Na Lookman Miraji, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Tuzo za Kimataifa za Heshima ambazo hutolewa kwa watu maalum kwa kutambua mchango ambao hutolewa na watu hao katika jamii husika zimefanyika nchini kwa mara kwanza mwaka huu.
Tuzo hizo maarufu kama (I-CHANGE INTERNATIONAL AWARDS) Kihistoria ziliasisiwa nchini Marekani mnamo mwaka 2011 zikiwa na lengo la kuthamini watu wanaofanya mambo mazuri katika jamii zao.
Tuzo hizo ambazo hutolewa kila mwaka zimekuwa zikihusisha watu kutoka mataifa 150 Duniani kote.
Kwa mwaka huu 2024 tuzo hizo zimeendeshwa kwa mara ya kwanza hapa nchini na kutolewa kwa baadhi ya Watanzania ambao imethibitika kuwa wamekuwa na mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali katika jamii ya kitanzania.
Hafla ya tuzo hizo zilifanyika hapa nchini mwishoni mwa juma lililopita katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere(JNICC) Dsm.
Tuzo hizo pia zilipata kuhudhuriwa na watu kutoka katika nyanja mbalimbali wakijumuishwa viongozi wa kiserikali, wasanii, wajasiriamali pamoja na watu maarufu kutoka tasnia mbalimbali.
Katika tuzo hizo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri mstaafu Prof;Anna Tibaijuka ambaye aliongoza waandaji wengine kuzikabidhi tuzo hizo kwa washindi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo Waziri Mstaafu Pro.; Anna Tibaijuka amesema ya kuwa tuzo hizo ni muhimu kwakuwa zimetambua watu mbalimbali hivyo ziende kuongeza thamani ya kuwa motisha kwa walioshinda tuzo hizo kuendelea kufanya mambo ya msingi katika jamii husika.
”Leo tumeona tuzo hizi zimetambua watu wanaofanya jamii yetu kuwa mahala salama zaidi kutoka katika fani mbalimbali. Tumeona hapa wasanii wametambuliwa hapa ,waandishi wa habari pamoja viongozi vijana pia wametambuliwa hapa na wengine pia kutoka katika nyanja mbalimbali.
Muhimu zaidi kwa walioshinda sio kwamba wafurahie kwamba wamepata tuzo ila maana kubwa ni wao kutambua ni namna gani wanazidisha mchango wao katika jamii na isiwe sehemu ya wao kujivunia na kujikweza” alisema Mstaafu Tibaijuka.
Akizungumza pia kwa niaba ya waandaji wa tuzo hizo, Mkurugenzi wa kampuni ya uandaaji matukio ijulikanayo kama ”Thevvents” Venitta Mwita amesema kwao ni furaha kubwa kuwa sehemu ya walioandaa tuzo hizo kubwa duniani hasa ikiwa ni kwa mara ya kwanza zinafanyika hapa nchini.
”Imekuwa ni furaha kwangu kama kiongozi kuongoza wengine kuandaa tukio hili kubwa na hii ni kiashiria mojawapo cha ukuwaji wetu kwa maana kuandaa tukio hili kwa mara kwanza maana yake nimeaminiwa na watu wa Marekani na nimeaminiwa hata na Watanzania wenzangu hivyo si kitu kidogo na ni jambo la kushukuru kwetu kama taasisi kupewa dhamana ya kuandaa tukio hili.” ameyasema hayo Mwita.
Tukio la tuzo hizo pia lilienda sambamba na ugawaji wa tuzo mbili za heshima ambayo ya kwanza ilikuwa ni tuzo ya udaktari wa heshima ambayo ilienda kwake Prof.Anna Tibaijuka kwa kuthamini pia mchango wake kwa wakati wote ndani ya jamii.
Na tuzo ya pili ilikuwa ni tuzo ya Ubalozi wa heshima (Humanitarian Ambassador) iliyokwenda kwake Ndg; Venitta Mwita kwa kutambua yale yote aliyoyafanya katika kufanikisha shughuli hizo.
Wafutao ni miongoni mwa baadhi ya Watanzania ambao walikabidhiwa tuzo kutoka katika nyanja mbalimbali.
Seleman Msindi maarufu kwa jina la Afande Sele ambaye ni msanii wa muziki kutoka hapa nchini ameshinda tuzo ya Uhamasishaji wa kutunza mazingira. Tuzo hiyo amekabidhiwa kutokana na jitihada zake anazozifanya katika jamii juu ya namna gani inaweza kushirikiana katika kulinda na kuyatunza mazingira. Tuzo hiyo ilitolewa mnamo tarehe 1 Julai 2024 huko nchini Marekani na kukabidhiwa kwake Julai 27 mwaka huu mbele ya Dkt; Ruben West kutoka nchini Marekani, Balozi Dominic Obadiah kutoka Kenya na Mstaafu Prof; Anna Tibaijuka.
Jokate Urban Mwegelo ambaye ni katibu Mkuu wa umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) amefanikiwa kushinda tuzo uongozi bora kwa upande wa jinsia ya kike. Tuzo hiyo ilitolewa mnamo tarehe 1 Julai Mosi mwaka huu huko nchini Marekani na kukabidhiwa kwake Julai 27 mwaka huu katika ukumbi wa kimataifa JNICC mbele ya Dkt; Ruben West kutoka nchini Marekani, Balozi Dominic Obadiah kutoka Kenya na Mstaafu Prof;Anna Tibaijuka.
Mariam Mbano ambaye ni mwandishi wa vitabu pamoja na riwaya ni miongoni mwa watanzania walikabidhiwa tuzo hizo kwa kutambulika kama mfano wa kuigwa kwa wanawake na wasichana kutokana na kazi anayoifanya inawezesha watu kufahamiana na kutengeneza fursa miongoni mwao na kumuongoza kila mmoja kujitambua na bora zaidi ya alivyokuwa awali na kuweza kujielezea vizuri.
Tuzo hiyo ilitolewa mnamo tarehe 1 Julai mwaka huu na kukabidhiwa kwake Julai 27 mwaka huu katika ukumbi wa kimataifa wa JNICC mbele ya Dkt; Ruben West kutoka nchini Marekani, Balozi Dominic Obadiah kutoka Kenya na Mstaafu Prof; Anna Tibaijuka.
Watanzania wengine waliotunikiwa tuzo hizo ni Millard Ayo (Mtangazaji), Eliud Samwel (Mchekeshaji),Tuma Provion( Mwanahabari), Joel Nanauka, Sophia Mbeyela, Laura Petie, Anna Mbisse ,Junior Abel, Hilda Kabe.