Awali ya yote namshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye kwa rehema zake nyingi anatuwezesha kuendelea kuwapo katika uso wa dunia hii.
Binafsi natambua kuwa nayaweza haya yote niyatendayo kila siku kwa sababu yupo mwenye uwezo kuliko wangu, na ndiye anitiaye nguvu na kuniwezesha ipasavyo kulingana na mapenzi yake.
Hivyo inanipasa nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa jinsi anavyotupigania na kutuongoza na hatimaye tuweze kuyamudu maisha yetu ya kila siku kwa kutumia rasilimali tulizonazo zikiwamo za madini na vito vyote vya thamani; na rasilimali nyingine kama ardhi, misitu, wanyamapori na maji.
Nikiri kwamba makala hii siyo mada kuhusu masuala ya kiroho, bali imenipasa nitangulize shukrani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye chanzo cha uhai wetu na vyote tulivyo navyo — vinavyoshikika (kama madini) na visivyoshikika kama hewa/upepo kwa sababu bila yeye kutuongoza kadri apendavyo sisi hatuwezi kitu.
Ni kwa misingi na neema hiyo imetokea kuwa viongozi wetu wameweza kuona kuwa ni vema Watanzania, hususani wazawa wakawa mstari wa mbele kwenye tasnia ya uchimbaji madini.
Tumesikia kuwa wilayani Kahama ambako dhahabu inapatikana kwa wingi, Watanzania sasa wameanza kushika usukani. Iwapo hali ni hiyo, basi ni jambo jema sana na mimi nawapongeza viongozi wahusika kwa kufanya uamuzi sahihi hadi kufikia hatua hiyo yenye kutia moyo. Hongera sana.
Madini ni mali ya nani: Watanzania au wawekezaji?
Mimi, kwa muda mrefu sana, nimekuwa nikijiuliza ni nani hasa mmiliki wa madini yanayopatikana katika ardhi ya Tanzania? Wakati wa uongozi wake, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alituonesha kuwa rasilimali madini ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu.
Akaongeza kuwa vema tusikurupuke kuyachimba maana uwezo wa kitaaluma na kiteknolojia kutuwezesha kuyachimba na kuyafaidi kama Taifa ulikuwa mdogo. Kwa mantiki hiyo, Baba wa Taifa akaagiza madini yasichimbwe. Akaagiza tuyaache kwanza hadi hapo tutakapokuwa na uwezo wa kuyachimba ili Taifa liweze kunufaika ipasavyo.
Mwalimu kwa wakati huo alijua fika kuwa tukifungua milango ya kuchimba madini bila Taifa letu kujenga uwezo imara wa kufanikisha lengo hilo ipasavyo, wataalamu na wafanyabiashara au wale wanaoitwa wawekezaji kutoka nje, ilimradi wanazo fedha nyingi; watatulalia na kutudanganya na hatimaye kuweza kufaidika zaidi kutokana na rasilimali madini tuliyonayo.
Kwa mtazamo huu, utaifa uliwekwa mbele kuliko maslahi binafsi na ilikuwa ni sera sahihi kufanya hivyo. Vilevile, msimamo huo ulinipa picha kuwa rasilimali madini ni mali ya Taifa letu au kwa maneno mengine ni mali ya Watanzania; na viongozi (kwa ngazi zote) wamepewa dhamana tu ya kusimamia na kuhakikisha Taifa letu linanufaika kutokana na uchimbaji madini, na si vinginevyo.
Changamoto
Changamoto za uchimbaji madini barani Afrika ni nyingi na karibu nchi nyingi za Kiafrika kilio chao ni Bara la Afrika kutonufaika ipasavyo na uchimbaji madini ya aina zote, ikiwamo mafuta na gesi asilia.
Mwaka 2010 nilihudhuria mkutano ulioitishwa na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika. Mkutano ulifanyika katika Makao Makuu ya Kamisheni hiyo, Addis Ababa, Ethiopia. Nilishangazwa na hoja kutoka kwa wajumbe karibu wote wakisema kuwa, “Minerals are a curse instead of being a blessing to Africa”. Hii ina maana kwamba rasilimali madini ni machukizo badala ya kuwa kitu cha baraka katika Afrika.
Karibu wote waliyasema hayo kwa hisia kali na uchungu mkubwa sana. Hii inamaanisha kuwa nchi zenye rasilimali madini barani Afrika hazinufaiki na rasilimali hizo kama ilivyotarajiwa.
Kama hivyo ndivyo, pengine tujiulize kwa nini hali iko hivyo kwa Bara la Afrika kuwa na rasilimali madini, lakini maendeleo yake kuwa duni? Kila kona kilio ni umaskini uliokithiri (persistent and widespread poverty) na tunaendelea kuwa katika lindi la umaskini wakati utajiri wa madini na maliasili nyingine (ardhi, misitu, wanyamapori, maji, samaki na mambokale) tunavyo kwa wingi katika Bara la Afrika?
Kama nilivyotangulia kueleza, Baba wa Taifa aliuona mapema udhaifu na akasema bora tujenge uwezo kwanza kuliko kukimbilia kuruhusu uchimbaji madini huku tukijua fika kuwa Taifa halitanufaika. Kilichotakiwa hapa ni Tanzania kujijengea uwezo wa kuchimba rasilimali madini (almasi, dhahabu, tanzanite, urani, makaa ya mawe, chuma, ulanga, bati, na vito vingine vya thamani pamoja na mafuta — crude oil na gesi asilia).
Kwa bahati mbaya suala la kujenga uwezo wa Taifa (kuwa na wataalamu waliobobea katika masuala ya elimu na ujuzi wa miamba na uwezo wa kuchimba na kusimamia shughuli zote na biashara ya madini, na vilevile uwezo wa kifedha — teknolojia) halijapewa msukumo wa kutosha kitaifa.
Kilichofanyika ni uchimbaji madini nchini Tanzania kupitia dhana ya uwekezaji na wachimbaji wadogo ambao pia bado wanahangaikia maisha kila mahali wanaposikia kuna madini. Uwezo wao wa kuchimba madini na hatimaye kuyasafisha tayari kwa kuuzwa, bado ni mdogo sana.
Kutokana na hali hiyo, wanachokifanya, na wengi wanasema ni shughuli za ‘kuganga njaa’ lakini siyo mwelekeo mzuri kinchi wa kuwafanya wananchi wake wanufaike kutokana na utajiri wa madini tulionao. Ili wachimbaji wadogo waweze kujipatia riziki yao ya kila siku na kuweza kukidhi haja yao kamili ya kujiletea maendeleo endelevu na yenye hadhi ya utunzaji wa mazingira, hakuna budi hatua za kitaifa na za makusudi zikachukuliwa kuwajengea uwezo.
Uwezo huo ni pamoja na mambo mengine ikiwa ni pamoja na kujiamini, kukopesheka (kupitia taasisi za fedha), kuyamudu masoko, kufanya shughuli zao kwa uhakika na kuweka maslahi ya Taifa letu mbele.
Zaidi ya mwongo mmoja uliopita, utandawazi uliingia duniani na Tanzania ikaona ni fursa mwafaka kuweza kufanya mambo yetu. Sera ya Taifa ya kujitegemea ikabadilika ikawa ni sera ya kuwakaribisha wawekezaji; na kibaya zaidi mkazo ukawekwa kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Ni kweli, mwenendo wa uchumi duniani kwa namna moja au nyingine umekuwa kandamizi hasa kwa mataifa yanayoendelea na kujulikana kama ni ‘maskini’ hasa katika Bara la Afrika. Hata kama nchi husika ina madini mengi au maliasili ya kutosha, bado inaonekena ni maskini tu na nchi tajiri kutumia udhaifu wetu wa kifikra kuweza kuzikandamiza kiuchumi nchi zinazoendelea.
Uzoefu unaonesha kuwa nchi zinazoendelea katika Bara la Afrika zisipokubaliana na matakwa ya nchi tajiri hujikuta katika hali ngumu kisiasa na kiuchumi. Hali kama hiyo haipendezi hata kidogo. Bora tukajitambua sisi tulivyo na kwa pamoja kama ‘watoto’ wa Afrika, kwa pamoja tukajizatiti kwa kuangalia uwezo wetu na tukachukua hatua bila ya kutegemea sana wenzetu wa nje.
Mimi binafsi naona kutegemea sana misaada na wawekezaji kutoka nchi zilizoendelea na tajiri kunatudumaza kifikra na kimatendo. Kwa maneno mengine, tunakuwa tegemezi zaidi kuliko kujitegemea na kujiwekea misingi ya kujiendeleza wenyewe kwa kutumia rasilimali tulizonazo.
Kwa mtazamo wangu, badala ya kukimbia kuleta watu wa nje kuchimba madini, ni bora kwanza tungelijenga uwezo wa nchi kuchimba na kuuza madini yetu wenyewe badala ya kutegemea wataalamu na wawekezaji kutoka nje.
Mimi naamini kuwa teknolojia ya kuchimba madini inafahamika, hivyo ilikuwa ni kiasi cha kuchukua hatua kama maandalizi ya kutuwezesha kuchimba madini yetu kwa kuwa na wataalamu waliobobea ambao wangeweza kuitumia teknolojia na kusimamia shughuli za kuchimba madini; hivyo kuiwezesha nchi kunufaika zaidi.
Sasa tunaongelea habari ya kuchimba gesi asilia na mafuta pengine yatajitokeza madini mengine zaidi. Je, tumejiandaa vya kutosha au ndiyo hivyo kengele imepigwa wajipange wawekezaji wa nje halafu watukalie kooni maana watajidai kuwa gesi asilia au mafuta ni rasilimali zao.
Kuna kitu kinaitwa “SONGAS” hii ni kampuni ya nani? Watanzania au watu kutoka nje ya Tanzania? Kama siyo ya Watanzania, sisi tunashindwa nini kama siyo udhaifu wa kisera na kisheria? Pengine tunaona hakuna umuhimu wa sisi kuwa mstari wa mbele katika kuumiliki uchumi wetu kupitia rasilimali kama hizo kwa kisingizio kuwa ni vitu vinavyohitaji utaalamu na teknolojia ya hali ya juu sana.
Kama hivyo ndivyo, si bora kwanza tukautafuta huo utaalamu kwa udi na uvumba tukawa nao sisi wenyewe ili tuweze kunufaika zaidi na rasilimali asilia tulizobahatika kuwa nazo hapa Tanzania? Hakuna mgeni atakayewekeza fedha zake kwa minajili ya kupata hasara.
Itakuwa wanavutwa sana na faida watakayoipata au kwa kutumia udhaifu wetu wa kutopambanua sawa sawa mambo ya kiuchumi na fedha na hatimaye kuwaachia wageni wakifanya wapendavyo na kunufaika zaidi. Hakuna usimamizi wala udhibiti wa kutosha, hivyo tunatoa mianya kwa wageni kutoka nje ya Tanzania kuweza kujinufaisha sana.
Itaendelea