“Ukweli una tabia moja nzuri sana, haujali mkubwa wala mdogo; haujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza kisasi; kama ukipuuza.
Ukiniona nataka kulipiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nikalipiga teke, basi litanivunja dole japo ningekuwa nani. Ukweli haupendi kupuuzwa-puuzwa.”
Maneno hayo ni ya Mwalimu Julius Nyerere aliyoandika katika kijitabu chake ‘TUJISAHIHISHE’ mnamo mwaka 1962. Nimenukuu maneno hayo ili yanipe vigingi na mserereko mzuri katika makala ya leo kuhusu ulinzi na usalama wetu Watanzania.
Falsafa au mafunzo yaliyomo katika nukuu hiyo ni tabia ya ukweli ambayo haijali haiba ya mtu, madhara ya kupuuza ukweli ambao daima huwa maumivu. Ukweli humsaidia adui kutambua jema na rafiki pia kutambua baya. Adui au rafiki hutenda lililo sahihi.
Ni mwezi sasa, vyombo vyetu vya habari kupitia taarifa za habari, matukio, makala na tahariri zake zimezungumzia na zimehadharisha kauli au vitendo vya baadhi ya watu – iwe ndani au nje ya nchi – vinavyojaribu kuchezea ulinzi na usalama wetu.
Vyombo vya ulinzi na usalama kwa kiasi chao vimepokea taarifa hizo na kupambana na kauli na vitendo viovu kwa mujibu na taratibu za kazi zao. Pamoja na vyombo hivyo kutimiza wajiu wao, bado usalama wetu umechezewa na maadui wetu na kutufanya wananchi tutaharuki.
Watu wanauawa kwa kuchinjwa kama wanyama. Tumesikia na wengine kushuhudia yaliyotokea katika sehemu mbalimbali nchini ikiwamo mikoa ya Geita, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam. Juzi tumepoteza ndugu zetu wanane waliochinjwa na kuuawa katika eneo la Amboni, Kitongoji cha Kibatini, Mtaa wa Mleni, Kata ya Mzizima, Jijini Tanga.
Matendo ya kuua yanaonekana kana kwamba yanapewa nafasi ili yawe ni sehemu ya tamaduni zetu, jambo ambalo si la kweli wala si sahihi. Wanaofanya hivyo ukweli wanajidanganya. Watanzania hatupendi wala hatuna desturi ya kuuanauana kama wanyama porini.
Ni kweli na sahihi tuna chombo cha ulinzi – Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na tuna chombo cha usalama wa raia – Polisi, na tuna chombo cha usalama wa Taifa. Vyombo hivyo vina askari shupavu, makini na weledi katika kufanya kazi zao. Binafsi navipongeza na kuvipa heko na kongole nyingi kwa sababu nchi haiko matatani. Ya Rabii tuepushe na majanga hayo ya kuuana. Amin.
Vyombo hivyo havina idadi kubwa sana ya walinzi kupita idadi ya Watanzania wote lau kama wanafanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa mno. Kwa kutambua hilo na kuona ipo haja ya kuwa na ulinzi na usalama timilifu, viongozi wazalendo wa nchi hii kwa ridhaa waliyopewa na wananchi, waliandaa Mwongozo kuhusu Ulinzi na Usalama ambao ndiyo kinga na jawabu la usalama wetu.
Mwongozo huo unasema, “Msingi wa maendeleo yote ya Watanzania ni Watanzania wenyewe. Kila Mtanzania; na hasa kila mzalendo na kila mjamaa. Msingi wa maendeleo ya ulinzi na usalama wa Watanzania ni Watanzania wenyewe. Kila Mtanzania; na hasa kila mzalendo na kila mjamaa. (Ibara 21, Mwongozo wa TANU, 1971).
Hata kama Ujamaa wenyewe tumeutupilia mbali Watanzania, mantiki ya ulinzi na usalama ipo pale pale. Mwongozo huo unaendelea kusema katika ibara ya 25 kuwa, “Kutokana na mwamko wa siasa, wananchi wafahamishwe maadui wa Taifa letu, na hila wanazotumia katika kupiga vita siasa yetu, uhuru wetu, uchumi wetu na utamaduni wetu. Papo hapo, ili wananchi waweze kumkabili adui huyo, lazima wafahamishwe nguvu za adui huyo katika fani zote, kama vile majeshi yao, biashara zao, maisha yao na tabia zao na jinsi zinavyogongana na hali yetu.
Si hivyo tu, ibara ya 26 baadhi ya maneno inasema, “Kwa hiyo, ni lazima kuanzisha mafunzo ya malisha (mgambo) kwa nchi nzima. Hawa malisha, kwa sababu wataenea nchi nzima, ndiyo watakaokuwa na wajibu wa kulinda mipaka ya nchi kavu na pwani, hali kadhalika anga, na kuwafichua majasusi na maadui kwa kushirikiana na majeshi yetu ya kawaida.”
Hakika Mwongozo huo uliimarisha ulinzi na usalama katika vijiji, mitaa, miji na sehemu za ofisini na viwandani na mashambani. Wajumbe wa nyumba 10, mafunzo ya mgambo na wanamgambo, mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), mafunzo ya Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Zanzibar na polisi viwandani na ulinzi wa sungusungu. Hali ilikuwa shwari nchini hadi kwenye milango ya mwaka 1995. Baada ya mwaka huo hadi leo hali si shwari huko mitaani na dalili za usalama kutoweka inaonekana kutokana na kupuuza usalama wetu wenyewe.
Nasikitika kutamka ujio wa mfumo wa vyama vingi vya siasa na haki za binadamu kueleweka visivyo kwa baadhi ya viongozi, kuwashawishi wananchi eti ulinzi si kazi zao ni kazi za askari pekee, hapo ndiyo kasoro. Tukapuuza ukweli na malipo ndiyo haya!
Ni vyema tukarudi katika busara zetu wananchi tushiriki kikamifu katika ulinzi wa mitaani. Namalizia kwa kunukuu yafuatayo, “Katika upande wa ulinzi wa Taifa, wananchi wawe macho na vibaraka waliomo nchini ambao wanaweza kutumiwa na maadui wa nje wenye nia mbaya ya kuliangamiza Taifa hili na wawe tayari kulinda Taifa inapolazimika kufanya hivyo” mwisho wa kunukuu. (Azimio la Arusha).