Watanzania wamehimizwa kujenga mazoea ya kutembelea Hifadhi za Taifa, kujionea vivutio vilivyopo na kujifunza mambo mbalimbali badala ya kusukuma jukumu hilo kwa wageni kutoka nchi za nje pekee.

Changamoto hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Chuo cha Udzungwa Mountain Trust (UMTC), Edgardo Welelo, akisema; “Wazawa nao wana jukumu la kuchangia Pato la Taifa kupitia sekta ya utalii.”

 

Katika mazungumzo na JAMHURI mjini Arusha hivi karibuni, Welelo amesema Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limepunguza gharama za kiingilio iki kuwawezesha wazawa wengi kuzuru hifadhi hizo.

 

“Kutembelea Hifadhi za Taifa kutawawezesha Watanzania kujifunza na kuelimika kupitia maliasili za wanyamapori, ndege na mazingira hai katika hifadhi hizo. Tusiache utajiri huu tuliojaaliwa na Mungu uwanufaishe wageni pekee,” amesisitiza.

 

Welelo amesema pamoja na malengo mengine, chuo hicho kilianzishwa ili kuchochea kasi ya kuitangaza Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa iliyopo mkoani Iringa.

 

“Chuo hiki kinalenga pia kuwezesha vijana kujua utalii. Hadi sasa wanafunzi zaidi ya 250 wamehitimu kozi za utalii, upishi, biashara, ujasiriamali, uongozi wa hoteli na watalii kwa gharama nafuu,” ameongeza.

 

Hata hivyo, chuo hicho kinakabiliwa na matatizo ya bajeti ndogo, eneo dogo na vitendea kazi visivyokidhi mahitaji ya uendeshaji.

 

Welelo ametumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa Serikali na wahisani mbalimbali, kuvisaidia vyuo vya aina hiyo kuviongezea uwezo wa kutoa mafunzo na kupanua wigo wa ajira nchini kwa manufaa ya Taifa kwa jumla.

 

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Goodluck Magalila, amewaasa wanafunzi kukazania masomo na kujiepusha na vitendo vya utovu wa nidhamu, na kuiga mila za nchi za Magharibi zinazodhalilisha utamaduni na maadili ya Kitanzania.