Rais Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji saini Makubaliano ya Awali ya Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG Project).
Makubaliano hayo kati ya serikali na kampuni za Shell na Equinor yametiwa saini Juni 11, 2022 Ikulu ya Chamwino, Dodoma na Rais Samia amesema mradi huo wenye thamani ya Sh trilioni 70 ni wa kimkakati kwa nchi na utakapokamilika utaingiza mapato na kuinua uchumi, utazalisha ajira na kuchangia katika kujenga uwezo wa Watanzania kupitia mafunzo, elimu, uhaulishaji wa teknolojia na utafiti.
Pamoja na mambo mengine, sisi Gazeti la JAMHURI tunaunga mkono kauli ya Rais Samia kwamba sasa ni wakati wa vijana wa Tanzania kujiandaa ili kuwa na ujuzi na weledi wa kutosha kuweza kuchangamkia fursa zitakazojitokeza.
Pia tunaunga mkono majadiliano yatakayoendelea katika mkataba huo yasimamie masilahi ya nchi na kuhakikisha mikoa ya Lindi na Mtwara inapata manufaa zaidi ili vizazi vijavyo vivune rasilimali za nchi kwa tija, manufaa na kujitegemea katika mradi huo ambao ujenzi wake utakamilishwa miaka mitano baada ya uamuzi wa mwisho wa uwekezaji (FID) kufikiwa mwaka 2025.
Vilevile tunaipongeza serikali kwa kusaini makubaliano hayo kwa sababu kwa muda mrefu sasa mradi huo umekuwa na maneno chungu nzima. Kwa sababu kampuni hizo na wabia wengine walianza mchakato huu karibu miaka 20 iliyopita na wakataka kukata tamaa.
Kimsingi, tunajua kwamba faida za mradi huo ni kubwa, kwa sababu tunakoelekea mbele ya safari ni wazi dunia itaanza kutumia nishati mbadala wa mafuta katika magari na vitu vingine tofauti, pia tutaanza kuwauzia nchi majirani.
Pia sifa zilizotajwa na Waziri wa Nishati, January Makamba, zinatuchagiza kuchangamkia fursa ya mradi huo ikiwamo mazingira mazuri ya soko la rasilimali ya gesi asilia, upekee wa gesi ya Tanzania iliyo na mchanganyiko wa hewa ya kaboni na salfa ndogo zaidi tofauti na gesi zinazozalishwa na mataifa mengine duniani.
Kwamba, gesi yetu inapendwa na inakimbiliwa duniani na hatua hiyo inasababisha faida iwe upande wetu, kwa kuwa sasa hivi kuna suala la mabadiliko ya tabianchi kwa dunia kuanza kuondokana na matumizi ya nishati chafu kwenda safi.
Kwamba, fursa nyingine ni ya mwenendo wa kijiopolitiki duniani unaohusisha watumiaji wakubwa wa nishati kutafuta vyanzo vipya huku Tanzania ikiwa miongoni mwa vyanzo vya uhakika vinavyotazamwa kwa jicho la pekee na inanufaika kijiografia kutokana na ukaribu wake katika asilimia 70 ya masoko ya gesi barani Asia.