idadi kamili ya wachimbaji madini waliofukiwa chini ya ardhi.

Mgodi huo uliporomoka katika Wilaya ya Mumbwa, takriban kilomita 150 magharibi mwa mji mkuu Lusaka. Hata hivyo chanzo cha kuporomoka kwa mgodi huo bado hakijajulikana.

Kamishna wa polisi Charity Chanda amesema miili tisa imepatikana kutoka eneo la tukio huku mtu mwengine akifariki dunia wakati akipokea matibabu hospitali.

Mbunge wa eneo hilo Collins Nzovu amefahamisha kuwa wachimba migodi 20 hawajulikani walipo na wanahofiwa wamepoteza maisha, ingawa Polisi haijathibitisha idadi hiyo.