Wastaafu wa kada mbalimbali serikalini wameitaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini ya Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, kuonesha hati ya Mungano wa Unguja na Pemba iwapo visiwa hivyo viliungana kisheria na mkataba kutambuliwa na Umoja wa Mataifa.
Uchunguzi wa JAMHURI umebaini hayo katika kongamano lililoitishwa na Jumuiya ya Wakulima na Wafanyakazi wastaafu Zanzibar lililofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari huko Makunduchi, Mkoa wa Kusini, Unguja, wiki iliyopita.
Kongamano hilo likiwa chini ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja, Ali Hassan Khamis, katika utawala wa Awamu ya Sita Zanzibar chini ya Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume, washiriki wameendelea kuhimiza visiwa hivyo kila upande kupata mamlaka yake kamili kama taifa.
Mjadala uliokuwa na mada mbili; za historia ya Zanzibar kuadhimisha Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na ile ya siasa na dini zilizowasilishwa na Ramadhani Nzori pamoja na Mwalimu Wahidi Kavishe. Mshiriki Zahra Abdulrazaq Mussa alisema kukithiri kwa mivutano na migongano ya kimawazo, kiitikadi na kiasili kunaweza kuleta hatari, hivyo umefika wakati jambo hilo kupatiwa utatuzi na kuoneshwa hati ya Muungano ya visiwa hivyo.
Zahra alisema ikiwa wazee kutoka Pemba waliwahi kutaka himaya ya kisiwa chao na mamlaka kamili, watu wenye asili ya Unguja nao wana wajibu wa kuvumiliwa ili kujitenga na wenzao wa Pemba.
Alisema mwaka 2001 kundi la wazee kutoka Pemba chini ya Mwenyekiti wao, Hamad Ali Mussa, aliyewahi kuwa Mbunge wa Ole, walifika Ofisi za Umoja wa Mataifa Dar es Salaam, wakitaka kujitenga na Unguja, hivyo sasa ni zamu ya Unguja kupewa miliki ya kisiwa chao na mamlaka kamili.
“Misuguano na mivutano hii inatisha. Pemba na Unguja watu wake siku moja wataingiana mwilini, njia pekee ni kila upande uwe na mamlaka, ioneshwe hati ya Muungano kama ipo, tusilazimishane,” alisema Zahra.
Aidha, Zahra alisema umefika wakati wa mipaka ya Unguja na Pemba itambulike, hati ya Muungano isomwe kipengele kwa kipengele, tarehe na mwaka wa kuungana ufahamike na kama hakuna kila upande uamue mambo yake.
Zahra ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe Abdulrazaq Mussa Simai (Kwacha), alihoji masafa kutoka Pemba hadi Unguja kuwa ni marefu yenye umbali kuliko Unguja na Tanganyika (Mrima), hivyo umbali huo unathibitisha si eneo moja.
Vuai Ali Haji, anayeishi Paje, Mkoa wa Kusini, alisema madai ya muda mrefu ya watu wa Pemba ni kutaka Serikali yao, viongozi wa SMZ na SMT hawana haki wala wajibu wa kuwanyima haki hiyo huku akisema njia ya kiungwana ni wananchi hao kupewa mamlaka yao.
Alisema ikiwa viongozi waliopo madarakani hawaoni Zanzibar inakoelekea na tishio la kuvurugika kwa amani, utulivu na umoja kutokana na kukithiri kwa madai ya watu wa Pemba na Unguja, lolote linaweza kutokea.
“Uvumilivu una ukomo wake, heri uwepo Muungano wa Tanganyika na Unguja wa Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume kuliko kuvutana kila kukicha, wapeni kisiwa chao, Waunguja tumechoka, hatuna cha kupoteza kwa kutengana nao,” alisema Vuai.
Maryam Pandu anayeishi Bwejuu akichangia, alisema waliopindua nchi kutoka mikononi mwa Sultan wa Oman, ndiyo wenye haki kulinda na kutetea Mapinduzi na kwamba inashangaza kusikia watu ambao hawakushiriki Mapinduzi Matukufu wakidai nchi yao.
Mshiriki huyo alisema Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 yalikuwa ni Mapinduzi ya Mungu kuwanusuru watu waliokandamizwa miaka mingi, hivyo yanapotokea makundi ya ovyo ovyo yakidhihaki na kukejeli, ni matusi na aibu kwa ASP na viongozi waliobaki.
Simai Jafari Bai, mkazi wa Kijiji cha Bambi, akichangia alisema Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ni kwa ajili ya kukomboa watu wa Unguja ambako ndiko kulikokuwa shina la mateso, kubaguliwa, kutumikishwa, kunyimwa ardhi, elimu na huduma za jamii na kwamba madhila hayo hayakuwasibu watu wa Pemba.
Hata hivyo, Simai aliwaasa wananchi wa Unguja akiwataka waache kuuza ardhi na nyumba za umma kwa matajiri, ambazo walipewa katika utawala wa Rais Abeid Karume na kuitaka SMZ izuie jambo hilo baada ya kuonekana watu wa Unguja kuwa ni madalali wa kuuza utu na ardhi iliyo na rutuba.
“Iko hatari ya kutokea vita ya ardhi kama Palestina na Israel. Wananchi wanauza ardhi na nyumba walizopewa na SMZ. Siku moja wanaouziwa watadai ni zao, wanyonge watakosa pa kuishi, kulima na maeneo ya kuzikana,” alisema Simai huku akishangiliwa.
Pia aliwatahadharisha wananchi wa Kisiwa cha Unguja kubaini mpango mkakati wa watu kutoka Pemba, wanaohamia kwa kasi Unguja na kusema bila ya tahadhari, Unguja itamezwa na Pemba kwa sababu watu kutoka Unguja hawana dhamira ya kuishi Pemba.