Wasira: Viongozi wa dini wametutia
nguvu kuendelea na uchaguzi mkuu
*Asema ushauri wao pamoja na wadau wengine utaendelea kuzingatiwa
*Asisitiza kuwa Dk. Samia kwa miaka minne amefanya kazi kubwa
*Atoa mwanga jinsi ilani ijayo ya CCM itakavyoleta ahueni kwa wakulima
Na Mwandishi Wetu, Chamwino
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewashukuru na kuwapongeza viongozi wa dini kwa ushauri kuhakikisha mchi inaendelea kuwa na amani hususan kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu na kubariki uchaguzi huo uendelee huku, ikisisitiza kuwa haidharau maoni yanayotolewa.
CCM imesisitiza kuwa haipuuzi ushauri mbalimbali unaotolewa kuelekea uchaguzi huo, lakini imesisitiza hautaahirishwa kwa kuwa mageuzi na mabadiliko ni jambo endelevu na haiwezi kuwa hoja ya kuahirisha uchaguzi.
Hayo yalielezwa jana Chamwino mkoani Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alipokuwa akipokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo.

“Uchaguzi utaendelea sio kwamba tunapuuza mawazo, tutaendelea kuzungumza mambo ambayo yanaendelea, na tunashukuru sana nchi imetulia. Viongozi wetu wa kiroho wametuongoza wametupa ushauri mzuri sana na mimi nashukuru sana kwa kututia moyo na kutuambia uchaguzi uendelee lakini kwa amani,” alisema.
Wasira alisema CCM ni Chama kinachozungumza na kuhimiza amani ndio maana taifa limekuwa na utulivu kwa miaka 60, alisisitiza kwamba hilo linafanya Chama kijivunie kwa kuwa ni ushahidi kwamba kinaweza kusimamia amani.
Alisisitiza haki iko ndani ya amani na kwamba ukiondoa amani utavunja haki za watu wengi hususan wanyonge, “ukiondoa amani watakaoumia hasa ni wanawake, watoto na walemavu.”
“Amani ni lazima sasa kuna wanaosema haki, na sisi tunasema ndani ya amani kuna haki, na haki hiyo inalindwa na amani kwa sababu ukiiondoa watu wengi wataathirika wala sio mtu mmoja ni wengi sana na ushahidi wake upo, sisi tumepokea wakimbizi maelfu kutokana na kuvunjia kwa amani kwa majirani zetu,” alisisitiza.

MKAKATI KUIMARISHA UCHUMI
Akizungumzia kuhusu Akilimo na uzalishaji wa chakula Wasira alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM ijayo, pqmoja na mambo mengine itatilia mkazo zaidi uzalishaji hususqn kwa wananchi walioko vijijini kupambana na umasikini.
“Umaskini unaweza kuondoshwa kama unawasaidia watu wa vijijini wapate njia bora ya uwekezaji, Progaramu ya Jenga Kesho Bora (BBT) ikiwa ‘transformed’ (ikiboreshwa) kaenda kila mkoa na wanakijiji sio tu kwa vijana wasomi itabadilisha maisha.
“Umwagiliaji ni lazima usambazwe na kwa kweli ninampongeze sana Rais Samia (Dk. Samia Suluhu Hassan), mimi nilikuwa Waziri wa Kilimo tatizo ambalo lilitukabili katika umwagiliaji ni kutokuwa na mfumo maalumu wa usimamizi wa suala hilo, kama huna hela humwagilii, utamwagilia na mvua tu kwa sababu miundombinu ya umwagiliani ni gharama,” alisema.
Alieleza kwa mfano Vietnam ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya kilimo kuliko nchi yoyote, “ukiweka ‘iregation’ Dodoma italeta mabadiliko kwa sababu mvua za hapa hazitabiriki.”
“Sasa mkifanya umwagiliaji kitu kinaichoitwa njaa na umasikini vitaisha, kwa hiyo uangaliwe uwezekano wa kutumia maji ya mvua kutengeneza mabwawa ya kufanya umwagiliaji ili watu inapowezekana walime kwa kutumia trekta badala ya jembe la mkono ambalo ni shingo ya umasikini.
“Jembe la mkono kwa sasa kwa vijana ni tatizo, na watu tusiwategemee sana kulima kwa jembe la mkoni.Hiki kitu katika ilani inayokuja tutatazama uwezekano wa kuweka mfumo matrekata ya kutoa huduma ili wakulima wawe wanatumia na kurudisha kwa kulipia,” alisma.
DK. SAMIA ANAKWENDA VIZURI
Akizungumzia kasi ya maendeleao, Wasira alisema kwa kipindi cha miaka minne nchi chini ya Rais Dk. Samia imszidi kupiga hatua kubwa.
“Kazi ambazo amezifanya Rais Samia kwa miaka minne ni kubwa. Maana unauliza tumetoka wapi na tuko wapi miaka minne baada ya kifo cha Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye kaulimbiu yake ilikuwa hapa kazi tu, nchi imeendelea kuimarika.
“Rais Samia akaja na kaulimbiu kwamba kazi iendelee na kazi imeendelea. Reli ya SGR aliachiwa karibu kufika Morogoro, leo hii ipo Makutupora (Singida), viipande vinavyobakia kutoka Mwanza kimoja kipo asilia 86 kwenda Isaka na kutoka Isaka kwenda Tabora kazi inaendelea,” alisema.

