ARUSHA
Na Hyasinti Mchau
Jiji la Arusha limo katika mkakati wa kukabiliana na tatizo la watoto wa mitaani kwa kujenga hosteli maalumu kwa ajili yao.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea eneo linalotarajiwa kutumika kwa ujenzi wa hosteli ‘maalumu’, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmilian Iraghe, amesema serikali imeamua kuja na muarobaini kwa kuwasaidia watoto hao.
“Tunaye mfadhili aliyekubali kujenga hosteli tano ndani ya muda mfupi sana. Mara watoto watakapoondoka mitaani na kuhamia hapa, ataanza kutoa chakula,” anasema Iraghe.
Anasema jiji linaamini kuwa wananchi, hasa wafanyabiashara wa Arusha na sehemu nyingine nchini watajitokeza kuunga mkono juhudi zake.
“Tatizo la watoto wa mitaani si dogo kama watu wanavyolichukulia. Hili ni bomu hatari kwa taifa linaloweza kuleta madhara makubwa kwa jamii nzima bila kujali familia walizotoka kama lisipotatuliwa haraka,” anasema.
Diwani wa Ormoti katika Kitongoji cha NAFCO, Rafael Lemweko, ndiye aliyemkabidhi Iraghe eneo lenye ukubwa wa ekari tano lililopo katika kata hiyo.
Iraghe amemshukuru Lemweko kwa kulitazama tatizo la watoto wa mitaani kwa jicho la kipekee.
Arusha ni miongoni mwa miji mikubwa nchini ambayo imekuwa ikishuhudia makumi kwa mamia ya watoto wakiishi katika mazingira magumu, wakilala mitaroni na mabarabarani bila kujali mvua, jua wala baridi.
Watoto hawa hutoka mikoa mbalimbali jirani na wakiwa jijini hujishughulisha na kuongoza magari wakati wa kuegesha, hivyo kujipatia kipato, huku wengine wakijibanza vichochoroni wakitumia dawa za kulevya huku wakivuta gundi.
“Watoto hawa hawana cha Idd wala Krismasi, nani anawajali? Hawana wazazi wala marafiki wa kuwasaidia, hivyo ni vema tukajitoa kuwasaidia mapema sana,” anasema Iraghe.
Wakati wa Sikukuu ya Krismasi, Meya wa Arusha alizungumza na baadhi ya watoto hao, akala nao chakula cha mchana, kisha kushiriki kufanya usafi.
Watoto wakamwambia wako tayari kuhamia katika eneo maalumu litakakojengwa hosteli ambalo lipo kilometa 15 kutoka jijini Arusha, wakiomba pia kupatiwa nafasi ya kujiendeleza kielimu ikiwa ni pamoja na ufundi wa stadi za maisha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Lemweko anasema Kijiji cha NAFCO kimetenga ekari 19 kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
“Lakini kwa kutambua tatizo la hawa watoto wetu, kwa pamoja tukaamua kutenga ekari 15 kwa ajili yao, na kwa furaha kubwa leo tumemkabidhi meya,” anasema.
Lemweko kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji na wananchi wakati wa kukabidhi eneo hilo, wameweka mipaka na kufanya sala maalumu kwa nia njema kwa taifa.