*Awapa darasa wanaodai sababu ya CCM kupitisha wagombea urais
*Asema yupo tayari kuwapa somo waifahamu vyema katiba ya chama
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema uamuzi wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliomchagua Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umezingatia Katiba ya chama na mamlaka ya mkutano huo.
Akizungumza leo Januari 26, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa mapokezi yake yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Wasira alisema kuwa baadhi ya wanaojiita wanachama wa CCM ambao hawajaelewa uamuzi huo wanapaswa kufundishwa.
“Baada ya Mkutano Mkuu kutambua kazi kubwa zilizofanywa na serikali zote mbili, Mkutano huo uliona hakuna sababu ya kuchelewesha kutangaza mgombea. Kama kuna watu hawajaelewa, tutawasaidia maana si kila mtu anaweza kuelewa sawa,” alisema Wasira.
Wasira alisisitiza kuwa Mkutano Mkuu wa CCM, kwa mujibu wa Katiba ya chama, ndiyo chombo chenye mamlaka ya mwisho ya kufanya maamuzi.
“Mkutano Mkuu una mamlaka ya kubadili, kurekebisha au kufuta maamuzi yoyote ya kikao cha chini yake. Wanachama wenu walipokutana wakaridhika, wakatumia mamlaka yao kumpa Dkt. Samia kipindi kingine cha miaka mitano. Kama huelewi, njoo kwangu nikufundishe maana Katiba ipo kichwani,” alisema.
Aliongeza kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilikutana kwa dharura kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikizuia uamuzi huo. Hii ilihusisha pia Kamati Maalum ya Zanzibar kumteua Dkt. Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais wa Zanzibar, kabla ya uteuzi wa Dkt. Samia kupitishwa kwa asilimia 100 na Mkutano Mkuu Maalum wa CCM.
Wasira alieleza kuwa uteuzi wa Dkt. Samia ulizingatia ibara ya 101 ya Katiba ya CCM, inayotaka mkutano mkuu kuchagua jina moja la mgombea urais.
“Uamuzi tulioufanya ni halali na umezingatia Katiba. Kwa hiyo, kama mtu ana mashaka, aje kwangu nitamsaidia kwa sababu tunafuata taratibu za kikatiba,” alisema.