Kwa mwongo zaidi ya mmoja, nimekuwa miongoni mwa waandishi waliosimama kidete kutetea uhai wa wanyamapori na misitu.

Mathalani, tumeamini kuwa bila Loliondo, Hifadhi ya Taifa Serengeti (SENAPA) haipo! Bila Loliondo, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) haipo; wala Masaai-Mara iliyopo Kenya, haiwezi kubaki salama. Loliondo ndiyo roho ya hifadhi hizi zote.

Kwa miaka zaidi ya 10 yamesemwa mengi na watu wachache wenye hila waliojipenyeza kwenye mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) kwa mgongo wa kutetea maslahi ya watu wa jamii ya wafugaji (Wamaasai) ilhali ukweli ukiwa kwamba kilichowaongoza kufanya hivyo ni maslahi yao tu.

Kwa miongo zaidi ya miwili ‘viongozi na watawala’ wa Loliondo wamekuwa ni NGOs kama TPCF, PWC, UCRT, NGONET, PALISEP, PINGOS FORUM, IRK-RAMAT n.k., huku zikiungwa mkono na wawezeshaji wao kama kampuni ya AndBeyond na asasi ya Dorobo Safaris. 

NGOs zimekwamisha maendeleo ya Loliondo kwa muda mrefu kwa sababu viongozi wengi katika Wilaya ya Ngorongoro ndiyo hao hao waliomo kwenye NGOs hizi. 

Loliondo imekuwa uwanja wa mapambano kwa sababu viongozi wengi, ama si raia wa nchi hii, au ni mamluki wa wageni.

Septemba, 1961 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitoa maneno yaliyokuja kuitwa ‘Ilani ya Arusha’. Hapa tunaona kuwa hata kabla ya Uhuru, Mwalimu alishatambua umuhimu wa kulinda wanyamapori, na hivyo akatoa mwelekeo (Ilani) ya kuuhifadhi urithi huu hata baada ya kuwa na Tanganyika huru. Mwalimu alisema maneno haya:

“Kudumisha uhai wa wanyamapori wetu ni suala linalotuhusu sana sisi sote katika Afrika. Viumbe hawa wa porini pamoja na mapori wanamoishi siyo tu kwamba ni muhimu kama mambo ya kustaajabisha na kuvutia, bali pia kwamba ni sehemu muhimu ya maliasili yetu na ustawi wa maisha yetu katika siku za baadaye.

Kwa kukubali dhamana ya kuhifadhi wanyama wetu tunatoa tamko la dhati kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu na watoto wetu wataweza kufaidi utajiri na thamani ya urithi huu.

Kuhifadhi wanyamapori na mapori waishimo kunahitaji utaalamu maalumu, watumishi waliofunzwa pamoja na fedha. Tunatazamia kupata ushirikiano kutoka kwa mataifa mengine katika kutekeleza jukumu hili muhimu. Kufanikiwa au kushindwa kwa jukumu hilo kutaathiri siyo tu Bara la Afrika pekee, bali ulimwengu mzima.”

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuchoka kuonya juu ya athari zinazosababishwa na kuua wanyamapori.

Akizungumza na viongozi wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na wa Serikali mkoani Kilimanjaro Agosti 10, 1975 alieleza makosa yanayowagharimu watu wa mataifa ya Ulaya na Marekani kutokana na kuua wanyamapori na kuharibu misitu. Mwalimu alisema:

“Ni vizuri kujifunza kwa wenzetu waliotangulia. Na wakati mwingine ni kujifunza kutokana na makosa yao. Wenzetu waliotangulia tunaowasema zaidi ni wale wa nchi zilizoendelea sana hasa za Ulaya na Amerika Kaskazini.

Wamefanya makosa mawili makubwa – wao wanajua, sisi hatujui. Wao wanajua kwa sababu wameyafanya makosa hayo, sisi kwa sababu hatuyafanya hatujui kwamba ni makosa. Moja mtashangaa nikilitamka. Wameharibu sana nchi zao kwa kitu wanachokiita maendeleo. Wameua vi-nyama vingi sana vilivyoumbwa na Mwenyezi Mungu – vingi. Wameua vyote. Hawana tena makundi makubwa makubwa ya wanyama kama tuliyonayo katika Afrika na hasa katika Tanzania. Hawana kabisa. Sasa wao wanajua kwamba wamefanya makosa, na wanakuja huku wanatwambia; ‘Sisi tumefanya makosa, tumeua wanyama wetu wote tumemaliza, tafadhalini msiue wanyama wenu.’ Sisi tunawaona kama wajiiinga wanapotuambia hivyo. Lakini wao wanajua kosa kubwa la kufuta wanyama na kuwamaliza; na kukatakata misitu yao na kuimaliza. Wanajua kosa walilolifanya na wanatuomba tusilifanye kosa hilo. Sasa wanakuja kwa wingi, ndio hao mnawaita watalii. Wanakuja kwa wingi kuja kuona wanyama. Wewe unamshangaa huyu mtu mzima anatoka kwao mbaaaaali kuja…anatoka kwao mbaaaali, analipa hela kuja kuona tembo, kwanini. Ana akili, hana akili! Ni kwa sababu ana akili ndio maana anatoka kwao mbaaali sana, analipa fedha anakuja kuona tembo. Angekuwa hana akili asingekuja. Anajua faida ya kuwa na ma-tembo, na ma-simba, na ma-nyati, na ma-chui, na ma-pundamilia katika nchi hii, lakini kwao wameshafuta. Sasa wanaanza kutuomba, wengine wanaanza kutuomba tuwauzieuzie angalau wafufuefufue, lakini kufufua si jambo jepesi. Ukishaifuta misitu, kuifufua na kuweka wanyama waishi kama walivyokuwa zamani vigumu sana, kwanza hali yake ile ni tofauti. Huwezi kuifufua, vigumu sana. Wala hawajui ilikuwaje hata waweze kuifufua. Sasa nasema wanatushawishi- Wazungu wanatushawishi katika jambo hilo ambalo hatujafanya kosa, tusifanye kosa. 

Serikali ya Tanzania imekubali, nadhani wananchi wanaanza kukubali kutofanya kosa hilo lililofanywa na wenzetu. Tuhifadhi wanyama wetu na tuhifadhi misitu yetu. Tusivuruge-vuruge mazingira ambayo tumeyarithi, na kwa kweli hatujui yamechukua muda gani hata yakawa hivyo; halafu tunafika sisi tunaita maendeleo tunavuruga vuruga, tunaharibu; tunaua wanyama, tunakata miti. Matokeo yake hatuwezi kuyajua.” mwisho wa kunukuu.

Wanaomuenzi Baba wa Taifa hawana budi kuyazingatia na kuyatekeleza maneno haya kwa vitendo. 

Katika safu hii, Toleo Na. 275, chini ya kichwa cha habari ‘Kulinda rasilimali za nchi ni wajibu wetu kikatiba’, nilisema hivi: Haya tunayafanya ili kutimiza wajibu wetu wa kikatiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatutaka tulinde mali ya umma. Ibara ya 27.-(1) inasema: “Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa Taifa kwa makini kama watu ambao ndiyo waamuzi wa hali ya baadaye ya Taifa lao.”

Ndivyo Katiba ya nchi yetu inavyotutaka. Wanyamapori na misitu ya Loliondo ni mali ya Watanzania kama ilivyo gesi mkoani Mtwara, almasi mkoani Shinyanga; dhahabu ya Tarime, Geita na kwingineko. Utajiri wa nchi sharti unufaishe nchi nzima. Hatuwezi kukaa kimya ilhali Loliondo ikiuawa kwa kigezo cha wanaoiua ndiyo wenye nayo! Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 90 ya mapato katika Wilaya ya Ngorongoro yanatokana na utalii – kwa maana ya wanyamapori na misitu! Asilimia 10 ndiyo iliyo kwenye mifugo na shughuli nyingine. Kwa mapato hayo, ni dhambi kubwa kwa kila mwenye uwezo wa kusema, kushindwa kusema wakati akiona Loliondo au Ngorongoro zikiuawa! Kampuni zilizopo leo zinaweza zisiwepo kesho, lakini Loliondo itabaki kuwa sehemu ya Tanzania. Thamani ya Loliondo inaonekana sasa kwa sababu kuna wanyamapori na misitu. Wanyamapori wakitoweka kwa kasi kama ilivyo sasa, ni wazi kuwa athari zake zitakuwa kubwa zaidi. Nilisema hivyo.

Msimamo wangu haujawahi kubadilika hata kama zitatumika nguvu na hila kujaribu kuchafua watu wanaosimama kwenye kweli.

Sidhani kama yupo Mtanzania mwenye weledi anayeshabikia kuondolewa kwa Wamaasai kule Loliondo au Ngorongoro kwa jumla. Hayupo. Kilichopo ni msuguano wa pande mbili. Mosi, ni ule unaohimiza uendelevu wa rasilimali hii ya wanyamapori na misitu; na upande wa pili ni wale walio tayari kujinufaisha hata kama Loliondo ikibidi kufa, ife.

Waziri Mkuu aliagiza kupatiwa ufumbuzi kwa mgogoro huu kupitia mazungumzo. Huu ni uamuzi mzuri hasa kwa nchi inayozingatia utawala wa sheria.

Lakini naomba iingie kwenye rekodi kuwa mgogoro wa Loliondo hauwezi kumalizwa kwa staili hii. Mgogoro huu hautakoma endapo viongozi wakuu wa Serikali watajazwa hofu yenye kuwafanya wapate kigugumizi.

Nguvu inayotumiwa kuzima mpango wa uhifadhi Loliondo ni kubwa mno. Kubwa sana. Tayari mambo kadhaa yameandaliwa kukwamisha mpango wowote wa kutenga eneo la uhifadhi.

Mosi, hujuma ya kwanza inayotayarishwa na NGOs ni kutumia jamii ya Kimaasai vijijini wajitokeze kwa wingi, waandamane na wapinge kutenga eneo la uhifadhi. Kuna baadhi ya NGOs tayari ziko katika vijiji vya kata saba na kata nyingine za Enguserosambu na Orgosorok kuwahamasisha wananchi wapinge mfumo wowote wasioutaka endapo utawekwa na Serikali.

Pili, NGOs zimejipanga kufungua kesi mahakamani kupinga mpango wowote wa kutenga eneo la uhifadhi, hasa endapo hakutakuwa na Hifadhi ya Jumuiya (WMA).

Tatu, NGOs zimejipanga kufanya maandamano ya uchochezi, upotoshaji na uchonganishi ili ziendelee kupokea fedha kutoka kwa wafadhili wa ndani na nje ya nchi. NGOs zimejipanga kuibua na kutengeneza migogoro mipya ya ardhi.

Kwa bahati mbaya sana, kuna genge la viongozi walioamua kukaa upande wa NGOs, ndiyo maana kila nikitafakari sioni mwanga kwenye utatuzi wa vurugu hizi za Liliondo. 

Hekaya za Loliondo ni jambo linaloelekea kuchusha baadhi ya watu. Nawaomba sana wasomaji wasichoke maana kuyasema haya ni wajibu wa kila Mtanzania mzalendo, hasa anayeguswa na rasilimali wanyamapori na misitu. Kutoyasema haya maana yake ni kukubaliana na dhambi inayoendelea kuukabili uhifadhi.