Na Deodatus Balile

Tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aitangazie dunia kwamba kwa sasa Tanzania imeamua kupambana na janga la corona, inavyoonekana kampeni hiyo inafanywa na Rais peke yake huku baadhi ya wateule wake wakiigiza.

Hii inatokana na ukweli kwamba haionekani nia ya dhati ya baadhi ya wateule wake kushirikiana naye katika kuhakikisha kampeni ya kupambana na janga la corona inakuwa endelevu na kila mmoja anashiriki kwa dhati katika kuhakikisha nchi inajilinda dhidi ya janga hilo.

Nasema hivi kwa sababau nimekuwa nikifuatilia kwa karibu namna ambavyo Rais alivyojitoa mhanga kupambana na janga la corona na muda wote katika kazi zake amekuwa mstari wa mbele kuhimiza wananchi kutambua uwepo wa ugonjwa huo na kutoa wito kwa kila mmoja kuchukua tahadhari katika kuhakikisha anajilinda.

Tunampongeza Rais kwa kutambua ukubwa wa tatizo hilo na ndiyo maana mara tu baada ya kuingia madarakani alianza kwa kukubali uwepo wa ugonjwa wenyewe na baada ya hapo akahakikisha haachi kuvaa barakoa na kufuata itifaki zote za kiafya kuhusiana na ugonjwa huo.

Bila kusita Rais aliunda timu ya wataalamu kuhusu corona na walikuja na mapendekezo thabiti kuhakikisha Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani inachukua hatua katika kukabiliana na kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo ambao hivi sasa umeathiri watu wengi na inawezekana hakuna familia isiyoguswa kwa namna moja ama nyingine, licha ya serikali kutoa takwimu kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), ambazo Watazania wengi hawazifahamu.

Sitanii, baada ya mapendekezo ya timu ya wataalamu iliyoundwa na Rais, pamoja na mambo mengine mengi, timu hiyo ilipendekeza matumizi ya chanjo, ambapo serikali kupitia kwa Rais Samia haikupuuza, kwani iliagiza chanjo na kuletwa nchini.

Baada ya chanjo kuletwa Rais alijitokeza hadharani na kuwa wa kwanza kupata chanjo hiyo, huku akitamka maneno mazito kwamba yeye ni Amiri Jeshi Mkuu, Rais, mama wa watoto  wanne, mke na bibi wa wajukuu kadhaa, lakini ameamua kuchanjwa baada ya kujiridhisha kwamba chanjo ni njia salama katika kujikinga dhidi ya ugonjwa wa corona au ukali wa ugonjwa huo pale unapoupata.

Sitanii, maneno haya ya Rais hayakuwa maneno rahisi, bali lilikuwa ni kama agizo kwa wateule wake kwamba, yeye amechanjwa na kilichobaki ni kwao kuuchukulia ugonjwa huo kwa uzito wa hali ya juu katika kuhakikisha wanaungana naye kufanya kampeni kubwa na mwisho wa siku kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa huo.

Sitanii, inasikitisha kuona kazi hiyo ameachiwa Rais peke yake licha ya maigizo machache yanayofanywa na baadhi ya wateule wake, hasa pale wanapokuwa kwenye kazi mbalimbali. Lakini kiukweli haionyeshi kama wateule wake wapo tayari kupambana na ugonjwa wa corona au bado wanatembea na dhana ileile kwamba Tanzania hakuna corona.

Tunawashuhudia baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya umma na viongozi wa kada tofauti wakiwa katika kazi mbalimbali katika maeneo yao bila kuchukua tahadhari yoyote ya ugonjwa wa corona. Huu ni usaliti!

Mfano rahisi ni suala la chanjo. Hebu fikiria chanjo milioni moja zilizoletwa Tanzania ambayo inakadiriwa kuwa na watu zaidi ya milioni 60, hadi sasa kwa mujibu wa Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, waliochanjwa ni watu 460,000 tu!

Sitanii, hii inaashiria wazi kuwa viongozi wengi wa serikali hawajachanjwa, watumishi wa afya ambao ndio wanatakiwa wawe mfano hawajachanjwa, viongozi wa chama anachotoka Rais, kikiwa na wanachama zaidi ya milioni nane, nao wengi hawajachanjwa. 

Hali hii inaonyesha dhahiri shahiri kwamba wakuu wa mikoa waliopewa jukumu la kumwakilisha Rais katika maeneo yao hawafanyi kazi hiyo vizuri.

Pamoja na kwamba chanjo hiyo ni hiari, lakini kwa viongozi kama Rais ameshachanjwa, waziri mkuu amechanjwa, wakuu wa vyombo vya dola wamechanjwa, tusingetegemea kukuta hata mtumishi mmoja wa serikali ambaye hajachanjwa, kwani kwa kufanya hivyo ni kushindwa kuiheshimu mamlaka inayoongoza. 

Vilevile nisamehe msomaji, sifahamu ni mawaziri wangapi waliochanjwa hadi sasa. Sikuona wakichanjwa na sisikii wakitangaza iwapo wamechanjwa.

Sitanii, tusingetegemea kuona wakuu wa mikoa wanashindwa kumuelewa Rais kwanini amechanjwa na wao wafanye nini kuhakikisha wanawasimamia watumishi waliopo katika maeneo yao ya serikali za mitaa kuwa wanapata chanjo na badala yake watu wanabembelezana tu. 

Hebu mpigie simu Mkurugenzi wa BRELA, muulize ilikuwaje wafanyakazi wote wa BRELA wamechanjwa? Ametumia mbinu ipi? Kupanga ni kuchagua.

Inashangaza kumuona mkuu wa mkoa anaibuka eti amefanikisha uchanjaji kwa asilimia 90. Ukiangalia watu waliochanjwa katika mkoa wake wenye watu zaidi ya milioni mbili, unakuta hata watu 50,000 hawafiki. Huu ni usanii wa wazi wazi na kushindwa kumuelewa aliyewateua.

Sitanii, kwa viongozi wanaojielewa na kama kweli wanamuelewa aliyewateua, kuamini kwamba chanjo ni jambo la hiari, ni kutojitambua. 

Rais anatumia diplomasia. Chanjo si jambo la hiari, ni jukumu la kila anayeamini kwamba anamtii Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na anaipenda afya yake, kuhakikisha anawaongoza Watanzania katika eneo lake wachanjwe ili kudhibiti janga la corona.

Ukiachana na chanjo, nenda katika ofisi za serikali uone hali ilivyo. Ofisi nyingi hakuna anayevaa barakoa, wala huyakuti maji tiririka. 

Hii inaonyesha wazi kabisa waliopewa dhamana ya kuongoza taasisi hizo hawamheshimu Rais. Kama wangekuwa wanamheshimu na kujielewa, ofisi za serikali zingekuwa mstari wa mbele katika kusimamia masuala ya msingi yanayohusu corona.

Mimi ninafikiri ni wakati wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi katika ofisi zote za serikali na kupeleka taarifa kwa Rais ya hali ilivyo na wale ambao hawataki kutambua kuwa corona ipo, waondolewe, kwani kushindwa kutekeleza masharti ya kuzuia corona kwa kiongozi aliyeteuliwa na Rais huo ni uuaji.

Sitanii, corona ipo na inaua. Katika nchi yetu kutokana na dharau, viongozi ambao wamepewa jukumu la kumsaidia Rais wengi hawako makini kuhusu uwepo wa ugonjwa huu, hali inayochangia hata wananchi wanaopata huduma kwenye ofisi za serikali nao kupuuza.

Kama viongozi wangekuwa tayari kuonyesha mfano kwa vitendo tungeona wananchi pia wakichukua hatua, lakini kilichopo hivi sasa ni kwa baadhi ya wateule wa Rais Samia kuendelea kuamini kwamba corona imepeperushwa na maombi ya kipindi kile ya siku tatu.

Sitanii, kama umeteuliwa na Rais Samia na ofisi yako watumishi wako hawajachanjwa, watu hawavai barakoa, hakuna maji tiririka, wala hakuna taratibu zozote za kiafya kuhusiana na kujikinga dhidi ya ugonjwa huo, ikiwamo kufanya vikao kwa kuzingatia umbali wa mtu na mtu, wewe hautoshi kuongoza ofisi ya umma, ni bora utoke mwenyewe.

Wizara ya Afya pia ijitathmini, kwani ni aibu kwa wizara hiyo kukuta watumishi wake wengi wakiwamo waganga wakuu wa wilaya na waganga wakuu wa mikoa hawajachanjwa. Huo ni usaliti na ni lazima Waziri wa Afya na wasaidizi wake wajitathmini.

Sitanii, juhudi zinazoonekana kuchukuliwa sasa na wizara hiyo ni kutokana na ujio wa fedha za wafadhili ambazo tusipoangalia fedha hizo zinaweza kuliwa huku mafanikio katika kudhibiti ugonjwa huo na watu kupata chanjo yakiwa ni sifuri.

Mwisho, Mheshimiwa Rais, naomba kukuuma sikio. Huko mitaani wanasema Waziri wa Afya na naibu wake waliwaambia watu wasichanjwe. Leo wamegeuka jiwe la chumvi wanataka watu wachanjwe. 

Watanzania wanaomba hawa uwapangie kazi nyingine kama kweli unataka ufanisi katika hili suala la chanjo. Nakiri sina ugomvi nao, na sijawahi kukutana hata na mmoja wao uso kwa uso, ila haya yanasemwa.

Nafahamu hili limo ndani ya mamlaka yako, lakini kwa wananchi wanaokupenda kwa jinsi unavyotuongoza bila kutufokea, wanaona waziri na naibu waziri historia ya matamshi yao inatia doa nia yako njema ya kupambana na corona. 

Naomba nikutakie wiki njema na usisahau kuwaambia mawaziri wa wizara nyingine kila wanapofanya mkutano wasisahau kutaja ajenda ya corona, hasa wananchi kuchanjwa, kwa nia ya kujikinga wao binafsi, familia zao na taifa kwa ujumla. Mungu ibariki Tanzania.