Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Watoto zaidi ya 1500 wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo wanatarajia kunufaika na matibabu ya maradhi hayo kutoka kituo cha matibabu ya magonjwa moyo nchini JKCI.
Hatua hiyo imekuja kupitia harambee maalumu ya kuchangia matibabu kwa watoto wa kitanzania wanaokabiliwa na changamoto hiyo.
Katika harambee hiyo iliyoongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt: Jakaya Mrisho Kikwete ilihusisha wadau mbalimbali wa taasisi binafsi na mashirika ya kiserikali kuona namna gani wanaweza kuchangia kufanikisha gharama zitakazofanikisha matibabu ya moyo kwa watoto wenye uhitaji.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt: Jakaya Kikwete ameipongeza taasisi hiyo ya moyo kwa kutambua changamoto iliyopo kwa watoto wadogo wa kitanzania pamoja kuelezea kuwa dira kuu ya kuanzishwa kwa kituo hicho huku lengo lake kuu ni kusaidia watanzania kupata matibabu ya moyo ndani ya nchi ili waweze kuepukana na gharama kubwa za matibabu nnje ya nchi.
“Hapo awali kulikuwa na changamoto ya huduma ya matibabu ya moyo nchini, changamoto hiyo tuliigundua na tukasema kuwa hakuna ulazima wa kwenda kutibiwa nnje ya nchi .Shabaha yetu ilikuwa ni kutibu watu wetu wa ndani ili tupunguze ulazima wa watu wetu kupelekwa nnje.”
Aidha Dkt: Kikwete aliongeza kwa kuzipongeza serikali za awamu ya tano na awamu ya sita kwa kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa kituo hicho katika utoaji vifaa vya kisasa pamoja mahitaji muhimu ya kituo hicho.
“Natoa pongezi kwa serikali ya awamu ya tano na sasa awamu ya sita kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwa kituo hicho. Taasisi hii imezidi kuimarishwa kwa kupatiwa vifaa vya kisasa na kuwezeshwa kwa mahitaji mengine ya vitendea kazi.” Alisema.
Kwa upande wake pia Mkurugenzi mkuu wa kituo hicho cha JKCI, Dr: Peter Kisenge nae ameelezea juu ya mchakato mzima wa kuja na wazo hilo la uchangishwaji wa fedha kusaidia watoto hao wenye uhitaji huku akitaja idadi ya watoto 500 kati ya 1500 kuwa wanahitaji matibabu ya haraka zaidi ili kuokoa maisha yao.
Kampeni hiyo imefanyika pia kwa ushirikiano wa timu wa timu ya madaktari wa moyo barani Afrika ambao walikuwa wakiunga mkono kwa asilimia kubwa zoezi hilo.