Na Mwanfishi Wetu. JamhuriMedia, Mwanza
Serikali Kanda ya Ziwa imesema haitawafumbia macho watendaji wa sekta ya afya wanaokwamisha jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika maboresho sekta ya afya.
Akizungumza leo Mei 19, 2023 katika kikao kazi cha watendaji hao wa Kanda ya Ziwa kwa mikoa mitano ya Mwanza, Simiyu, Mara Geita na Shinyanga na Bohari ya Dawa (MSD), Katibu Tawala wa Mara Msalika Makungu, ameema lengo la Rais Dk.Samia kufanya maboresho ya sekta hiyo ni kumpatia huduma bora mwananchi hivyo watendaji watambue wajibu walionao katika kufanya kazi kwa weledi na kumsaidia kufikia lengo la maboresho hayo.
Amesema Kanda hiyo haitawafumbia macho watendaji wanaokwamisha jitihada hizo kwa makusudi.
Amesema, kikao kazi hicho ni muhimu kwa watendaji kuwakumbusha wajibu walio nao katika kufanya kazi kwa weledi na kuwa sehemu ya mabadiliko kwa kutoa huduma nzuri kuanzia katika mapokezi ya wagonjwa, lugha na kuwa na matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.
“ Ni muhimu wataalamu watimize majukumu yao kwa weledi na huduma ziwafikie wananchi kwa kuwa sekta ya afya ni sekta mtambuka yenye tija katika utekelezaji wa malengo ya mpango wa serikali kijamii na kiuchumi,”amesema.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda hiyo wa MSD, Egidius Rwezaura, amesema hivi karibuni wanatarajia kupokea vifaa vya afya zikiwemo dawa na vifaa tiba aina 100 ikiwemo vitanda na mshine za maabara ambavyo vitamaliza changamoto ya mahitaji yaliyopo.
Pia amesema mkakati ni kuwapo vifaa vingine vingi vya akiba katika bohari, kufikia lengo la Rais Dk. Samia katika maboresho ya huduma sekta ya afya nchini.
Naye Mfamasia Mratibu Kiongozi wa Huduma za Bidhaa za Afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mathew Mganga, amesema watendaaji hao watambue kuwa Rais ametoa fedha nyingi za dawa na vifaa ni vyema zitumike katika ununuzi wa bidhaa hizo na sio matumizii mengine.
Amesema lengo la maboresho sekta hiyo, ni kufanikisha huduma bora kwa wananchi ambapo bado fedha zinazomiminika na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Rais Dk.Samia haiendani na huduma bora wanazopatiwa wananchi hivyo ni lazima kuchukua hatua.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk.Zabron Masatu, amesema wamepokea maelekezo hayo wataenda kubanana ndani katika utendaji kuweza kufikia lengo la Rais katika maboresho ya huduma bora za afya kwa wananchi.