Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Rukwa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Baraka Markusi Nyangala (30), mfanyabiashara na mkazi wa mtaa wa Kasisiwe Manispaa ya Sumbawanga.
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa, ACP, Shadrack Masija amesema kuwa watuhumiwa hao walimuuwa kwa kumpiga na rungu kichwani kisha kuchimba shimo na kumfukia akiwa hai.
ACP Masija amesema kuwa watuhumiwa hao walifanya tukio hilo Septemba 28, mwaka huu, baada ya kumpigia simu marehemu kumjulisha kuwa kuna maharage wanauza.
Amesema kuwa baada ya kukubaliana alikwenda kijiji Cha Katazi, Wilaya ya Kalambo kwa ajili ya kununua maharage wakiwa wote wanne ndipo walipofika porini walitimiza nia yao ya kumpiga Rrngu kichwani.
Amesema kuwa marehemu akiwa na watuhumiwa hao walifanikiwa kumnyang’anya fedha sh 1,840,000 pamoja na pikipiki na baada ya kitendo hicho walichimba shimo na kumfukia akiwa hai.
Ameongeza kuwa taarifa ya kupotea kwa Baraka Nyangala zilifika Polisi na ndipo uchunguzi ulifanyika kwa kuwatumia intelejensia na wataalamu wa Cyber Crime na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa ambao baada ya mahojiano waliongoza mpaka eneo walilomfukia marehemu.
Amesema kuwa lengo la tukio hilo ni unyang’anyi wa mali kutoka kwa marehemu na kutoa wito kwa jamii kuacha tamaa za kupata utajiri au mali za haraka haraka pasipo kufanya kazi halali.
Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Frank Simsokwe (33) , Edfonsi Simsokwe (28) na Niikas Lunguya (38) ambao baada ya kuhojiwa walikiri na kwenda kuonyesha eneo walilomfukia.