Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi-Dar es Salaam

Wasomi na wanazuoni wameliomba Jeshi la Polisi kuendana na mabadiliko ya duniani ya sasa ambayo imejikita zaidi katika tehama na tafiti ambazo zitaleta tija katika jamii na Taifa kwa ujumla husasani katika kukabiliana na uhalifu ukiwemo wa kimtandao ambao umeshika kasi kwa sasa.

Akiongea leo mara baada ya kukabidhi vitabu zaidi ya mia tano vilivyo katika nakala laini katika chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam (DPA) Daktari Hilderbrand Shayo kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam amesema kuwa kwa sasa dunia imebadilika ambapo wameona vyema watoe vitabu hivyo kwa ajili ya kuwajengea uwezo mkubwa wa kitaaluma askari wa Jeshi la Polisi waliopo katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.

Ameongeza kuwa lengo la kutoa vitabu hivyo ni kuweza kujenga uwezo mpana kwa askari katika nyanja mbalimbali ikiwemo tehama na maswala ya jinsia ambayo yamekuwa ni changamoto katika jamii yetu.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam Kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Daktari Lazaro Mambosasa amebainisha kuwa kitendo cha kupatikana kwa vitabu hivyo zaidi ya mia tano vinakwenda kuongeza maarifa na ujuzi kwa askari wa Jeshi hilo.

Nae Profesa Beatus Alois Kundi ambae ni mkuu wa kitengo cha uhandisi kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam amesema, bila kuwa na muongozo mzuri ambao utasimamia mabadiliko ya Jeshi ni vigumu kuja na matokeo chanya kwa taifa ambapo amebainisha kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Msataafu IGP Saidi Mwema yeye ametoa dira kwa Jeshi la Polisi kutokana na uandishi wake wa kitabu alicho kizindua siku za hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Johari Rotana jijini Dar es salaam.

Sambamba na hilo Mkuu wa kitengo cha utafiti cha Jeshi la Polisi kilichopo katika chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam Kamishna msaidizi wa Polisi Ralph Meela amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Wambura kwa kutoa mwelekeo wa matumizi ya teknolojia katika kupambana na uhalifu hapa Nchini.

Kwa upande wake mwanafunzi wa kozi ya uofisa Rose Mbaga amewashukuru wanazuoni hao kwa kutoa vitabu hivyo ambavyo vitawaongezea maarifa katika utendaji wa kazi mara baada ya kumalza mafunzo yao, ameongeza kuwa elimu hiyo inakwenda kuwafikia maofisa na askari wengine katika maeneo mbalimbali hapa Nchini.