Miaka 14 imepita tangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere afariki dunia. Ameiacha dunia ikiwa katika mapambano, misuguano na vita kali ya maneno na silaha kati ya wanyonge na wenye nguvu kuhusu uonevu, dhuluma, haki na ukweli.

Mwalimu Nyerere alipokuja duniani, Aprili 13, 1922 na kupewa jina la Kambarage, alikuta dunia imo katika misukosuko ya ukoloni, uchumi wa kinyonyaji na utawala wa mabavu kati ya mataifa ya Yuropa dhidi ya mataifa ya Afrika, Asia na mengineyo. Ni miaka minne tu tangu Vita ya Kwanza ya Dunia kumalizika (1914-1918).

 

Kambarage alipofikisha umri wa miaka 17 akiwa barobaro wa Kizanaki aliendelea kutafuta elimu ya mazingira katika Shule ya Mtakatifu Maria (St Mary’s), Tabora kuanzia mwaka 1937 hadi 1942 huku akishuhudia Vita ya Pili ya Dunia (1939-1945). Vita hii ilienea katika sehemu nyingi za dunia; Yuropa, Afrika, Asia na ilikuwa vita ya mabeberu waliokuwa wakigombea maslahi.

 

Mabeberu wa Yuropa wasio na makoloni — Wajerumani, Wataliano na Wajapani – waliungana kupigana na mabeberu wenye makoloni —  Waingereza, Wafaransa, Wareno, Wabelgiji na wengine. Marekani ilijiunga na kundi hilo kwa sababu za kiuchumi, kwani iliruhusiwa kuingiza vitegauchumi vyake katika makoloni ya mataifa hayo.

 

Asili ya utu wake, Uzanaki, utamaduni, na Utanganyika wake, havikumzubaisha kufikiri dunia ni kitu gani mbele ya mwanadamu. Ubongo wake ulimfanya afikiri, atenganishe na atende mambo mema na akwepe mabaya ya dunia. Akili zake pevu zilimwongoza vema, enzi za ujana wake katika mazungumzo, majadiliano na matendo.

 

Kambarage alishtua mbongo na fikra za wazazi, ndugu, marafiki na jamii ya kabila la Wazanaki hata kumtabiria angekuwa mtu wa heshima, busara na kiongozi mzuri ukubwani. Ni kweli ujana wake aliutumia vema shuleni hadi vyuoni kwa kuwaunganisha wasomi wenzake katika umoja wa mapambano dhidi ya ukoloni, uonevu na dhuluma. Nje ya masomo ya elimu, alitumia vipaji vyake kuwaunganisha wananchi katika harakati za ukombozi barani Afrika.

 

Uchungaji mbuzi haukuwa upeo wa elimu yake wala ndoa haikuwa kimbilio lake kama walivyokuwa vijana wenzake wa Kizanaki. Uchezaji ngoma kama zile za mbegete, kirere, etono, nyerukerege na unywaji wa pombe ya amachicha na oburundi havikumshughulisha sana. Kilimo cha mtama, uwele na mboga mboga kilishtua misuli yake mwilini na michezo ya utotoni na ujanani ulichangamsha akili zake na kuzifanya kuwa tambuzi juu ya mambo mbalimbali duniani.

 

Chifu Nyerere Burito na Christina Mugaya wa Nyong’ombe walijaaliwa na Mwenyezi Mungu kuzaa mtoto huyu wa kiume,  Kambarage. Kuja kwake duniani kumesaidia mambo mengi yakiwamo mirindimo ya siasa, haki na ukombozi. Leo tunapomkumbuka Tanzania inalia, Afrika inasikitika na dunia inatafakari.

 

Makuzi na elimu hayakuwa ya tabu wala shida. Alianza Shule ya Mwisenge, Musoma akiwa na umri wa miaka 12. Baada ya miaka minne alijiunga na Shule ya Mtakatifu Maria (St. Mary’s) Tabora, 1937. Januari 1943, alijiunga na Chuo cha Makerere, Uganda na alipata Diploma ya Ualimu mwaka 1945.

 

Mnamo Oktoba 1949 hadi Julai 1952 alisoma katika Chuo Kikuu cha Edinburgh, Scotland ambako alipata Shahada ya Uzamili (M.A). Alipomaliza masomo yake, alirudi nchini na kuanza kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Francis (St. Francis) Pugu, Februari 1953.

 

Katika harakati zote alizopata kuzifanya ujanani, mwishoni alitambua bado hajatimiza mambo muhimu mawili. Dini na ndoa. Alijiona mpungufu na mchache wa shukrani kama asingetimiza mambo hayo mbele ya Muumba wake. Desemba 1943 alibatizwa na Father Mathias Koenen kwa utaratibu wa Kanisa Katoliki. Januari 21, 1953 alifunga ndoa na Mwalimu mwenzake Maria Gabrieli, huko Musoma mkoani Mara.

 

Kauli na matendo yake Kambarage Nyerere yalijidhihirisha alipokuwa shuleni hadi chuoni. Vitabu vilikuwa mito yake ya kulalia. Maandishi vitabuni yalikuwa mate yake ya kulainisha ulimi kudanda chini na juu kinywani mwake. Macho yaliona maandishi, masikio yalipokea maelezo, na kichwa kilitunza yaliyosemwa. Kifua kilihifadhi mema na mabaya kuficha siri ya utu na ubinadamu wake.

 

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anaweza kusimuliwa katika fasili mbalimbali kulingana na mtoa fasihi anavyomuona, anavyomtambua na anavyomkubali. Mtawala, mwanasiasa, mwanamichezo, mwana-lugha, mwana-dini, rafiki, adui na kadhalika almradi kila mtu analo la kusema kuhusu yeye. Lakini wote hao na wengineo katika mapambo yao yote watatoa mambo makuu mawili — mema na mabaya.

 

Marehemu au hayati yeyote hukumbukwa kwa mambo yake aliyotenda enzi za uhai wake duniani, na huko ahera atahukumiwa kwa amali yake aliyochuma alipokuwa duniani. Si mimi wala si wewe, hatuna haki ya kuhukumu mambo au matendo ya mtu yeyote aliyefariki dunia, zaidi ya kumwombea kwa Muumba wake amweke Mahali Pema Peponi au Mbinguni.

 

Mwalimu Julius K. Nyerere anakumbukwa kwa mambo mengi aliyofanya kwa Watanzania, Waafrika na hata watu wa mataifa mengine duniani. Kati ya mambo hayo ni Uhuru wa Tanganyika, ukombozi wa nchi za Afrika, upiganiaji haki na utetezi kwa wanyonge, kupinga ubaguzi wa aina yoyote na uongozi wake uliojaa hekima na busara. Ameijenga na kuitangaza Tanzania duniani. Leo tunamkumbuka.

 

Wakati tunamkumbuka Mwalimu Nyerere, nimeona tuangalie kauli zake mbili zinatukumbusha nini na je, tunazienzi? Machi 7, 1955 Mwalimu Nyerere kwa mara ya kwanza alihutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa nchini Marekani alipotumwa na chama cha siasa cha TANU. Katika hotuba yake jambo mojawapo alilosema ni kuhusu wageni na ardhi.

 

“…. Katika mambo yaletayo wasiwasi kati ya mataifa yaliyomo Tanganyika ni habari ya wageni kuhamia katika nchi na kupewa ardhi. Lazima nirudie kutia mkazo tena kwamba Wazungu na Wahindi waliomo Tanganyika ni Watanganyika wenzetu. Hatupendi wafukuzwe au wafanyiwe ubaguzi wa namna yoyote. Lakini Wahindi na Wazungu tuliowakubali ni wale ambao wameisha kukubali kukaa Tanganyika daima. Mhindi ambaye bado yuko India au Pakistan si Mtanganyika.

 

“Kadhalika Mzungu aliye Uingereza au Ugiriki si Mtanganyika. Hao hatuwataki. Hatutaki nchi yetu iwe mahali pa kupunguzia Wahindi, Wazungu au Waamerika waliozidi katika nchi zao. Kwa hiyo tumesema wazi wazi kwamba tutapinga uhamiaji wa wageni katika Tanganyika.

 

“Lakini sina budi nisema wazi kwamba hatutapinga wageni wa aina yoyote kuingia Tanganyika. Tutawakaribisha walimu wa dini na watumishi wa Serikali ambao tunawahitaji kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakaribisha wageni wanaokuja kufanya biashara nasi na kuanzisha viwanda maalum ambavyo ni vya faida kwa nchi nzima. Watu wa aina hizi kwa kweli si wahamiaji wa Tanganyika. Kusudi lao si kukaa Tanganyika bali kufanya biashara.

 

“Sehemu kubwa sana za nchi yetu zimekwisha kuchukuliwa na wageni, hatujapata kudai kwamba wanyang’anywe ardhi hiyo. Lakini tumedai kwamba muda wa miaka 99  ni muda mrefu mno wa kukodisha ardhi kwa wageni. Katika miaka hiyo 99 Tanganyika itaweza kuwa na watu zaidi ya mara tatu ya wale waliomo sasa.

 

“Kwa hiyo tumesema kwamba tangu mwanzo ilibidi ardhi ikodishwe kwa muda mfupi wa miaka 33. Tumedai pia muda huu unapoisha Serikali haina budi ikisie mahitaji ya wenyeji kabla ya kukubali tena ardhi hiyo kwa mgeni. Hayo tumesema kwa ajili ya ardhi ambayo imekwisha kukodishwa kwa wageni. Lakini hatutaki ardhi yoyote ambayo haijakodishwa kwa wageni ikodishwe tena.’’

 

Hotuba nyingine tuiangalie ni ile aliyoitoa Machi 5, 1999 wakati wa kupokea digrii ya heshima ya udaktari (Doctor of Letters) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Katika hotuba hiyo alizungumzia suala la elimu. Alisema:

 

Kwanza, elimu yetu iwe ni kwa wote. Kama elimu yetu ya msingi haitakuwa kwa wote, basi watakaoikosa zaidi watakuwa wasichana. Kila mtoto katika nchi hii awe wa kiume au wa kike lazima apate kiwango cha chini cha elimu kama haki yake.  Mfumo wa sasa wa miaka miwili (2) ya elimu ya awali na miaka saba (7) ya elimu ya msingi kwa maoni yangu una mantiki na unawezekana. Tutaongeza kiwango kadri uwezo wetu utakavyokuwa unaongezeka.

 

Pili, elimu yetu haina budi kuwa bora. Hasa elimu ya msingi lazima iwe ni nzuri sana; kwa sababu hii ndiyo elimu rasmi pekee ambayo Watanzania wengi wanaweza kuipata. Hivi sasa ubora wa elimu yetu ya msingi unatisha kabisa. Hatuna budi kuchukua hatua kama jambo lenye umuhimu wa  pekee kitaifa. Mbali na ukweli kwamba ni elimu inayotolewa kwa idadi kubwa ya raia wa Tanzania, bali ni msingi wa mfumo mzima wa elimu yetu. Ndiyo elimu ya MSINGI. Kama elimu hii ni dhaifu basi mfumo mzima wa elimu utaharibika.

 

Tatu, elimu yetu haina budi kuwa yenye manufaa. Katika kiwango cha elimu ya chuo kikuu wanafunzi na walimu waliamini kwamba tulichokuwa tunatangaza ilikuwa aina fulani ya elimu duni. Walitukumbusha kuwa, elimu ya chuo kikuu ilikuwa ni kwa wote, halali ulimwenguni pote. Ni kwa jinsi gani inaweza kurekebishwa ili kwenda sambamba na mahitaji ya Watanzania bila kuifanya duni ikilinganishwa na elimu ya chuo kikuu inayotolewa sehemu nyingine ulimwenguni?

 

Ilikuwa wakati huo tulipojaribu kusisitiza umuhimu wa elimu ya ufundi katika kiwango cha elimu ya sekondari. Hiyo ingekuwa ni hatua ya kuondokana na wazo la shule za sarufi za mfumo wa elimu wa Kiingereza.

 

“Hali kadhalika tulipotangaza elimu ya kujitegemea hasa katika kiwango cha chini, tulionekana kama watu fulani, wajinga wa itikadi ambao hawajui lolote kuhusu elimu ya kweli.

 

“Uwezekano wa msomi wa chuo kikuu kukosa kazi haukuwapo, bila kujali sifa za elimu yake. Lakini hivi sasa hali imebadilika; katika kundi la watu wasio na kazi wamo wahitimu wa chuo kikuu pia. Huu si upuuzi tu kwa nchi maskini kama Tanzania, bali ni maafa.

 

“Mwisho, elimu yetu hasa Elimu ya Juu lazima iwajibike. Elimu ya kujitegemea siyo elimu ya uchoyo. Hiyo ni kwa ajili ya mtu kujitegemea, lakini pia ni kwa ajili ya nchi yetu kujitegemea. Ninaamini kwamba jamii ina wajibu wa kuwaelimisha watu wake. Umuhimu wa watu katika kuchangia moja kwa moja katika elimu ya watoto wao hauwezi kuwa sababu ya kufanya jumuia yote, inayowakilishwa na Serikali za Mitaa na Serikali Kuu kuepuka jukumu lake la kumsaidia kila Mtanzania kupata elimu nzuri.

 

“Lakini kwa nchi maskini kama Tanzania, haiwezi kumudu kuwaelimisha wachoyo. Inawekeza katika elimu ikiamini kwamba, kitegauchumi cha aina hiyo ni kizuri kwa wote wanaohusika na kwa jamii yote kwa ujumla. Kwa lugha au msemo wa jana: Elimu ya Kujitegemea hasa katika kiwango hiki cha elimu ya juu lazima pia iwe ni Elimu kwa ajili ya Huduma.’’

 

Je, katika kauli hizo, Watanzania tunazienzi? Tujadili.