DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Kwa mara ya kwanza wataalamu wazawa wa magonjwa ya moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamezibua mishipa miwili inayopeleka damu kwa wakati mmoja kwenye moyo (mishipa pacha ya damu – bifurcation lesion) iliyokuwa imeziba kwa asilimia 95 na kusababisha shida ya kupitisha damu.
Uzibuaji wa mishipa hiyo ulifanyika kwa njia ya upasuaji wa moyo kwa kutumia tundu dogo (minimum Invasive Surgery) bila kufungua kifua kwa kutoboa mshipa kwenye paja (Percutaneous Coronary Angioplasty) kwa kutumia mtambo wa Cathlab (Catheterization Laboratory) ambayo ni maabara inayotumia mionzi maalumu kwa ajili ya uchunguzi na tiba za magonjwa ya moyo.
Hayo yamesemwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na daktari mbobezi wa magonjwa ya moyo, Dk. Tulizo Shemu, ambaye pia ni mzibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa JKCI wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii mara baada ya kumaliza kufanya upasuaji uliochukua saa mbili na nusu, ukihusisha jopo la madaktari wabobezi watatu.
Dk. Shemu amesema awali uzibuaji wa mishipa hiyo pacha iliyoziba kwa wakati mmoja ulikuwa unafanyika kwa kushirikiana na wataalamu kutoka nje ya nchi, ambao hufika JKCI kutoa huduma za matibabu na mafunzo; lakini sasa wataalamu wazawa wamefanya wenyewe wakiwa peke yao.
Anasema kabla ya kufanya upasuaji huo walikuwa wanakutana na wagonjwa ambao mishipa kama hiyo ilikuwa imeziba, walikuwa wanazibua upande mmoja wa mshipa wa moyo na baada ya siku kadhaa kupita wanazibua mshipa mwingine uliobaki, jambo ambalo liliweza kusababisha mshipa uliozibuliwa nao kuziba tena na kuhatarisha maisha ya mgonjwa. Pia kufanya gharama ya upasuaji kuwa mara mbili.
“Wakati wa kufanya uchunguzi tuligundua mishipa hii muhimu ya damu ilikuwa imeziba kwa wakati mmoja tumefanikiwa kuizibua yote miwili. Kufanya upasuaji wa aina hii si rahisi, kwani ni upasuaji mgumu (Complex Percutaneous Coronary Intervention – PCI), katika upasuaji huu wataalamu wanakuwa wengi, vifaa vinavyotumika ni vingi na vya aina tofauti na tunatumia muda mrefu.
“Faida za kufanya upasuaji wa kuzibua mishipa miwili kwa pamoja ni kuokoa maisha ya mgonjwa na kuokoa gharama za upasuaji,” anasema Dk. Shemu.
Anasema mishipa ya damu ya moyo huziba kutokana na kuwapo mafuta mengi katika mishipa (cholesterol) hiyo kutokana na kula kiasi kikubwa cha chakula chenye wanga, sukari na mafuta mengi, kwani katika mwili wa binadamu mafuta yanahifadhiwa sehemu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kwenye ini, figo, moyo na mishipa ya damu.
Dk. Shemu anasema magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo yamekuwa yakisababisha vifo vya ghafla na kiharusi na kuwataka watu wanapojisikia moyo kuuma, mwili kuchoka baada ya kufanya kazi kidogo au kutembea umbali mfupi kuwahi hospitalini mapema kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kama watakutwa na matatizo ya moyo wapate matibabu mapema na kwa wakati. Wakikaa nyumbani shida zitaongezeka pamoja na hata kupoteza maisha.
“Sasa hivi magonjwa ya mishipa ya damu ya moyo yanasababisha vifo vya watu wengi, ni muhimu kubadili mtindo wa maisha kwa kula chakula bora, kufanya mazoezi, kunywa pombe kwa kiasi, kuacha kuvuta sigara na kupunguza msongo wa mawazo wanaokutana nao katika maisha. Kwa kufanya hivyo unaweza kuepuka kupata magonjwa haya,” anasisitiza Dk. Shemu.
Kwa upande wake Mama Sada Haji kutoka Zanzibr ambaye alizibuliwa mishipa hiyo ya damu alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema alikuwa anapata maumivu makali eneo la kifuani upande wa kushoto, akibeba mizigo midogo anakosa nguvu, pia anatokwa jasho jingi.
“Baada ya kujisikia maumivu nilipelekwa hospitali ya kwanza na kuandikiwa dawa za kutumia, nilizitumia dawa hizo kwa muda wa miaka minane lakini tatizo likawa linaendelea. Watoto wangu walinipeleka katika hospitali nyingine na kufanyiwa vipimo na kugundulika kuwa na tatizo kwenye moyo, daktari akanituma kuja kutibiwa hapa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Baada ya kufika hapa na kufanyiwa vipimo siku ya Alhamisi iliyopita niliambiwa mishipa miwili ya damu ilikuwa imeziba na inatakiwa kuzibuliwa,” anasema.
“Siku ya Jumatatu Aprili 04, 2022 nilifanyiwa upasuaji wa kuzibuliwa mishipa hiyo. Baada ya kufanyiwa upasuaji huo sasa hivi najisikia vizuri, maumivu hakuna tena kama ilivyokuwa awali, ninakula chakula vizuri na daktari ameniambia nitaruhusiwa kurudi nyumbani siku chache zijazo,” anasema Mama Sada.
Mama Sada aliwashauri watu wenye matatizo kama yake wasikate tamaa, wakihisi maumivu waende hospitalini wakafanyiwe uchunguzi kwani vifaa vipo na wataalamu wapo wanaotoa huduma za kuzibua mishipa ya damu ya moyo.