Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Longido

Serikali imeombwa kufanya maboresho ya sheria ya Ukatili wa Kijinsia ili kutoa adhabu kali kwa wanaokeketa watoto baada ya kubainika kuibuka mbinu mpya ya kukeketa watoto wa kike wakiwa chini ya miaka miwili wilayani Longido,mkoa Arusha.

Wakizungumza katika kongamano la kupinga ukeketaji wilaya ya Longido lililoandaliwa na Taasisi ya wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni(MAIPAC) kwa kushirikiana na SAVVY Media group , maafisa wa serikali na wanaharakati wa kupinga ukeketaji na wanawake wa longido walisema bila kuwepo sheria kali vitendo vya ukeketaji vitaendelea.

Mkuu wa Dawati la Jinsia katika Kituo cha Polisi wilaya ya Longido,Coplo Fransisca Lucas alisema sheria ya kupambana na matukio ya ukatili ni muhimu iboreshwe ili iwe kali.

“Tukiangalia kifungu cha 89(a) cha sheria ya kukabiliana na makosa ya kijinsia, adhabu inayotolewa ni ndogo sana ambayo na kifungo kisichozidi mwaka mmoja au faini isiyodhidi milioni moja kwa ambaye atatiwa hatiani kwa makosa haya”alisema

Alisema Jeshi la polisi kwa kushirikiana na Maafisa Ustawi wa Jamii na maafisa wa Afya wamekuwa wakitumia gharama kubwa kufatilia watuhumiwa wa ukeketaji lakini baada ya kukamatwa wamekuwa wakipigwa faini ndogo ikiwepo faini ya 100,000 tu kwa wanaotiwa hatiani.

Kaimu Mganga mkuu wa wilaya ya Longido Dk James Masokola alisema vitendo vya ukeketaji ambavyo vimekuwa vikisababisha madhara makubwa kwa watoto wa kike ikiwepo vifo vinaendelea kutokana na adhabu ndogo kutolewa licha ya elimu kutolewa.

“Watoto wanaokeketwa wanatokwa na damu nyingi,wanawake wakiokeketwa wakati wa kujifungua wanatokwa na damu nyingi na kupata madhara nakubwa hivyo hakuna sababu sababu yoyote ya kukeketawatoto”alisema

Mkurugenzi wa MAIPAC Mussa Juma alisema ni tabia ya kukeketa watoto wadogo Longido inapaswa kukomeshwa kwa kutolewa adhabu kali kwa wanaowakeketa watoto na wazazi waliotoa idhini.

Juma aliwaomba viongozi wa Mila ya Kimasai maarufu kama Laigwanani kuwa mabalozi wazuri wa kupinga ukeketaji kwani serikali tayari imepiga marufuku vitendo hivyo.

Afisa Ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Longido,Leonia Ndunguru alisema vitendo vya ukatili wanawake na watoto vimeongezeka mkoa Arusha n kufikia asilimia 43 kwa mwaka kutoka asilimia 41 miaka mitatu iliyopita.

“Lazima tukomeshe matukio ya kukeketa watoto wadogo wanakeketwa na hata karibuni tumepokea matukio mawili sasa lazima tukomeshe na alipongeza MAIPAC na Savvy kuandaa mdahalo huo”alisema

Mkazi longido Marykinoi Olkendanyi alisema ukeketaji umekuwa na madhara kwani yeye amekeketwa na alipata ugonjwa wa festula wakati wa kujifungua na bila jitihada za maafisa wa afya asingepona.

Alisema chanzo cha watoto kukeketwa ni wanaume wanapotaka kupokea mahali ili watoto waolewe lakini wanawake wanafursa ya kuzuia ukeketaji bila wanaume kujua kwani wao ndio hukaa ndani na Ngariba.

Mary laizer Mwelimishaji kupinga ukeketaji alisema yeye ni mhanga wa ukeketaji lakini ameweza kuzuia watoto wake kukeketwa na amewavukisha rika bila kukeketwa.

Afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la UN Women , Beatrice Makenge ambaye alishiriki mdahalo huo uliokuwa sehemu ya maadhimisho ya kimataifa ya kupinga ukeketaji duniani,aliwataka wazazi kuacha kukeketa watoto wao.

Alisema vitendo vya ukeketaji licha ya kuathiri afya ya watoto wa kike pia inawaondolea hali ya kujiamini katika maisha yao na kujiona wapo dhaifu.

Meneja SAVVY Media Borry Mbaraka alisema wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwepo MAIPAC,Serikali,Mashirika ya ndani na nje ya nchi kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wa kike.

Afisa Maendeleo wa halmashauri Longido,Monica Wambura na Mkurugenzi wa Shirika la Tembo, Paulina Sumayani walisema jitihada za pamoja baina ya serikali na Asasi za Kiraia zitasaidia kukomesha ukeketaji Longido.

Katika mdahalo huo, walikubaliana kushirikiana kupinga ukeketaji na kuwa mabalozi katika maeneo yao kutoa elimu ya kupinga ukeketaji na kushiriki kuhamasisha adhabu kali kutolewa kwa wanaokeketa watoto.