Wananchi wa Kata ya Makata katika Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi, wamesema hawatashiriki shughuli za kisiasa kwa madai ya kutelekezwa na wanasiasa na Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kutowapelekea huduma za kijamii kwa muda mrefu, JAMHURI limeambiwa.
Wamesema mgomo huo wanauanzia uchaguzi ndani ya vyama na chaguzi za kiserikali za mitaa kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa.
JAMHURI limefika katika kata hiyo, iliyopo umbali wa kilomita 12 kutoka Liwale mjini, na kuambiwa na wananchi kuwa wanakusudia kuchukua hatua hiyo kutokana na halmashauri hiyo kuitelekeza kata yao kwa kutopeleka miradi ya maji, afya na elimu kwa muda mrefu.
“Makata hatutaki siasa tena, haina maana wala faida kwetu kuchagua viongozi kwa sababu wameamua kututenga, ngoja tuishi kama ndani ya kisiwa,” alisema Haji Kipungo (74), mkazi wa kata hiyo.
Amesema wameamua kuikataa siasa kuanzia uchaguzi huu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ngazi ya shina na tawi na kwamba utaratibu huu utaendelea kwa vyama vyote hadi Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 iwapo halmashauri na wanasiasa wataendelea kutotatua kero zinazowakabili.
“Hakuna sababu ya kufanya uchaguzi wa kuunda uongozi kwa sababu hoja zetu hazitekelezwi. Taarifa za uamuzi huu tumekwisha wafikishia halmashauri na vyama vya siasa vyote. Tunapenda salamu hizi zimfikie pia Rais John Magufuli kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale imetutelekeza kwa kipindi kirefu sana, sasa basi inatosha,” amesema.
Wananchi hao wamechukua hatua hiyo kutokana na kutokuwapo kwa huduma ya maji katika kituo cha afya na kutelekezwa kwa ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya kata hiyo.
“Tatizo la maji linapelekea (sababisha) watu kuhatarisha maisha yao kutokana na uwepo wa wanyama wakali. Watoto wetu wanafuata maji kwa kutembea umbali mrefu sana, halmashauri inatuzungusha kana kwamba sisi ni watoto ilhali tarafa za Kibutuka na Liwale mjini zinahuduma zote. Mipango ya miradi ya maji imekuwapo kwa vipindi vyote vya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, ambapo mingine ilianzishwa na kutelekezwa bila kumalizika.
Makata ilipata hadhi ya kata mwaka 1975 na kufanywa kuwa makao makuu ya Tarafa ya Makata. Wakazi wake ambao ni zaidi ya elfu saba wanailaumu halmashauri kwa kutowapelekea huduma za kijamii tofauti na inavyofanya katika tarafa za Kibutuka na Liwale mjini.
Katibu wa Baraza la Wazee wa Kata ya Makata, Mohammed Liunilo, amesema kuwa shida ya maji katika kata hiyo ni ya siku nyingi.
“Tenki la maji Makata lilijengwa kati ya mwaka 1983/84 lengo likiwa ni kuwawezesha wananchi kupata maji kwa kuyavuta kutoka mto Makata ambao upo umbali wa kilomita tatu. Ililetwa mashine ya kuvuta maji hayo miaka hiyo hiyo maji yakawa yanavunwa kutoka mto Makata ambako kulijengwa kituo cha pampu na huduma hiyo ilidumu kwa muda wa mwaka mmoja tu,” amesema.
Liunilo amesema Mhandisi wa Maji Halmashauri ya Liwale alifika katika kata hiyo na kuichukua pampu hiyo kwa madai kuwa Mwalimu Julius Nyerere alikuja katika ziara Liwale kukagua miradi ya maji na kwa sababu pampu ilikiwa mbovu, walikuja kuazima yao ambayo haikurudishwa hadi sasa.
Amesema kuwa Kata ya Makata imepakana na Hifadhi ya Selous na inazungukwa na mapori ya Kitumbinungu, Lutete, Libumbu na Kikuti.
Naye Mosi Ngomambo amesema kwa miaka mingi wamekuwa wakitegemea maji ya mto Makata ambayo hukauka baada ya masika kwa sababu yanatiririka kuelekea vijiji vingine.
“Kuna kisima kimechimbwa pembeni mwa mto huo na mfadhili ambacho hukauka pale tu maji ya mto yanapokata. Ni mwezi mmoja sasa maji yakichotwa kwa muda wa saa tatu katika kisima hicho yanatoka yakiwa na rangi ya kutu. Kipo kisima kingine ambacho watu wa Makata huchota maji, kipo Mpindimbi umbali wa nusu saa kwa mguu. Na hayo maji yanapatikana kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa nane. Ukipita mwezi huo inabidi kuamka saa tisa usiku kwenda kutafuta maji. Huku tumezungukwa na mapori yenye wanyama. Ni hatari kuchanganyikana nao katika kutafuta maji. Watu wanauawa na wengine wanajeruhiwa na chui katika harakati za kupata maji kwa sababu tunachangia vyanzo vya maji.
“Mama yangu katikati ya mwezi Juni mwaka huu alivamiwa na chui huko kijiji cha Mitawa akitafuta maji. Kutokana na shida ya maji, tunaiomba Serikali itukumbuke. Maji tunayapata katika mazingira hatarishi, simba na chui wapo huku. Hata huo mto Makata upo porini,” amesema Adam Mtagaju.
Kwa upande wake, Salima Lipala (70), mama yake Mtagaju, amesema kuwa alivamiwa na chui wakati anakwenda kuteka maji katika chemchemi
“Ni Mungu tu amenisaidia, aliponivamia nilikuwa na kisu ambacho nilikibeba kwa ajili ya kuchanjia kuni, nilikitumia kujihami kwa kumkata nacho usoni. Nilipiga yowe ambapo mume wangu alisikia na kupiga yowe pia; bahati nzuri kulikuwapo na vijana kama watatu mashambani ambao walikuja mbio. Alinijeruhi usoni na kuning’ata mguuni. Nilijikata kiganja kwa hofu nilipokuwa natetea uhai wangu,” amesema Salima.
Muuguzi wa Zahanati ya Makata, Fraja Jordan Salima Lipala, alifikishwa katika zahanati hiyo Juni 20, mwaka huu, na kushonwa nyuzi 12 na kuchomwa sindano ya tetenasi baada ya kujeruhiwa na chui wakati alipokuwa akifuata maji.
Mwananchi mwingine, Ahmad Likwalile, amesema Halmashauri ya Wilaya ya Liwale iliwaambia wakazi wa Makata kuchangia fedha za mradi wa maji baada ya Benki ya Dunia kuonesha nia ya kusaidia mradi huo.
Amesema ilipofika mwaka 2011 Benki ya Dunia ilipeleka mradi wa maji na wananchi kutakiwa kuchangia Sh milioni 10 lakini zilichangwa Sh. milioni 8/- kutoka kwenye mfuko wa maendeleo ya kijiji na kuiweka fedha hiyo kwenye akaunti ya mfuko wa maji wa kijiji.
“Alipokuja Scott ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Go Drill International, na ambaye ndiye amefadhili uchimbaji wa kile kisima kilichopo jirani na Mto Makata, tukamwambia sisi tumekwishachanga fedha ambayo tunataraji kupata maji ya bomba kwa fedha hiyo na msaada wa Benki ya Dunia; hivyo sisi hatukuwa na chochote cha kuchangia ujenzi wa kisima kile.”
Scott alikichimba kwa fedha yake mwenyewe kama msaada. Tumekuwa tukiuliza fedha hii ilipo hatupewi majibu wala mchanganuo wa namna ilivyotumika kutoka kwa mkurugenzi.
Walituambia mradi huo ungeligharimu Sh milioni 250 ambao ulikuwa ni wa kuchimba kisima kirefu chenye uwezo wa kuvuna maji ya mvua pia na kwamba kungesambazwa mabomba Makata; huo mradi tunaweza kusema umekufa maana ni miaka zaidi ya mitano sasa na sisi tunasota na kero ya maji. Tumechoka hatutaki wanasiasa tena na wala chama chochote kisije kufanya siasa Makata,” amesema Likwalile.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Liwale, Omary Chingwile, amekiri kuwapo kwa tatizo la maji na kwamba jambo hilo linashughulikiwa kulingana na wakati unavyokwenda. Serikali itashughulikia yote hayo na wala wananchi hawana sababu ya kususia shughuli za kisiasa katika kata hiyo.
Hata hivyo, Chingwile hakuwa tayari kuweka bayana kiasi cha fedha ambacho halmashauri hiyo imetengewa na Serikali kwa ajili ya uendelezaji sekta ya maji katika mwaka wa fedha 2017/18.
“Tunachokifanya sasa ni kukiweka kijiji hicho kwenye mpango wa maji vijijini ambapo kila tarafa inatengewa vijiji 10. Mpango huu ulianza mwaka wa fedha 2015/16. Kunahitajika Sh bilioni moja kwa ajili ya kuweka mtandao wa maji Makata, Mpengele na Kigwema,” amesama Chingwile.
Naye Mhandisi wa Maji wa Wilaya, Andrew Kilembe, amesema kuwa katika hatua ya kukabiliana na tatizo la maji Makata, mwaka jana kulichimbwa kisima cha pampu ya mkono kwa ufadhili wa Kampuni ya Go Drill International.
“Hapo siku za nyuma kulikuwapo mpango wa mradi mkubwa wa maji, ila haukutekelezwa kulingana na chanzo cha maji ambao ni mto Makata kukauka mara kwa mara. Mwaka 2016/17 tulikuwa na mpango wa upatikanaji wa maji kupitia mpango wa maji safi na mazingira vijijini unaohusisha vijiji 10 ikiwamo Kata ya Makata. Mwaka huo wa fedha hatukupata pesa ya kutosha, hivyo haukutekelezeka Makata.
“Tulipewa Sh 831,919,000 ambapo tulitakiwa kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Likombola, Kipule na Ndunyungu. Mwaka 2014/15 tulitekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Barikiwa, Mpiga miti na Namiu; mwaka 2015/16 tulitekeleza katika vijiji vya Mbaya, Namtumbwa, Kichonda, Mitawa na Namakororo. Mwaka huu wa fedha 2017/18 mradi wa maji utatekelezwa katika vijiji 15 kikiwamo cha Makata.
“Lakini inategemeana na kiwango cha fedha tutakachokipata. Sasa tumepokea barua kutoka Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambayo inatupa idhini ya kuandaa andiko la kuomba fedha ya kufanyia upembuzi yakinifu ili kupata gharama sahihi ya mradi huo. Halmashauri, kwa kushirikiana na Kampuni ya Go Drill International, tumeweza kuchimba visima 15 katika tarafa zote tatu za Kibutuka, Liwale na Makata. Miongoni mwa hizo, tarafa ya Makata kuna visima viwili, cha mto Makata na cha kijiji cha Mkutano,” amesema Mhandisi Kilembe.
Mbunge wa jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka, amesema kuwa atafanya ziara katika Kata ya Makata ili kuzungumza na wananchi hao kuhusiana na kero zinazowakabili.
“Mimi nimekuwa bungeni kwa miezi mitatu mfululizo. Kwa sababu Bunge limekwisha, nitakwenda kuzungumza nao. Hatua waliyoifikia ya kususia shughuli za siasa kufanyika katika kata nzima siyo nzuri na inaweza kuwa na madhara makubwa kwao na sisi waliotuchagua,” amesema.
Diwani wa Kata ya Makata, Mfaume Mpungu, amekiri kufahamu uwepo wa mgomo wa kushiriki katika shughuli za kisiasa kwa wakazi wa kata hiyo.
“Hizo taarifa za kugomea shughuli za kisiasa nazifahamu. Wamegoma kuchukua fomu za kugombea nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi huu mdogo wakishinikiza kutatuliwa kwanza matatizo yao. Hoja hiyo iliibuka kwenye kikao cha Baraza la Maendeleo ya Kata cha mwezi Aprili mwaka huu. Kwamba hatua hiyo ni shinikizo la kuonesha kuwa wametelekezwa na viongozi. Nafahamu pia wana mpango wa kuifunga ofisi ya kata ambayo wamejenga kwa nguvu zao. Mimi sina uwezo peke yangu wa kushughulika na kero zote, hivyo malalamiko yote nimekwisha yafikisha katika ngazi ya halmashauri. Sasa siwezi kuiamuru halmashauri kutenda kinyume na inavyopanga,” amesema Mpungu.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu, upatikanaji wa maji vijiji ni wa asilimia 36 na mijini ni asilimia 37.
Na FRANCIS KAJUBI