Wastaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wanaendelea kuhangaikia madai ya mapunjo ya mafao yao, safari hii wakidhamiria ‘kumwangukia’ Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha.
Wastaafu hao wapatao 933 wanadai kupunjwa zaidi ya Sh bilioni saba za mafao huku wakiituhumu Wizara ya Fedha kuwa ndiyo kizingiti kikuu cha ufumbuzi wa suala hilo kwa zaidi ya miaka 16 sasa.
Mwenyekiti wa wastaafu hao, Rashid Mohamed, ameiambia JAMHURI Dar es Salaam juzi, kwamba wameahidiwa kwenda kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha wiki hii.
“Tumehangaikia suala hili tangu mwaka 1997, tumekwenda kwa viongozi mbalimbali wa Wizara na Ikulu hatujapatiwa ufumbuzi, sasa tuna ahadi ya kukutana tena na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha,” amesema.
Ahadi ya kukutana na Katibu Mkuu huyo imekuja wiki moja baada ya baadhi ya watumishi wa Hazina kutishia kuwasweka rumande viongozi wa wastaafu hao walipokwenda kuuliza hatma ya madai yao.
Wiki moja kabla ya kutishiwa hivyo, viongozi hao walifanya mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam na kutaka Ikulu iwaombe radhi ndani ya kipindi cha siku saba kwa kuwaita waongo.
Hivi karibuni, Msaidizi wa Rais – Ikulu, Kassim Mtawa na Katibu wa Rais, Prosper Mbena walipotakiwa na JAMHURI kuzungumzia malalamiko hayo walisema wastaafu hao ni waongo, madai yao hayana ukweli wowote.
JAMHURI inaendelea na juhudi za kumpata Msajili wa Hazina, Elipina Mlaki aweze kufafanua suala la madai ya wastaafu hao.