Na Tatu Mohamed, JakhuriMedia
WANAFUNZI na walimu katika Shule ya Msingi ya Kibondemaji iliyopo Mbagala, jijini Dar es Salaam wanachukua hatua za muda mfupi na za muda mrefu, kuzikabili athari za kimazingira katika shule hiyo, zinazoaminika kuwa matokeo mabadiliko ya tabianchi.
Athari kubwa ambazo zimekuwa zikiathiri mazingira ya shule hiyo iliyopo Manispaa ya Temeke, ni mmomonyoko wa udongo ambao hutokea wakati mvua kubwa zinaponyesha na wakati mwingine hali hiyo huathiri mazingira ya kufundishia kwa walimu na yale ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Katika muktadha huo, mara kadhaa wanafunzi hujikuta wakiwa na kibarua kigumu cha kujaza mchanga kwenye viroba na kuvipanga katika sehemu za mazingira ya shule kama hatua za muda mfupi za kukabiliana na mmonyoko ambao unaonekana kuwa na athari kubwa katika mazingira ya shule hiyo.
Baadhi ya wanafuzi na walimu katika shule hiyo wanasema mazingira shuleni hapo yameharibiwa sana na mvua kubwa ambazo hunyesha katika vipindi na nyakati tofauti, kiasi cha kuathiri shughuli za kitaaluma, huku wengine wakieleza kuwapo kwa athari hasa wakati wa kiangazi.
“Tuko kwenye mlima ambao unaelekea bondeni na hakuna kingo za maji, kwa hiyo maji yanakuja mengi sana yanapita katikati ya madarasa na kuweza kuharibu miundombinu,” anasema Aisha Mandalu ambaye ni Mwalimu wa Mazingira katika shule hiyo.
Anaongeza: “Kwahiyo tunapambana nayo kutokana na hali tunaweza kujaza viroba vya mchanga…tukifanya hivyo inaweza kuchukua miezi sita au mwaka lakini baadae hali inarudi tena pale pale.”
Kauli ya mwalimu huyo inaungwa mkono na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo ambao wanasema wakati wa kipindi cha mvua kubwa kunakuwa na mmonyoko katika maeneo ya shule hiyo pamoja na maji kupita kwa wingi.
Akladu Rashid ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita anasema mvua inaponyesha huwalazimu kujaza mchanga kwenye viroba ili kuzuia mmonyoko wa udongo ambao husababisha mashimo na makorongo katika mazingira ya shule yao.
HATUA ZA MUDA MREFU
Kutokana na hali hiyo, shule hiyo imeanza kutekeleza program za muda mrefu za uhifadhi wa mazingira ambazo ni shirikishi kwa wanafunzi, zinazojumuisha uundaji wa klabu za mazingira na upandaji wa miti ili kunusuru mazingira ya shule hiyo.
Mwalimu wa Mazingira, Hamisa Kibire anasema kwa kushirikiana na We World kupitia mradi wa ‘PAMOJA TUNABORESHA ELIMU’, wamekuwa wakitoa elimu kwa wanafunzi kuhusu masuala mbalimbali ya jinsi ya kuhifadhi mazingira na kwamba taasisi hiyo inatoa msaada ndani nan je ya darasa.
“Lakini mbali zaidi kutokana na mabadiliko ya elimu na Teknolojia wametusaidia kutufundisha mifumo mbalimbali na kwa upande wa mazingira wametuletea vifaa vya chooni kwa wanafunzi, vifaa vya kuhifadhia taka pamoja na kutujengea tanuri la kuchomea taka,” anasema Kabire naa kuongeza:
“Pia WeWorld wanatoa msaada kwa wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu na wale wazito kuelewa darasani wameandaliwa darasa lao na kumekuwa na walimu wanawafundisha”.
Mwalimu huyo anasema pia wamewasaidia namna ya ufundishaji, uandaaji wa zana, vifaa vya shule pamoja na mafunzo na stadi mbalimbali. “Kadhalika wametujengea madarasa, ofisi ya walimu pamoja na kutupatia madawati kwa sababu kuna wanafunzi walikuwa wanakaa chini.
“Tunaishukuru We World kwa msaada mkubwa ambao wametupatia kwa muda mrefu na tunawaomba waendelee kutusaidia katika mambo mbalimbali ili kuhakikisha tunaendelea kutoa elimu,” anassisiti za Mwalimu Kibire.
ELIMU YA MAZINGIRA
Asma Ismail ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano anasema wamekuwa wakifundishwa mambo mbalimbali kuhusu mabadiliko ya Tabianchi pamoja na athari zake.
“Walimu wanatufundisha jinsi ya kutunza mazingira, kupanda miti na kuacha kukata miti ovyo. Lakini pia wanatufundisha masuala ya usafi na kuacha tabia ya kuchezea maji machafu ili kujiepusha na magonjwa kama vile kipindupindu,” anasema Asma.
Naye Mwanafunzi wa darasa la sita, Kaini Saidi anasema wanajitahidi kupambana na mabadiliko ya Tabianchi ambapo wanaendelea kuotesha miti katika maeneo mbalimbali ya shule yao.
Maelezo yao yanaungwa mkono na Mwalimu wa Mazingira, Malandu anasema: “Tunawapa wanafuzni elimu maana yasingekuwa mawe pangekuwa korongo. Nawaomba wafadhili waweze kutusaidia kuweka kingo za kupitishia maji.”
Anaongeza: “Kauli mbiu yetu ni kwamba kama itatokea ukakata mti (ikiwa kuna ulazima wa kukatwa) basi ihakikishwe imepandwa miti. Lakini kwa sababu bado tuna maeneo mengi yaliyo wazi tuendelee kupanda miti na kuhakikisha inakua ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
“Kwahiyo katika hilo watoto ni washiriki wazuri, sisi ni kusimamia tu hilo… hivi karibuni tulipata miti mingi kutoka CRDB na baada ya kuipokea kuliiotesha. Tumewasimamia watoto na kuwagawia miti, ikibidi waite hata majina yao lakini wahakikishe imepata maji, mbolea kwa ajili ya kuiwezesha kukua,” anasema Mwalimu Malandu.
Hatua za elimu shirikishi kwa wanafunzi ni jibu la kile kilichojiri Oktoba 2023 nchini Tanzania, ambako zilisikika sauti za watoto na vijana zikitaka mamlaka na jamii kwa ujumla kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi, huku wakipendekeza elimu kuhusu suala hilo kuingizwa katika mifumo ya ufundishaji.
Sauti hizo zilitoka katika hitimisho la mashauriano yaliyoongozwa na UNICEF Tanzania, kwa ushirikiano na Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Nchini Tanzania, karibu nusu ya idadi ya watu wana umri chini ya miaka 18.
Katika ripoti inayoitwa: “Watoto kwa Hatua za Mabadiliko ya Tabianchi: Sauti kutoka Tanzania” watoto hao walisisitiza umuhimu wa kuingiza mtazamo wa wao katika suluhisho za mabadiliko ya tabianchi kwa maelezo kwamba kudi hilo ndilo linaloathiriwa zaidi na mabadiliko huo.
Sauti hizo za watoto na vijana, zilizokolezwa kupitia utafiti wa U-Report uliohusisha washiriki zaidi ya 12,000 katika mikoa ya Mbeya, Kigoma na Zanzibar zinaonyesha hitaji la haraka la elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Matokeo ya ripoti yanaonyesha kuwa asilimia 60 ya vijana waliyohojiwa waliona kuwa shule zao hazishughulikii ipasavyo mzozo wa tabianchi, huku asilimia 80 wakisema elimu kama hiyo ni muhimu kwa mustakabali endelevu.
ATHARI KIBONDEMAJI
Mwanafunzi wa darasa la sita, Akladu anasema: “Inaponyesha mvua kubwa hapa shuleni hua tunateseka sana. Yaani wanafunzi wanadondoka ovyo kutokana udongo kumomonyoka na kuacha mashimo.
Anabainisha kuwa yeye ni mmoja wa waathirika wa mmonyoko huo kwani ameshawahi kuanguka na kuumia mkono. “Kuna siku nilianguka na kuumia mkono, hata hivyo walimu walinisaidia wakanipa huduma ya kwanza nikaendelea vizuri,” anasema Rashid.
Mwingine ni Hamisa Japhet ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano anasema pia mvua zinaponyesha kubwa shuleni hapo hua wanakaa muda wote darasani kutokana na maji kupita kwa wingi.
“Hapa ni kama njia ya maji, yanajaa sana kwahiyo hua tunatulia tu darasani, ingawa kuna wanafunzi wengine hua wanayafata maji hayo kuyachezea na kuogelea,” anasema Hamisa.
Kwa upande mwingine, hali huwa tofauti wakati wa kiangazi ambapo pia hali huwa siyo rafiki wanafunzi. Kaini Saidi ambaye ni Mwanafunzi wa darasa la sita anasema wakati wa jua kali hukabiliwa na joto kali madarasani, huku mimea katika shule hiyo ikikauka.
“Yaani kunakuwa na vumbi sana ambalo linaingia hadi darasani, tunashindwa kucheza kwasababu ya jua kali sana pamoja na hilo vumbi,” anasema Kaini.
Mwalimu Mandalu anasema:”Hii ni changamoto inayotusumbua sana, kuna wanafunzi wanaanguka na hata kuna mwalimu aliwahi kuanguka na kuvunjika mguu kutokana na mazingira haya. Hapo maji yakipita udongo unaondoka yanabaki mawe, ni hatari kwa watoto.”
Hali hii ya athari za mvua na joto kali katika Shule ya Msingi ya Kibondemaji, inatokea wakati Dunia ikiwa katika harakati za kukabiliana na mabadiliko makubwa ya tabianchi ambayo yanatajwa kuwa na athari kubwa kwa watoto na vijana.
Katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP29), uliofanyika Novemba 11, 2024 Baku nchini Azerbaijan, takwimu za Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) zilizoonesha kuwa takribani watoto Bilioni 1 wako hatarini kutokana na mabadiliko ya Tabianchi.
Mwaka 2021 UNICEF walitoa taarifa kwamba vijana na watoto katika baadhi ya nchi duniani walikuwa katika hatari zaidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, yakitishia afya zao, elimu, na ulinzi, na kuwaweka kwenye hatari ya magonjwa.
Ripoti hiyo “Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi ni mgogoro wa haki za mtoto: Kutambulisha hatari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto” ulikuwa ni uchambuzi wa kwanza wa kina unaobaisha hatari ya mabadiliko ya tabianchi kwa mtazamo wa watoto.
Kadhalika katika ripoti zake kadhaa zilizofuata, UNICEF inaziweka nchi kutokana na kiwango chake cha hatari ya athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine ya kimazingira kwa watoto kama vile vimbunga na ongezeko la joto, na vile vile kuathiriwa kwao na majanga hayo, kwa misingi ya ufikiaji wao wa huduma muhimu.
“Na watoto hawa wanakabiliwa na kukumbwa na hatari mchanganyiko za mabadiliko ya tabianchi na majanga mengine ya kimazingira na hivyo kuwaweka katika hatari kubwa kwa sababu ya kutokuwa na huduma muhimu na za kutosha, kama maji na usafi wa mazingira, huduma za afya na elimu,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.