Na Mwandishi Jeshi la Polisi, Dodoma.
Jeshi la Polisi Nchini limesema Katika kushiriki Maadhimisho ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa mwaka 2024 litashirikiana na Wadau mbalimbali kufanya Maadhimisho hayo katika Kanda Maalum ya Kipolisi Tarime Rorya ambapo Jumla ya watoto 184 waliofanyiwa vitendo vya ukatili wameokolewa na Jeshi hilo.
Akitoa taarifa hiyo Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema kuwa Jeshi la Polisi limeamua kuadhimisha siku hizo 16 katika Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya ambapo Maafisa, Wakaguzi na Askari wengine wanaofanya kazi katika Madawati ya Jinsia na Watoto Tanzania Bara na Zanzibar sambamba na Wakaguzi wa Kata za Tarime Rorya, Serengeti na Butiama ambapo wataweka kambi.
DCP Misime ameongeza kuwa Shughuli watakazofanya wakiwa huko ni pamoja na kutoa elimu juu ya Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji dhidi ya watoto, ikiwepo Madhara ya Ukeketaji.
Aidha Jeshi limebainisha kuwa Watashirikisha Wadau mbalimbali wakiwepo Viongozi wa Serikali za Mitaa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kimila, Wazazi, Viongozi wa Koo na Makundi mengine.
Sambamba na hayo amefafanua kuwa Lengo kubwa ni kuzuia vitendo vya Ukatili wa Kijinsia kwa kiasi kikubwa zaidi wakati na baada ya Maadhimisho haya.
Amesisitiza pia tangu Maadhimisho haya ya siku 16 yalipoanza Novemba 25, 2024 Jeshi la Polisi limefanikiwa kuokoa watoto zaidi ya 184 ambao walikuwa wameandaliwa kukeketwa mwezi wa Disemba 2024 na kwa kushirikiana na wadau wengine wamehifadhiwa sehemu maalum wakati hatua zingine za kisheria zikiendelea.
Msemaji wa Jeshi hilo akasema kuwa Jeshi la Polisi linatoa rai kwa Wananchi wote kutumia Maadhimisho haya kushirikiana kwa dhati ili kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa Kijinsia.