Baadhi ya wanasheria, viongozi, wananchi na watumiaji wa dawa za kulevya wamependekeza kuanzishwa kwa Mahakama Maalum ya Dawa za Kulevya wakiamini kuwa itapunguza tatizo hili nchini, ingawa baadhi ya viongozi wamesema uadilifu ni zaidi ya Mahakama Maalum, gazeti la JAMHURI limebaini.
Kwa muda wa miezi sita, gazeti hili limekuwa likichunguza iwapo mfumo wa kisheria nchini unachangia kwa njia yoyote kushawishi wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya kuendelea na biashara hiyo, hali iliyobaini ulegevu katika sheria ya kupambana na biashara hiyo haramu.
Hata hivyo, baada ya kuchapisha mfululizo wa habari za udhaifu uliopo kisheria kuanzia mwaka 2012, ikiwamo kutaja majina ya wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya 490, hatimaye Serikali imependekeza muswada wa sheria mpya ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2015, inayorekebisha mengi kati ya mapungufu ya awali pasipo kupendekeza uanzishwaji wa Mahakama Maalumu ya kushughulikia dawa za kulevya.
Mwanasheria Deus Kibamba, Mkurugenzi wa Kituo cha Taarifa Tanzania (TCIB), ameliambia JAMHURI kuwa suala la Mahakama Maalum ya Dawa za Kulevya ambalo halimo katika muswada wa sheria mpya, liingizwe kwani litaitoa nchi hapa ilipo na kuisogeza mbele katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
“Ingekuwapo Mahakama Maalum, moja, kesi zingekuwa zinakwenda haraka, maana sasa hivi kesi zinapangiwa kalenda sawa na kesi nyingine. Hili likiwamo kwenye sheria si jambo baya, kwani halitatutoa tulipo sasa kwenda pabaya, bali pazuri zaidi. Pili litaongeza hamasa ya waandishi wa habari, wanasheria, wafanyabiashara na jamii kwa ujumla itafuatilia kwa karibu watuhumiwa siku watakapofikishwa mahakamani, na hivyo kuongeza ari na ufuatiliaji.
“Tutazidi kuwajua hata watu wanaofanya biashara hii kwa ukaribu zaidi kuliko hali ilivyo sasa ambapo kesi zao zinachanganywa tu pale Kisutu na kufunikwafunikwa,” amesema Kibamba.
Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa Mahakama ya aina hiyo ikianzishwa lazima uwepo mfumo wa kuiangalia kwa karibu isitumbukie katika mtego wa ama “wakubwa kupeleka vimemo kimyakimya ndugu zao waachiwe au wahusika kuitia mfukoni kwa kuwa wanajua itakuwa na uamuzi wa mwisho.”
Mary Chatanda, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), ameliambia JAMHURI kuwa: “Ikiwapo Mahakama ya Dawa za Kulevya, hakutakuwapo ucheleweshaji [wa kesi]. Mtu akikamatwa na mzigo leo, kesho ushahidi unatolewa anahukumiwa kifungo cha maisha jela, woga utakuwapo na watu wataacha kujihusisha na hii biashara. Huwezi kusema ni gharama kwa kitu kama hiki kinachoangamiza taifa,” anasema.
Amesema katika Bunge la Februari mwakani ambapo muswada huu utajadiliwa, atahakikisha kati ya marekebisho makubwa yatakayofanywa kwenye ‘Sheria’ hii ni kuanzishwa kwa Mahakama Maalum ya Dawa za Kulevya, watuhumiwa waweze kukamatwa na kutiwa hatiani mara moja badala ya utaratibu wa sasa ambao kesi nyingi zinacheleweshwa na hatimaye kuharibiwa.
Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, amesema mchakato wa kuwafungulia mashitaka na kuwatia hatiani wahalifu wanaofanya biashara ya dawa za kulevya unapaswa kuangaliwa kwa jicho la pekee ikiwamo mfumo wa kisheria kujengewa uwezo wa kusikiliza kesi zao kwa uharaka zaidi na kuwafunga maisha wenye kufanya biashara hiyo.
“Ni vigumu kukwepa suala la Mahakama Maalum, lakini la msingi adhabu iwe kali kwa sababu kama mtu anauza dawa za kulevya ukimpiga fani ya milioni 10, ni sawa na bure. Faini iwe ya juu sana, kiasi kwamba mtu asijaribu hata kufanya hiyo biashara, na kuongeza:
“Uwezo wa kulipa milioni 10 ni kama hela ya kununua andazi tu kwa mtu huyu. Ikiwezekana hakuna sababu ya faini, huyu ana tofauti na muuaji, ni sawa na kumwambia mtu aliyeua naye atoe faini. Hawa watu tuondoe adhabu ya faini, ni kifungo tu. Nitalipigania hili,” anasema Nkamia.
Naibu Spika, Job Ndugai, anasema sheria na mfumo mzima wa kuendesha kesi za dawa za kulevya unapaswa kupitiwa, kuepusha watu waliokamatwa na dawa za kulevya kuchukua muda mrefu bila kuhukumiwa.
Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), aliyejipambanua kupambana na dawa za kulevya nchini, amesema Bunge la Februari atahudhuria kila kikao cha kamati kuhakikisha suala la Mahakama Maalumu ya Dawa za Kulevya linaingizwa kwenye hii sheria mpya, hali itakayosukuma mapambano ya vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kasi zaidi.
Grace Kiwelu, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), ameliambia JAMHURI kuwa hukumu zikitolewa haraka hasa kwa viongozi walioko kwenye siasa na serikalini zinaweza kutuma ujumbe mzito kuwa Serikali iko makini na inapambana na vita dhidi ya dawa za kulevya.
“Rais anasema anayo orodha [ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya], lakini hadi leo anakaribia kutoka madarakani hajaitoa. Kama kuna Mahakama Maalum ya Dawa za Kulevya, hawa ‘marafiki’ zake wakatajwa, wakakamatwa leo hii na kufikishwa mahakamani kisha wakahukumiwa kifungo cha maisha jela, huwezi kuona mtu anajihusisha tena na dawa za kulevya,” anasema Grace.
Mbunge wa Arusha mjini (CHADEMA), Gobless Lema, anasema yeye kama Waziri wa Mambo ya Ndani Kivuli, haoni nia ya Serikali ya kupambana na tatizo la dawa za kulevya hapa nchini. Anasema suala la Mahakama Maalum, viongozi hawawezi kulipa nafasi kwa maana wanajua litawaumbua kwa kuwafunga haraka marafiki zao.
Godfrey Teu, Mwenyekiti wa Chama cha Watumiaji wa Dawa za Kulevya Tanzania (TanPUD), amesema anaamini Mahakama Maalumu ya Dawa za Kulevya inaweza kuwatendea haki wanaokamatwa kwa kuzushiwa kwani majaji watakaoiendesha watakuwa na uelewa mpaya juu ya “mfumo, tatizo na mwenendo” wa dawa za kulevya nchini.
Iddi Azzan Mbunge wa Kinondoni (CCM), ingawa anapinga suala la kuanzishwa kwa Mahakama Maalum ya Dawa za Kulevya, bado anataka uwepo uharakishaji wa kesi zinazohusu dawa za kulevya.
“Sikubaliani na wazo la Mahakama [Maalumu ya Dawa za Kulevya]. Tutakuwa na mahakama nyingi sana. Itaanzishwa Mahakama ya Rushwa, mwizi wa kuku, mauaji, naamini mahakama zilizopo zinaweza kushughulikia suala hili. Majaji ni wengi, mawakili ni wengi. Ni jukumu la mahakama kuendesha kesi bila kuzichelewesha, hata ukianzisha Mahakama ya Dawa za Kulevya tatizo linaweza kuwa lilelile…”
“Lakini nashangaa kwamba mtu anashuka ‘airport’ (uwanja wa ndege), kakamatwa na pipi na zimemtoka, zimeonekana, kitu gani kinacheleweshwa? Kama Mlinzi wa Amani [awepo aje] mbele ya mahakama [atoe ushahidi], hukumu inatoka mchezo unakwisha. Kuna wengine wako ndani, wengine ujanja ujanja wanapata dhamana wako nje. Kasi ya hukumu itaongeza woga,” anasema Azzan.
Anasema utaratibu wa kukamata watu kisha wakaonekana mitaani bila kuhukumiwa unawafanya vijana waone kuwa kazi hiyo ni ya maana na hawaoni tishio la kupotea uraiani hivyo wanaiendeleza.
Habari hii ni nyongeza ya habari kuu za uchunguzi ambazo zimedhaminiwa na Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa kushirikiana na Ofisi ya Kuzuia Uhalifu na Dawa za Kulevya ya Umoja wa Mataifa (UNDOC), na Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini (DCC).