Na Allan Vicent,JamhuriMedia, Tabora

Watoto wawili wa familia moja katika Kijiji cha Itetemia, Kata ya Itetemia katika Halmashauri ya Manispaa Tabora wamepoteza maisha baada ya kutumbukia katika shimo la choo lililokuwa limejaa maji.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Richard Abwao amethibitisha watoto hao kupoteza maisha wakiwa wanacheza pamoja katika eneo lililokuwa na shimo lililochimbwa kwa ajili ya choo.

Ametaja waliofariki kuwa ni Rashid Hamis mwenye umri wa miaka 3 na mdogo wake Sada Juma mwenye umri wa mwaka 1 na nusu.

Amesema watoto hao walipatwa na umati huo walipokuwa wakicheza karibu na shimo la choo lililokuwa limejaa maji ambapo walitumbukia na kushindwa kutoka hadi wapita njia walipowaona wakihangaika na kuwaokoa.

Kamanda Abwao alibainisha kuwa watoto hao waliokolewa wakiwa hai na kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini kwa bahati mbaya wakapoteza maisha kutokana na kunywa maji mengi.

Ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuchukua tahadhari kwa watoto wao katika kipindi hiki ambapo mvua kubwa zinaendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kupelekea maji kujaa katika maeneo mengi.

Kamanda amesisitiza kuwa jamii inapaswa kuhakikisha watoto wanacheza katika maeneo yaliyo salama na mashimo yaliyo wazi yafukiwe mapema ili kuepusha madhara kama hayo katika kipindi hiki cha mvua.

Please follow and like us:
Pin Share