Tanzania Bara ina eneo la hekta zaidi ya milioni 94.7. Wakati tunapata Uhuru Desemba 9, 1961 sehemu kubwa ya ardhi ilikuwa imefunikwa na misitu na mapori. Waingereza walioitawala Tanganyika baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyoanza mwaka 1914 hadi 1918, waliweka Sera ya Misitu mwaka 1953.
Sera hii iliweza kutekelezwa kwa kutumia Sheria ya Misitu (Forest Ordinance) ya mwaka 1957. Wakati huo hapakuwapo takwimu sahihi zilizoonesha Tanganyika ilikuwa na eneo kiasi gani lenye misitu ya asili na mapori. Hii ni kwa sababu wakoloni hawakuona umuhimu wa kupima kutokana na gharama za upimaji misitu (forest inventory) kuwa kubwa sana.
Hata hivyo, wakoloni waliweza kupima maeneo machache waliyoyaona kuwa ya muhimu sana katika kuhifadhi mazingira, hasa misitu yenye vyanzo vingi vya maji na baioanuai nyingi na hivyo kuyaweka maeneo kama hayo chini ya usimamizi wa kisheria.
Wakati tulipopata Uhuru, misitu zaidi ya 212 yenye jumla ya hekta takriban milioni 11.7 ilikuwa imetangazwa kuwa misitu iliyohifadhiwa kisheria (Forest Reserves). Wakoloni hawakuona haja ya kuipima misitu yote kwa sababu misitu ilionekana ipo kwa wingi na watu (wakazi wa Tanganyika kwa wakati huo) walikuwa wachache (takribani watu milioni tisa) ikilinganishwa na idadi ya sasa ya watu zaidi ya milioni 44.
Wakoloni wote (Wajerumani na Waingereza) waliweka nguvu zao katika kukusanya fedha (ushuru na mrabaha) kutokana na mazao ya misitu waliyokuwa wanavunwa. Kufika miaka ya 1970 na 1980 kulikuwapo angezeko kubwa kwa kilimo cha kuhamahama (shifting cultivation) katika sehemu mbalimbali nchini.
Vilevile, uchomaji moto misitu na mapori wakati wa kiangazi ulishamiri kiasi cha kuhatarisha mazingira. Pamoja na hayo, mifugo (ng’ombe, kondoo na mbuzi) katika baadhi ya maeneo iliongezeka na kuzidi uwezo wa maeneo ya malisho. Kutokana na mifugo kuzidi uwezo wa malisho, hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, wafugaji walianza kuhamia mikoa mingine baada ya kuona kuwa sehemu zao zimeharibiwa sana.
Haya yote yalisababisha misitu kuanza kutoweka kwa kasi kubwa na hali ya mazingira kuwa mbaya. Kwa mfano, katika maeneo ya Kondoa mkoani Dodoma na sehemu za Mkoa wa Shinyanga. Kasi ya mmomonyoko wa udongo ilikuwa kubwa kiasi cha kusababisha baadhi ya maeneo kuwa na makorongo makubwa na kutishia hali ya maisha kwa wakazi wa maeneo husika.
Hivyo, kutokana na hali hiyo Serikali ililazimika kuchukua hatua za haraka kupunguza kasi ya mmomonyoko wa udongo nchini. Moja ya hatua zilizochukuliwa ilikuwa kuanzisha miradi ya kurekebisha sehemu zilizokuwa zimeharibika mno hasa kwa kutengeneza makingamaji na kuyaimarisha kwa kuotesha nyasi na miti, hasa minyaa (Euphobia tirucalii) katika Mkoa wa Shinyanga. Pia kuongeza kasi ya kuhamasisha wananchi ili wapande miti sehemu mbalimbali nchini.
Miradi iliyoanzishwa ni pamoja na mradi wa Hifadhi Ardhi Dodoma (HADO) na Hifadhi Ardhi Shinyanga (HASHI) iliyotekelezwa Dodoma na Shinyanga kuanzia katikati ya miaka ya 1970 na 1980.
Pamoja na Serikali kuchukua hatua hiyo, ilianzisha kitengo cha kuelimisha wananchi na kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kutunza mazingira na kupanda miti vijijini. Kwa kuwa Serikali ilikuwa imeishaanzisha Sera na Programu ya Vijiji vya Ujamaa, Wizara ya Maliasili na Utalii iliona ni vyema kwenda sambamba na programu hiyo.
Kupitia misaada ya fedha kutoka Serikali ya Sweden, kitengo cha kuelimisha na kuhamasisha wananchi vijijini juu ya umuhimu wa kutunza na kutumia vizuri rasilimali ardhi, misitu na wanyamapori katika wizara hiyo, kiliimarishwa kwa kupatiwa vitendea kazi.
Vifaa kama magari ya kuoneshea sinema, tepurikoda za kurekodi vipindi vya redio na kamera viliwezesha Idara ya Misitu na Nyuki, kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kutunza Mazingira.
Kazi hii muhimu ya kuhamasisha na kuelimisha umma umuhimu wa misitu katika maisha yetu ya kila siku inaendelea hadi sasa. Makala haya ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi hizo za Serikali ili mazingira yanayotuzunguka yaendelee kutunzwa vizuri na yawe endelevu.
Idadi ya Watanzania imeongezeka, kama ilivyo kwa mifugo pia. Hali hii inatishia uhai na ustawi wa mazingira. Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 zinaonesha kuwa Tanzania Bara ina watu zaidi ya milioni 44; na mifugo isiyopungua milioni 42 (ng’ombe milioni 21.3; mbuzi milioni 15.2 na kondoo milioni 6.4).
Kutokana na ongezeko kubwa la wanadamu na mifugo, matumizi ya rasilimali misitu pia yameongezeka mno. Kwa mfano, mahitaji ya mkaa ikiwa nishati ya kupikia kwa wakazi wa mijini yameongezeka kutokana na kukosekana nishati mbadala ambayo familia nyingi mijini zenye kipato kidogo zingeweza kuimudu.
Gharama za umeme, gesiasilia, gesi itokanayo na mafuta (Liquid Petroleum Gas-LPG), mafuta ya taa na umeme-jua ni za juu mno kiasi kwamba wakazi wengi wa vijijini na mijini hawawezi kuzimudu.
Kutokana na hali hiyo asilimia zaidi ya 90 hutumia mkaa unaotokana na miti ya asili. Uzoefu unaonesha kuwa kina mama wengi hawapendi kutumia mkaa kutokana na ukweli kuwa si nishati safi maana katika harakati za kutumia mkaa mhusika huweza kuchafuka ikilinganishwa na vyanzo vingine vya nishati ya kupikia kama umeme wa kawaida au umeme-jua na gesi.
Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti, Kamati ya Misitu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).
Itaendelea