Na Stela Gama – JKCI
Watoto 23 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo katika kambi maalumu ya matibabu ya moyo kwa watoto inayofanyika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo maalumu ya upasuaji inafanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na wenzao wa kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia.
Akizungumzia kuhusu kambi hiyo Mkurugenzi wa upasuaji na daktari bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi wa JKCI Dkt. Angela Muhozya alisema kambi hiyo ni muendelezo wa ushirikiano mzuri uliopo na wenzao wa Saudi Arabia katika kutibu watoto wanaosumbuliwa na matatizo ya moyo.
“Mpaka kufikia leo hii ni siku ya tano tangu kambi hii imeanza na tumeweza kuwafanyia upasuaji watoto wapatao 23 na tunatarajia kuwafanyia watoto 40 na kwa wale waliofanyiwa upasuaji siku za mwanzo wanaendelea vizuri, wamesharuhusiwa kutoka katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) wako wodini wanaendelea na matibabu”, alisema Dkt. Angela.
Wataalamu wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kilichopo nchini Saudi Arabia wakifanya upasuaji wa kurekebisha mishipa ya damu ya moyo wa mtoto ambayo haijakaa katika mpangilio wake wakati wa kambi maalumu ya upasuaji wa moyo inayofanyika JKCI.
Dkt. Angela alisema wameweza kumfanyia upasuaji wa moyo mtoto mdogo mwenye umri wa siku tatu ambaye mishipa yake ya moyo haikuwa katika mpangilio wake sahihi kama inavyotakiwa kuwa na kwa sasa anaendelea vizuri.
“Tunawashukuru wenzetu wa Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu kwa kujitoa kwao kwani licha ya kutoa huduma za matibabu pia wametupatia vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 ambavyo vinatumika katika kufanya upasuaji huu wa moyo unaoendelea ”, alisema Dkt. Angela.
Kwa upande wake daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu kutoka Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu Mohammad Shihata alisema kambi hiyo imekuwa ikidhaminiwa na Mfalme Salman wa nchini Saudi Arabia kuwawezesha watoto kupata matibabu na kubadilishana ujuzi na madaktari wa JKCI.
Dkt. Shihata alisema timu nzima ya watu 26 kutoka nchini Saudi Arabia ambao ni waatalamu wa usingizi, waendesha mashine za moyo, wauguzi na madaktari wameshiriki katika kambi hiyo ili kuhakikisha watoto wengi wanafanyiwa upasuaji wa moyo.
“Hii ni siku yetu ya tano na ni mara ya yangu ya saba kuja hapa nchini kufanya upasuaji wa moyo kwa watoto, siku zote tumekuwa tukipokea ushirikiano mzuri kutoka kwa madaktari wa JKCI katika kufanikisha utoaji wa huduma hii”, alisema Dkt. Shihata.
Kwa upande wa wazazi ambao watoto wao wamefanyiwa upasuaji wa moyo katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kuokoa maisha ya watoto hao wenye matatizo ya moyo.
Zainabu Mussa kutoka mkoani Kigoma mzazi ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji katika kambi hiyo alisema mtoto wake alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa ya moyo tangu alipomzaa na kumpeleka katika hospitali mbalimbali bila ya mafanikio.
“Mwanangu alipofikisha umri wa miezi mitano hakuwa anaweza kukaa, anakosa nguvu na kutoka jasho kwa wingi lakini hatukuweza kugundua mapema kama anashida ya tundu kwenye moyo hadi pale wataalamu wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) walivyofanya kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo mkoani Kigoma”, alisema Zainabu.
“Namshukuru sana Mungu mara baada ya mtoto wangu kupatiwa matibabu anaendelea vizuri, nawashukuru pia wataalamu wa JKCI kwanhuduma zao nzuri na ningependa kuwashauri wazazi wasisite kuwapeleka watoto hospitali endapo wataona watoto wao hawakui vizuri”, alisema Zainabu.
“Mwanangu aligundulika kuwa na shida ya moyo wakati anatibiwa katika Hospitali ya mkoa Temeke baada ya kupewa rufaa ya kuja JKCI aligundulika kuwa na tundu kwenye moyo, namshukuru Mungu amefanyiwa upasuaji na anaendelea vizuri”, alisema Zuhura Mkamba.