Wadau mbalimbali nchini wametoa maoni yao mara baada ya wiki iliyopita Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kumtangaza Ettiene Ndayiragije kuwa kocha mkuu wa muda wa timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars.
Kocha huyo anachukua mikoba iliyoachwa na raia wa Nigeria, Emmanuel Amunike, ambaye mkataba wake wa kuifundisha timu hiyo ulisitishwa baada ya Stars kutofanya vizuri katika mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika nchini Misri.
Ndayiragije amepewa kandarasi hiyo ikiwa ni siku kadhaa tangu apewe mkataba wa kuifundisha timu ya soka ya Azam nchini. Kabla ya hapo alikuwa akiinoa timu ya KMC aliyoiwezesha kushika nafasi ya nne katika msimu uliopita wa ligi kuu.
Ndayiragije anatarajiwa kuanza kuiongoza Stars kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kufuzu michuano ya wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN), Julai 28, mwaka huu katika dimba la Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ndayiragije anakaimu nafasi hiyo huku akisaidiana na Suleimani Matola, Juma Mgunda na beki na nahodha wa zamani wa timu ya Yanga, Nadir Haroub ‘Canavaro’.
Kutokana na uteuzi wa Kocha Ndayiragije, wadau mbalimbali wa soka wamezungumza na gazeti hili na miongoni mwao ni Mwalimu Alex Kashasha, ambaye amesema kujenga timu kunahitaji muda wa kutosha.
“Sisi hatujapiga hatua kama wenzetu katika maendeleo ya soka. Wenzetu Misri ambao baada ya kufanya vibaya katika michuano ya AFCON wakamtimua Kocha wao, Javier Aguirre,” amesema.
Vilevile Kashasha ameongeza kuwa: “Tatizo tumekuwa na kasumba ya kutowaamini walimu wazawa. Bado makocha wa ndani wameonekana hawana thamani wakati timu ya Mtibwa Sugar imetumia walimu wa ndani na kwa miaka kadhaa wamecheza soka la ushindani wa hali juu pamoja na kuzisumbua klabu kubwa.
“Watanzania tuna papara za kuhitaji matokeo papo hapo tunapocheza, nina tamani tushinde kutokana na misingi inayowezesha kushinda, misingi ambayo ni pamoja na kuwekeza kwenye soka, sambamba na maandalizi ya kutosha,” amesema.
Kashasha anaamini kuwa Kocha Ndayiragije ana uwezo wa kuisuka Taifa Stars na kuibwaga Kenya katika mchezo wao ujao.
“Anaweza kuangalia mechi ambayo mtangulizi wake alifungwa na Kenya kule Misri, akabaini kwa nini alifungwa halafu akaja na falsafa mpya inayoweza kuleta matokeo chanya kwa Stars,” amesema.
Kwa upande wake mchambuzi wa soka anayechipukia, Ally Kamwe, naye anasema: “Kama wachezaji wadogo wa timu ya KMC walimuelewa kwa haraka Kocha Ndayiragije, kwa nini wachezaji wenye kaliba ya kina Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude na Paul Godfrey wasimuelewe Ndayiragije?” Lakini kama tumemchagua Ndayiragije kukaimu nafasi ya kuwa kocha wa Stars, michuano ya fainali za CHAN kisiwe kipimo cha kumuamini moja kwa moja.