Watoto wawili ambao ni mapacha wenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita wamepoteza maisha baada ya kutumbukia kwenye lambo la maji yaliyokuwa yametuama mita chache kutoka kwenye nyumba yao wakati wakicheza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa,amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo lilitokea Aprili 23,2023, majira ya saa 8, mchana,katika kijiji cha Runele, Kata ya Hungumalwa, Tarafa ya Nyamilama Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza.
Amesema kuwa watoto hap ambao wote walikuwa ni wa kiume ambao wazazi wao ni Jimuku Rozalia (28) na Avelina Nkwaya (20) wote wakulima na wakazi wa kijiji cha Runele.
Amewataka marehemu hao kuwa ni Kulwa Jimoku na Doto Jimoku, wote wakiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi sita, ambapo walikutwa na umauti huo wakati wakicheza nje kidogo ya nyumba yao ambako kulikuwa na lambo la maji.
Kamanda amesema kuwa watoto hao walitumbukia kwenye lambo hilo ambalo lipo mita 30 kutoka kwenye nyumba yao na limetengenezwa na wazazi wao kwa lengo la kuhifadhia maji ya kunyweshea mifugo yao.
Kamanda amesema kuwa chanzo cha tukio hilo ni michezo ya watoto na uzembe wa wazazi kutokuwa makini kwani wakati tukio linatokea wazazi wao walikuwa wanaendelea na shughuli za kilimo nyumbani hapo.
Miili ya Kulwa na Doto imefanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.
Pia alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini kwa kuwalinda watoto hususani katika kipindi hiki cha mvua ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.