Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma
MKUTANO Mkuu maalum wa chama Cha Mapinduzi (CCM),unaoendelea jijini Dodoma umechagua kwa kishindo Stephen Masato Wasira, kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.
Katika mkutano huo, kura 1921 zilipigwa, ambapo kura halali zilikuwa 1917. Kura za hapana zilikuwa 7 na kura za ndiyo zilikuwa 1910 sawa na asilimia 99.42 huku kura 4 zikiharibika.
Uchaguzi huu unamuweka Wasira katika nafasi muhimu ndani ya chama tawala, ambapo atakuwa na jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli za chama katika upande wa Bara.
Stephen Wasira, ambaye ni miongoni mwa viongozi wakongwe na wenye uzoefu mkubwa katika siasa za Tanzania, amehudumu katika nafasi mbalimbali serikalini, ikiwa ni pamoja na kuwa Mbunge na Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne.
Kwa nafasi hii, Wasira anapata nafasi ya kuendeleza ushawishi wake ndani ya CCM, wakati chama hicho kikiendelea na maandalizi ya uchaguzi ujao na mikakati ya kisiasa.
Mkutano Mkuu unaoendelea Dodoma unalenga kujadili masuala muhimu kuhusu mustakabali wa chama, na uteuzi wa Wasira ni miongoni mwa matukio makubwa yanayoendelea katika mkutano huo.
Kwa sasa, Wasira anakuwa sehemu ya uongozi wa juu wa CCM, akichukua nafasi muhimu katika kusimamia mikakati ya chama na kuimarisha uhusiano kati ya CCM na wananchi wa Tanzania Bara.