Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga
Watoto wawili wa familia moja wanaoishi Kijiji cha Dugushuli, Kata ya Igaga, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamekufa huku sita wakijeruhiwa baada ya kushambuliwa na fisi.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi majira ya saa 7:00 mchana ambapo alieleza fisi huyo alitokea porini akiwa anamkimbiza mtu.
Fisi huyo alikimbilia ndani na kuanza kumjeruhi mama wa watoto akiwa amesimama mlangoni na kisha kuingia ndani kushambulia watoto hao hadi kufa na kujeruhi wengine sita.
Kamanda Magomi aliwataja watoto waliokufa ni Musa Masanja (8) na Stephano Masanja mwenye miezi sita huku miili yao ikiwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kishapu.
Alisema, Felster Tano (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu alijeruhiwa maeneo ya mguuni na hali yake ni mbaya ambapo alikimbizwa hospitali ya rufaa ya mkoa iliyopo Mwawaza kupata matibabu.
“Majeruhi watano wamelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu baada ya kujeruhiwa maeneo mbalimbali kwenye miili yao na hali zao zinaendelea vizuri,” alisema Magomi.
Magomi alisema kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori walimtafuta fisi huyo na kufanikiwa kumuua huku akiiomba jamii kuwa waangalifu na mapori yaliyopo karibu na nyumba zao.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Joseph Mkude alisema matukio ya watu kuvamiwa na fisi yamekuwepo na aliomba jamii na askari wanyamapori kutoka halmashauri kuhakikisha wanajihadhari na wanyama hao wanaoishi jirani na makazi ya watu ili waishi kwa amani.