Na Mwandishi Wetu,WHMTH,Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Jim Yonazi ametoa rai kwa wataalamu 79 waliohitimu mafunzo ya uendeshaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano yaliyotolewa na Kampuni ya HUAWEI Tanzania kuhakikisha wanalitumikia Taifa kwa weledi na uzalendo mkubwa ili kutekeleza ajenda ya uchumi wa kidijiti.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti wataalamu hao jijini Dodoma jana,Dkt.Yonazi amewataka wataalamu hao kuhakikisha wanafanya vizuri katika maeneo yao ya kitaaluma na kuishauri Serikali nini kifanyike ili Mkongo wa Taifa uendelee kuleta ushindani wa kiuchumi utakaoleta tija kwa Taifa na wananchi kwa ujumla.
“Ni heshima kubwa kupata fursa ya kuitumikia nchi, kuhitimu mafunzo haya sio kwa ajili ya kupata cheti tu, bali kuboresha mwenendo na utendaji wenu katika kutumikia taaluma na ujuzi mlioupata kwa manufaa ya nchi”, amesisitiza Dkt. Yonazi.
Ameongeza kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia ya TEHAMA wataalamu hao wanatakiwa kuwa na utamaduni wa kujifunza mara kwa mara ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kuwa chachu kwa wengine.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Miundombinu ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Mhandisi Nikusubila Mwambije amesema kuwa jumla ya wataalamu 114 wamepatiwa mafunzo hayo ambapo wahitimu hao 79 waliotunikiwa vyeti wamepata mafunzo ndani ya nchi kwa siku 10 na wataalamu 35 watapata mafunzo hayo nje ya nchi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yaliyotolewa kwa wataalamu hao kutoka Wizara ya Ulinzi na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) ni muhimu kutokana na ufungaji wa mitambo ya teknolojia ya kisasa ya kuendesha Mkongo wa Taifa iliyofungwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wa Mkurugenzi Msaidizi wa HUAWEI Tanzania Tom Tao amesema kuwa kampuni ya HUAWEI Tanzania itaendelea kushirikiana na Wizara hiyo kuleta mapinduzi ya kidijiti kwa kushiriki katika usambazaji wa miundombinu ya TEHAMA na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha TEHAMA kwa nchi za zinazoizunguka.
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari