Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
MWENYEKITI wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Prof. Sifuni Mchome ametoa wito kwa Watanzania kwenda VETA kujifunza ili kuweza kupata ujuzi wa aina mbalimbali.
Ameyasema hayo jana jijini Dodoma alipotembelea katika banda lao lililopo kwenye maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane).
“Watanzania tukimbilie veta kupata ujuzi… ujuzi huu sasa hivi unapatikana karibu nchi nzima. Rais Samia Suluhu Hassan ametusaidia katika kujenga vyuo vingi nchini, tena vinajengwa kwa kasi kubwa na lengo ni kuongeza ujuzi katika maeneo mbalimbali.
“Veta ipo kwaajili ya Watanzania na watu wote…kwa kila rika na elimu uliyonayo. Unaweza ukawa umemaliza Chuo kikuu, Veta inakuhudumia, Veta inakuhitaji, ina ujuzi ambao unaweza kukusaidia katika maisha yako ya kawaida. Unaweza kuwa Mhasibu au Mwanasheria au umehitimu kitu chochote, Veta ina ujuzi ambao utauhitaji kuutumia katika maisha yako ya kawaida,” amesema na kuongeza kuwa:
“Wakati ambao unaona kuna changamoto ya ajira, kipato, VETA inaweza kukusaidia kupata ajira na kipato na ukafanya mambo makubwa na makubwa zaidi,” amesema.
Aidha, Prof. Mchome amesema VETA ni Kilimo pamoja na mbadala wa changamoto mbalimbali za jamii.
“Tumeona katika banda letu kuna mashine ambayo inaweza kutengeneza vyakula vya wanyama, Kuku, Ng’ombe na Mbwa. Baadhi ya vyakula hivi tunaviagiza kutoka nje na Kwa gharama kubwa.
“Fedha za kigeni zinakwenda ambazo tunazihitaji katika uchumi wa nchi yetu…sasa vitu hivi tukiweza kuvizalisha, tukakidhi matakwa ya soko la ndani tunaweza pia tukaviuza Nchi zingine ambazo hazina hizo Teknolojia. Na tukishayauza haya tutaingiza Fedha za kigeni,” amesema na kuongeza kuwa:
“Dhana hii nzima maana yake VETA ni Kilimo, na inaweza kusaidia kilimo kikaimarika na inaweza kusaidia yale tunayoyaongea kama changamoto za Kilimo zikapata ufumbuzi wake ili nchi iweze kuimarisha uchumi wake. VETA ni mbadala wa mambo mbalimbali ambayo tunaona ni changamoto,” amefafanua.