Wafanyakazi watano wa machimbo ya mawe wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa kufuatia shambulio lililofanywa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab katika eneo la machimbo katika Kijiji cha Bur Abor, Mandera Mashariki nchini Kenya.
Katika kisa kilichotokea mapema Jumanne asubuhi, wavamizi hao waliwavizia wafanyakazi muda mfupi baada ya kufika eneo hilo mwendo wa saa moja asubuhi na kulizingira gari lao na kufyatua risasi.
Wakati wafanyakazi 25 wakifanikiwa kukimbia eneo la tukio, washambuliaji waliwaua kwa kuwapiga risasi watu watano na kuwaacha wengine wawili na majeraha mabaya.
Kulingana na gazeti moja ya humo nchini, Kamishna wa kaunti ya Mandera Henry Ochako alithibitisha kisa hicho.
Kufikia sasa hakuna kikundi kilichojitokeza kuwa kimetekeleza shambulizi hilo huku raia wakitakiwa kuwa waangalifu na kuripoti wanachokijua kusaidia uchunguzi.
Kwa mujibu wa kiongozi wa mtaa wa Bur Abor, Mohamed Abdiaziz Roble ”Tunashirikiana na vyombo vya usalama kuchunguza tukio na kurejesha utulivu mtaani”.
