Katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani, wafanyakazi wanawake kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) wametoa mahitaji mbalimbali kwa watoto wanaopatiwa matibabu ya moyo kwenye Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam Machi 6, 2023.
Wanawake hao pia wamegharimia matibabu ya upasuaji wa moyo kwa watoto watatu wenye uhitaji waliolazwa kwenye Taasisi hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano, WCF, Laura Kunenge amesema.
“Sisi kama wanawake wa WCF tunajua ukimsaidia mama umesaidia familia nzima, tunaunga na wanawake wote Duniani katika kusherehekea siku ya wanawake Duniani na tunaungana na Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha tunaisaidia jamii nzima, tunakuwa karibu na jamii yetu, kama ambavyo tunapenda familia zetu, familia ikiwa bora ni wazi maisha ya watanzania yanakuwa bora.” Alisema.
Amesema msada huo mdogo ni ishara kuwa WCF inaunga mkono juhudi zinazofanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo katika kufanya juhudi za kitabibu lakini wanapopata usaidizi wa mahitaji mbalimbali kutoka kwa jamii kama ambavyo wao wamefanya inaongeza faraja kwa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi hiyo.
“Tunawaombe watoto wetu wapone upesi na wapate nafuu ya haraka.” amesema Laura Kunenge.
Akizungumza mara baada ya kupokea msada huo, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi JKCI,Robert Aloyce Malya, amesema taasisi ya JKCI inapokea wagonjwa wenye uwezo tofauti tofauti, kitendo cha Wanawake wa WCF kutoa msada huo wa hali na mali ni faraja kubwa sana.
“Tunawashukuru sana kwa msada waliotoa, wamekuja na mahitaji mbalimbali kama tunavyoona lakinmi pia wametoa mchango wa fedha kuhakikisha wale wagonjwa ambao wamekuwa na changamoto ya kukidhi gharama za matibabu wanaweza kufanya hivyo, tunashukuru sana.” amesema Malya.
Baadhi ya Akina mama wanaouguza watoto wao wanaopatiwa matibabu ya moyo kwenye Taasisi hiyo wamewashukuru wanawake wwenzao kutoka WCF kwa msada huo wa mahitaji mbalimbali waliopokea.
“Mimi waliniambia mwanao anatatizo la valves kwa hiyo anahitaji kufanyiwa upasuaji, nikasumbuka kutafuta pesa bila mafanikio, lakini nikaambiwa nisubiri, kwa msada huu nawashukuru sana.” Alisema Warda Issa anayetoka Mkoa wa Pwani ambaye mtoto wake wa miaka 12 Abdulrasul Jumanne anasubiri kufanyiwa upasuaji wa Moyo.
Naye Cecilia Muhale ambaye yeye anatoka Bababti Mkoa wa Manyara ambaye mtoto wake wa miaka 12 anasubiri kufanyiwa upasuaji.
“Mwanangu hapati usingizi vizuri, anatatizo la kupumua, nashukuru tangu nifike hapa tarehe 31 mwezi wa 12 angalau anapata nafuu, hapa nasubiri afanyiwe upasuaji, nashukuru sana kwa msada huu na Mungu awabariki.” amesema.
Kwa zaidi ya karne moja watu duniani kote wamekuwa wakiadhimisha Machi 8 kama siku maalum kwa wanawake.