Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia ,Mafia
Watu watano wamefariki dunia huku wengine wawili wakiwa hawajulikani walipo baada ya boti walilokuwa wakisafiria kuzama, katika kingo za mto Rufiji,ikitokea wilaya ya Mafia Mkoani Pwani.
Aidha watu wanane katika ajali hiyo wameokolewa wakiwa hai.
Akitoa taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mafia Zephania Sumaye alieleza, boti hiyo ya wavuvi, ilikuwa na watu 15 ambapo inadaiwa kupata ajali katika kingo za mto Rufiji baada ya kugonga kuta za mto huo majira ya saa nane mchana Oktoba 30, 2023.
Amesema ,miili ya watu watano waliofariki iliokolewa Oktoba 31 ambapo amewataja baadhi yao kuwa ni mwanaume mmoja ambaye hajafahamika jina lake na mwanamke Mwanahamis Hamis (28,) mkazi wa Bungu Kibiti.
Zephania alisema ,jitihada za uokozi zinaendelea kufanywa na timu ya uokoaji ambayo tayari ilishajipanga baada ya tahadhari zinazoendelea kutolewa na mamlaka ya hali ya hewa kuhusiana na mvua kubwa kunyesha na Mafia ikiwa moja wapo ya maeneo yaliyotajwa.
” Mamlaka imetoa tahadhari na sisi tunaendelea kuwasisitiza wakazi wa Mafia na wanaozunguka bahari ya Hindi kuwa makini katika kipindi hiki kuzingatia tahadhari zinazotolewa” amefafanua Zephania.
Ameeleza kwamba, wavuvi na watu wengine wanaofanya shughuli zao kando ya bahari wanatakiwa kusitisha kwa muda ili kuepuka madhara ynayoweza kutokea.