Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza Mkutano wa kimataifa wa sekta ya Mifugo na uvuvi (AGRF-2023) September 5-8,2023 Jijini Dar Es Salaam utakaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 3000 wanaojihusisha na mnyororo wa thamani wa Mifugo na chakula.

Kutokana na hatua hiyo,Serikali imewataka wadau wa Mifugo na uvuvi nchini kuwa na utayari wa kushiriki mkutano huo (AGRF)ili kujadili mikakati na hatua madhubuti za kuimarisha usalama wa chakula barani Afrika,ustawi wa uchumi na kuwezesha Afrika kuzalisha chakula na kujilisha yenyewe.

Akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mkutano huo jana Jijini hapa,Waziri wa Mifugo na uvuvi Abdalla Ulega alisema ni wakati sasa Tanzania inapaswa kuelekeza nguvu kwenye mfumo wa chakula na kujadili juu ya usalama na kulisha Dunia chakula kizuri cha daraja la kwanza.

Amesema Tanzania inaenda kuwa mwenyeji wa mkutano huo hivyo Ushiriki wa wadau wa kisekta watanufaika na fursa zitakazopatikana ikiwemo kukutana na wafanyabiasha mashuhuri na wawekezaji kutoka nchi mbalimbali hali inayotazamwa kufungua milango ya uwekezaji na mashirikiano kibiashara.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Abdalla Ulega akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 14,2023 Jijini Dodoma kuhusu mkutano wa kimataifa wa wadau wa Mifugo wa AGRF 2023 unaotarajiwa kufanyika Septemba 5 hadi 8 mwaka huu jijini Dar Es Salaam.

“Lengo ni kuwezesha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu kuingia kwenye ufugaji na uvuvi na kuwa na uwezo wa kusafirisha Mifugo hai nje ya nchi na kuitangaza nchi,ili kurahisisha hayo Serikali inaendelea kuboresha utaratibu wa upatikanaji wa vibali vya kusafirisha Mifugo na mazao yake nje ili kuleta unafuu kwa wafugaji,”amesisitiza

Pamoja na hayo Waziri Ulega amesema mkutano huo utatoa fursa ya kuongeza uzalilishaji na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kuuza ziada ya mazao na kufafanua kuwa kwa sasa biashara ya nyama imeshamiri na kuuza tani 12,000 kwa mwaka sawa na Dola za marekani milioni 51 ambapo kabla ya hapo Tanzania iliuza tani 1600 pekee .

“Lazima tufuge Kwa malengo,wafugaji wanapaswa kuelewa kuna kuishi na kuku na kufanya biashara ya kuku, tuingie kwenye kufuga mifugo biashara na sio kuiishi na Mifugo kama wengi wanavyofanya huko vijijini,”amesema na kuongeza;

“Sisi kama Serikali tulianzisha mkakati wa mashamba darasa Kwa halmashauri 44 zenye Mifugo Kwa kuanzisha mashamba zaidi ya 100 Ili kuwaonesha wafugaji kuwa inawezekana kulima,kuvuna na kuhifadhi Kwa faida zaidi,hii itaenda sambamba na urasilimishaji wa Kilimo cha majani na uhifadhi wa ardhi,pomoja na kuwa na Ranchi za asili,”amesisitiza

Waziri huyo pia ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha wadau kuandaa taarifa za Kampuni zao kwa ufasaha ili iwe rahisi kujitangaza na kuvutia wawekezaji,wafadhili na kuongeza wigo wa biashara zao.