Na Munir Shemweta, WANMM

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kuwabana wamiliki wote wa ardhi wasiolipa kodi ya pango la ardhi sambamba na kutoendeleza maeneo wanayomiliki.

Wakiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa sharti la kulipa kodi na kuendeleza kwa wamiliki wa ardhi  Mkoa wa Pwani tarehe 13 februari 2025, timu maalum ya ukaguzi kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Mandeleo ya Makazi imesema hatua hiyo ni juhudi za wizara kukusanya kodi pamoja na kuhakikisha maeneo yanayomilikiwa na  wananchi yanaendelezwa.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mapato na Uwekezaji Wizara ya Ardhi Bw. Leonard Msafiri amesema, kwa mujibu wa sheria wamiliki wa ardhi wanatakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi na wasipofanya hivyo wanapaswa kupewa notisi ya kulipa ndani ya siku kumi na nne.

‘’Ulipaji wa kodi ya ardhi ni wajibu wa kisheria kwa mmiliki chini ya fungu 33 la sheria ya ardhi sura 113’’. Amesema

Akiwa katika shamba namba 57, 58, 59 na 60 lilipo Miswe Kibaha Mkoani Pwani, Kamishna wa Ardhi Msaidiźi Mapato na Uwekezaji Wizara ya Ardhi amemweleza mmiliki wa mashamba hayo kuwa ana nafasi ndani ya siku kumi na nne kulipa kodi ya ardhi. 

Aidha, Kamishna wa ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani Ndg. Hussein Sadiki Iddi, ameeleza kuwa ndani ya siku hizo kumi na nne mmiliki anaweza kufika Ofisi za ardhi ili kupewa ushauri na kueweka namna nzuri ya kufanya mazungumzo ya kulipa deni linalomkabili. 

Timu ya ukaguzi ilitembelea pia shamba namba 2 eneo la Miswe kata Mbwawa, halmashauri ya manispaa Kibaha ambapo mmiliki wake anadaiwa kiasi cha Tsh mil 690. Katika eneo hilo Kamishna Msafiri alielekeza mmiliki wake kupatiwa barua ya onyo ikiwa ni hatua ya kwanza ya mchakato wa ufutaji ardhi kwa mujibu wa fungu la 45 ya sheria ya ardhi sura ya 113. Barua hiyo alikabidhiwa Bw. Dunia Mrisho Kinyogoli ambaye ni  mwakilishi Miswe

Vile vile, timu hiyo ilitembelea kituo cha mafuta cha ATN picha ya ndege mkoani Pwani ambapo mmiliki wake amadaiwa kiasi cha Tsh 24. Mmiliki huyo alikabidhiwa barua ya onyo kupitia Meneja wa kituo Bw. Abdallah Bawazir.

Kamishna Msafiri alieleza kuwa zoezi la kufuatilia madeni ya kodi ya pango la ardhi ni endelevu na linafanyika katika mikoa yote hivyo amehimiza wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi kuhakikisha wanalipa madeni yao ili kuepuka usumbufu unaoweza kuwapata wakati wa kuendesha shughuli zao.

Timu Maalum ya kukagua utekelezaji sharti la kulipa kodi ya pango la ardhi ikizungumza na mmiliki wa Kampuni ya Buibui Investment Ltd Bw, Kessy Mwaipopo ilipotembelea eneo la kampuni hiyo lilipo Miswe Kibaha mkoa wa Pwani tarehe 13 Februari 2025.

Timu Maalum ya kukagua utekelezaji wa sharti la kulipa kodi ya pango la ardhi kutoka Wizara ya Ardhi ikikagua baadhi ya nyaraka ilipofika eneo la shamba la Miswe Farm tarehe 13 Februari 2025, Kibaha mkoani Pwani.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Pwani Ndg Husein Sadick Iddi akiangalia baadhi ya nyaraka wakati timu maalum ya ukaguzi kutoka wizara ya ardhi ilipotembelea shamba la Miswe lililopo halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani tarehe 13 Februari 2025.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi anayeshughulikia Mapato na Uwekezaji kutoka Wizara ya Ardhi Bw, Leonarld Msafiri (Katikati) akimfafanulia jambo Meneja wa Kituo cha Mafuta cha Picha ya Ndege mkoani Pwani Bw. Abdallah Bawaziri (Kushoto) wakati timu ya wizara ya ardhi ilipofuatilia sharti la ulipaji kodi ya pango la ardhi kwenye kituo hicho tarehe 13 Februari 2025. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)