Kumbukumbu  zangu zinanifahamisha ni miaka 25 sasa tangu mnong’ono wa kwanza kusikika mkoani Kagera kuwa kulikuwa na mgonjwa wa Ukimwi. Mnong’ono huo ukawa  dhahiri ilipodhihirika kuwa kuna ugonjwa wa Ukimwi nchini, mwaka 1984.

Tangu wakati huo hadi leo, Serikali, matabibu, watafiti wa wananchi kadhaa wamekuwa katika jitihada mbalimbali za kukinga na kutoa tiba kwa watu wenye Virusi vya Ukimwi (VVU) na ugonjwa wa Ukimwi, ili kunusuru nguvu kazi na uhai wa watu.

Pamoja na jitihada zote zinazofanywa za kutoa elimu kuhusu madhara ya Ukimwi, kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi na tiba ya ugonjwa huo bado mambo ni mabichi.  Bado watu wanapata maambukizi ya VVU na ugonjwa wa Ukimwi. Hili ni tatizo kwa Watanzania.

Taarifa ya Serikali, kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, na Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) nchini zinaeleza hadi sasa kuna Watanzania wagonjwa wa Ukimwi wapatao milioni moja na laki sita (milioni 1.6) kutokana na maambukizi ya VVU. Poleni wagonjwa.

Hizi si habari nzuri na za kufurahia.  Ni maelezo yenye sura ya huzuni, masikitiko na mshangao kwa sababu ndani ya miaka 25 tumekuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ambayo inaleta bughudha katika nguvu kazi na unyanyapaa katika kuuguza.

Naona woga kutamka idadi ya watu waliofariki dunia kuchelea kuamsha kilio kwa wafiwa na kutia hofu kwa wale wote waliopata maambukizi ya VVU na Ukimwi. Hapa sina budi kutoa pole kwa wale wote waliofiwa na ndugu zao.

Niseme tu, anayeishi na VVU anaweza kuishi hata kwa miaka 15 au zaidi ilimradi afuate masharti ya ushauri unaotolewa na madaktari, na kama anapata lishe bora kwa kuzingatia mahitaji yake ya afya.

Serikali na hata mtu mmoja mmoja wameonesha nia, lengo na ushirikiano katika kuzuia maambukizi ya VVU na kuondoa ugonjwa wa Ukimwi.  Lakini baadhi ya watu majumbani na mitaani bila soni wanakebehi dhamira hizo.

Baadhi ya watendaji na wauguzi katika kinga na tiba hawakutoa ushirikiano wa dhati kunusuru maambukizi na vifo kutokana na ugonjwa huu.  Laiti kama umakini ungepewa kipaumbele, leo tusingezungumzia janga hili kwa huzuni.

Familia, ndugu na marafiki wangethubutu kukinga na kutibu ugonjwa huo, maelezo yangu katika makala haya yangekuwa mazuri na matamu mithili ya tone la asali kinywani. Lakini yamekosa ladha hiyo kutokana na kiburi, choyo, inda na ujinga wa watu dhidi ya Ukimwi.

Masuala ya kebehi, puuza na nyanyapaa ndani ya jamii ya Watanzania, ndiyo yaliyotufikisha kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa Ukimwi.  Achilia mbali idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huu.  Watanzania lazima tubadili tabia. Na hapo ndipo ile ladha ya asali inapokosekana.

Mapinduzi au mabadiliko hayapo tu kwenye siasa na tabia ya nchi  bali yapo hata katika mwenendo wa mtu.  Mtu anapoweza kubadili tabia yake amefanya mapinduzi makubwa katika taratibu za kuendesha maisha yake iwe kiuchumi, kielimu au kiafya.

Baadhi ya watu hawapendi au hawajui kama ipo haja ya kubadili tabia.  Kukomesha maambukizi na kuondoa Ukimiwi.  Tume ya Kudhibiti  Ukimwi (TACAIDS) inaeleza kuwa kasi ya maambukizi ya VVU inaendelea kupungua hasa miongoni mwa vijana wa kike na wa kiume.

Tunaelezwa kutoka serikalini kuwa maambukizi ya Ukimwi kwa Tanzania Bara yamepungua kutoka asilimia 5.8 mwaka 2008 hadi kufikia asilimia 5.3 mwaka 2012. Aidha, tohara kwa wanaume imepunguza maambukizi ya VVU kwa asillimia 60.  Hii ni faraja kwetu.

Wakati mafanikio hayo yanapatikana, Watanzania hatuna budi kuungana na Serikali katika kutekeleza mpango wa kufikia sifuri tatu kwa maana ya maambukizi – o, vifo – 0 na unyanyapaa – 0; mnamo mwaka 2018.

Kwa maoni yangu wanahabari na vyombo vya habari tuna nafasi nzuri ya kuendesha kampeni hii ya sifuri 3 kama ilivyotolewa na Serikali. Hata hivyo, binafsi nina hoja zifuatazo, ambazo zinahitaji kuangaliwa.

Ni kweli vyombo vya habari vinatumika ipasavyo katika kampeni dhidi ya Ukimwi?  Wamiliki wa vyombo hivyo wamehusishwa kikamilifu? Sera za vyombo hivyo zinasemaje katika suala la Ukimwi?  Je, umma wa Watanzania umeandaliwa kupokea kampeni hiyo?

Mnyororo wa mawasiliano ya umma unazingatiwa katika vyombo vya habari, na mwisho nini msimamo na mkakati wa mwenye kampeni hiyo?