Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha

Wataalamu wabobezi katika sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi wamekutana jijini, katika kongamano la siku moja kwa lengo la kujadili mchango wao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kongamano hilo limeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuongeza uelewa kuhusu shughuli za Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) ambapo ripoti zitakazoandaliwa katika mzunguko wa saba wa IPCC (AR7) kuhusu tathmini ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na fursa za kushiriki katika mchakato huo, ikijumuisha uandishi, uteuzi wa wataalamu na mapitio ya ripoti za IPCC.

Akizungumza juzi jijini Arusha  Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa(TMA),Jaji Mshibe Ali Bakari amesema ushiriki wa wataalamu wengi kutoka Afrika Mashariki katika mchakato wa IPCC inaonesha ni namna gani wanatoa mchango wao kikamilifu katika utayarishaji wa ripoti za tathmini ya saba ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ya IPCC.

“Ni matumaini yangu kuwa kupitia makongamano kama haya ya uhamasishaji wa wanasayansi kujihusisha katika kufanya tafiti zinazokidhi matakwa ya IPCC, wataalam wengi zaidi kutoka Afrika Mashariki wataweza kutoa mchango wao kikamilifu katika utayarishaji wa ripoti za tathmini ya Saba ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ya IPCC (IPCC AR7),”amesema Jaji. Mshibe.

Amesema  kongamano hilo lilihamasisha wanasayansi hasa vijana, watendaji, wakufunzi na wanafunzi kufuatilia na kushiriki katika mchakato mzima wa shughuli za IPCC hasa katika mzunguko wake wa saba ulioanza mwaka 2023 na unatarajiwa kumalizika kati ya mwaka 2029 na 2030.

Naye, Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa IPCC amesema namna ambavyo ripoti za IPCC zimekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kimataifa na katika nchi moja moja. 

Ripoti ya IPCC ya AR7 inayoandaliwa inatarajiwa kuwa ya kina na itakuwa na jukumu muhimu katika mustakabali wa hatua za kuchukua dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa natabianchi kwa kuzingatia taarifa za kisayansi zilizohakikiwa vyema ambapo zina mchango mkubwa katika kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kikanda na Duniani kote”. Amesema Dkt. Chang’a.

Kongamano hilo limeratibiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, likijumuisha wataalamu wa sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tasnia zinazohusiana kutoka Tanzania na Afrika Mashariki.