na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Arusha

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk Pindi Chana amekitaka Chuo cha Misitu Olmotonyi kilichopo jijini Arusha kufanya utafiti katika Hifadhi ya Ngorongoro kubaini chanzo cha mimea vamizi.

Dk Chana ametoa agizo hilo leo Oktoba 16, alipofanya ziara ya kikazi chuoni hapo na kuzungumza na watumishi wa chuo hicho katika kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano Olmotonyi.

“Kwa kuwa hapa tunatoa huduma ya ushauri wa kitaalamu na Utafiti wa Misitu na Uhifadhi naomba nielekeze muwasiliane na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ili mfanye tafiti kuhusu namna ya kudhibiti mimea vamizi,” amesema Dk Chana.

Dk Chana amekipongeza chuo hicho kwa kubuni andiko la uanzishwaji wa miundombinu ya utalii na kuwasisitiza kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kufanikisha lengo hilo na kuwasisitiza kuendelea kuwajengea watumishi uwezo wa kitaalamu wapate masomo ya juu

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia utalii, Nkoba Mabula amekipongeza chuo hicho kwa kuwa na maeneo maaalumu yanayoendeleza utalii na kuahidi kufanya ziara chuoni hapo kuona maeneo hayo na kutafuta namna ya kuyaendeleza Ili kuvutia watalii zaidi.

Mkuu wa Chuo cha Misitu Olmotonyi, Dk Joseph Makero ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kukiboresha chuo hicho pamoja kuongeza idadi ya watumishi wanaopangiwa kituo cha kazi chuoni hapo.