Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, ameiagiza Wilaya ya Kilwa kuunda timu itakayofanya uchunguzi ili kubaini watendaji waliosababisha kukwama kwa ujenzi wa zahanati ya Kijiji cha Kisongo, pamoja na ujenzi wa maabara ya Shule ya Sekondari Kata ya Lihimalyao.
Zambi ameyasema hayo baada ya kufanya ziara ya kikazi Januari 7 mwaka huu, katika Kata ya Lihimalyao na kubaini mambo kadhaa ikiwamo uzembe uliofanywa na baadhi ya watendaji na kusababisha vifaa mbalimbali vya ujenzi kuharibika ikiwamo mifuko ya saruji.
Kabla ya ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Gazeti la JAMHURI Toleo Na.275 lilichapisha habari inayohusu ukosefu wa baadhi ya huduma za jamii, huku kukiwa na miradi mbalimbali, ikiwamo zahanati ya Kijiji cha Kisongo iliyoshindwa kumalizika kwa kipindi cha miaka sita, huku kukiwa na mifuko ya saruji zaidi ya 100 iliyotelekezwa katika mradi huo.
Akizungumza na JAMHURI, Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi, amesema kupitia ziara hiyo ameweza kubaini mambo mbalimbali katika kata hiyo, huku akimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, kuunda timu itakayobaini watu waliosababisha uharibifu huo.
“Nimeamua Mkuu wa Wilaya aunde timu ambayo itachunguza wakina nani waliosimamia ujenzi huo ili kujua kila mtu alitimiza uwajibu wake kwa kiasi gani,” amesema Zambi.
Amesema amekuwa akifanya hivyo katika ujenzi wowote wa Serikali ikiwamo zahanati, sekondari, Ofisi za Serikali za Kijiji mkoani hapo, kutokana na kuwapo kwa uzembe unaofanywa na baadhi ya viongozi kwa kushindwa kusimamia.
Zambi anaeleza kuwa kila Kijiji kina Serikali yake, na Halmashauri ya Serikali ya Kijiji ni Serikali yenye mamlaka kamili pamoja na kamati mbalimbali.
“Pale wanapopata msaada au kupewa vifaa vya ujenzi na kushindwa kuvitumia ni uzembe ambao umefanyika,”amesema Zambi.
Mkuu huyo wa Mkoa, amebainisha kuwa katika ziara hiyo, miongoni mwa mambo aliyoyakuta ni pamoja na ujenzi wa maabara katika Shule ya Sekondari ya Kata Lihimalyao, ambapo ujenzi wake umefanywa chini ya kiwango na kusababisha kenchi kuwekwa vibaya na kusababisha mabati zaidi ya 80 kutolewa.
“Nitaendelea kuchukua hatua za kisheria katika maeneo yote ambayo yatabainika, au watumishi wa Serikali wanafanya ujanja,” amesema Zambi.
Hata hivyo, amebainisha kuwa katika kuleta maendeleo katika kata hiyo, Halmashauri ya Kilwa katika bajeti yake mwaka 2017/2018 wanatarajia kujenga mabwawa makubwa ya maji ambayo yatakuwa msaada katika kutatua kero ya maji.
Amesema kuwa mpango mwingine ni kuboresha miundombinu ya barabara kutoka eneo la Hoteli Tatu hadi Kata ya Lihimalyao ambao inatarajia kutekelezwa hivi karibuni na Halmashauri ya Kilwa.
Akizungumzia huduma ya afya, Zambi anasema kuwa zahanati mbili zilizopo Kata ya Lihimalyao zinatarajia kukamilika Juni mwaka huu, na kwamba kati ya vijiji sita vilivyopo katika kata hiyo – viwili ndiyo vinavyoweza kukosa zanahati.
Zambi amesema mpaka sasa Halmashauri zote za Mkoa wa Lindi tayari zimepokea fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa, huku halmashauri nyingine tayari zimeanza kugawa dawa katika vituo mbalimbali vya afya.
Upande wa kilimo, Zambi amesema Lihimalyao ni miongoni mwa kata katika Wilaya ya Kilwa zinazoongoza kwa kilimo cha korosho. Licha ya kufanya vizuri katika zao hilo lakini baadhi ya watu wameonekana kuyatelekeza mashamba ya mikorosho.
“Mimi kinachonisikitika wananchi wa kata hiyo wametelekeza mashamba ya mikorosho, ndiyo maana nimekuwa nikienda kuhamashisha ili watu wapande mikorosho na kuitunza ili wapate fedha na kuboresha maisha yao,” amesema Zambi.
Mkuu wa Mkoa huyo ametoa angalizo kwa watumishi wote wa Halmashauri ya Lindi ambao hawawajibiki, kwani kutowajibika kwao kutasababisha kuchukuliwa hatua za kisheria bila kuoneana aibu.
“Watanzania wanapaswa kutambua kuwa hii ni Serikali ya Awamu ya Tano, na kila mtu anatakiwa kuwajibika ipasavyo ili kuleta maendeleo…kama mtu hawezi kujituma katika Serikali hii hasa katika Mkoa wa Lindi hawezi kuvumiliwa,” amesema Zambi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kisongo, Abedi Selemani, amelishukuru gazeti la JAMHURI kwa kuwasaidia kuifahamisha Serikali matatizo yao, jambo lililomlazimu Mkuu wa Mkoa kufika kijijini kwao kujionea hali halisi.
“Bila ninyi kuibua haya yanayoendelea hapa kwetu tungeishia kusikia maendeleo kwingine, kazi mnayofanya ya kuendelea kuufahamisha umma kile kinachoendelea hapa nchini kwa lengo la kuleta maendeleo kwa Taifa, naomba msiiache,” anasema Selemani.
Selemani amesema kuwa ujio wa Mkuu wa Mkoa katika Kata ya Lihimayalyo ni faraja kwa wanakijiji wa Kisongo na kata kwa ujumla.
Anabainisha kuwa kupitia ziara ya Mkuu wa Mkoa, viongozi wa idara katika Halmashauri ya Kilwa wameweza kueleza mipango ya kimaendeleo ikiwamo kumalizia zahanati ya Kijiji cha Kisongo.
“Nimefurahi kusika ujenzi wa zahanati ya Kisongo inamaliziwa na Halmashauri, kwani wanakijiji tulikuwa hatuna fedha,” amesema Selemani.
Desemba mwaka wa jana, JAMHURI ilitembelea miradi kadhaa iliyoko katika Kijiji cha Kisongo, Kata ya Lihimalyao, na kubaini ukosefu wa huduma ikiwamo maji, afya na huku kukiwa na miradi viporo iliyoshindwa kumalizika kutokana na ukosefu wa fedha.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji uliopo Kijiji cha Kisongo, Kitongoji cha Mangesani, ambapo inadaiwa ujenzi wa mradi huo ulitekelezwa chini ya kiwango na kusababishwa kutofanya kazi.
Mradi mwingine ni ujenzi wa zahanati uliopo Kijiji cha Kisongo, ambao umeshindwa kukamilika kwa zaidi ya miaka sita, huku kukiwa na mifuko ya saruji zaidi ya 100 iliyotelekezwa kwa muda mrefu na kusababisha kuharibika katika mradi huo.