Elizabeth Alexandra Mary Windsor alizaliwa mnamo Aprili 21,1926, katika jumba lililokuwa karibu na Berkeley Square jijini London.
Alikuwa kifungua mimba wa Albert, Mwanamfalme Mtawala wa York, aliyekuwa mwana wa pili wa kiume wa George V, na mkewe ambaye zamani alifahamika kama Lady Elizabeth Bowes-Lyon.
Elizabeth na dadake, Margaret Rose, aliyezaliwa mwaka 1930, walipewa elimu nyumbani na kulelewa katika mazingira ya familia yaliyojaa upendo.Elizabeth alikuwa na uhusiano wa karibu sana na babake na babu yake, George V.
Alipokuwa na miaka sita, Elizabeth alimwambia mwalimu wake wa uendeshaji farasi kwamba alitaka kuwa “mwanamke wa kukaa mashambani na awe na farasi na mbwa wengi.”
Alidaiwa kuanza kuonyesha hisia za juu sana za kuwajibika kutoka akiwa na umri mdogo sana.
Winston Churchill, ambaye baadaye alikuwa waziri mkuu, alinukuliwa akisema kwamba “alionyesha hisia za kuwa na mamlaka, ambazo zilikuwa nadra sana kupata kwa mtoto kama yeye.”
Licha ya kutohudhuria masomo katika shule ya kawaida, Elizabeth alifanya vyema sana katika kuzifahamu lugha mbalimbali na alifanya usomaji wa kina wa historia ya kikatiba.
Princess Elizabeth, akiwa na wazazi wake na dadake mdogo Margaret, wakati wa kutawazwa kwa babake kuwa mfalme, sherehe ambayo ilikuwa “ya kuvutia na ya kufana sana”.
Baada ya kifo cha George V mwaka 1936, mwanawe mkubwa wa kiume, aliyefahamika kama David, alirithi ufalme na kuwa Mfalme Edward VIII.
Hata hivyo, mwanamke aliyeamua kumuoa, Mmarekani aliyekuwa ametalikiwa mara mbili Wallis Simpson, hakukubalika kwa misingi ya kisiasa na kidini wakati huo. Mwishoni mwa mwaka, alijiuzulu.
Mwanamfalme Mtawala wa York, babake Malkia Elizabeth, alichukua ufalme na kuwa Mfalme George VI. Kutawazwa kwake kulimdokezea Elizabeth maisha yaliyomsubiri na baadaye aliandika kwamba aliiona sherehe hiyo kuwa “ya kupendeza sana”.
Huku uhasama na wasiwasi ukiongezeka Ulaya, Mfalme huyo mpya, pamoja na mkewe, Malkia Elizabeth, walichukua jukumu la kurejesha imani ya umma katika familia ya kifalme.
Mwaka 1939, bintimfalme huyo aliyekuwa na miaka 13 wakati huo, aliandamana na Mfalme na Malkia kwenye hafla katika chuo cha jeshi la wanamaji la Royal Naval College, Dartmouth.
Kwa pamoja na dadake Margaret, alimsindikiza mmoja wa waliokuwa wanafuzu, binamu wake wa kiwango cha tatu, Mwanamfalme Philip wa Ugiriki.
Harusi ya Bintimfalme Elizabeth na Philip Mountbatten ilirejesha furaha katika mazingira magumu ya baada ya vita
Hiyo haikuwa mara yao ya kwanza kukutana, lakini ilikuwa mara ya kwanza kwake kuanza kuvutiwa naye.
Prince Philip aliwatembelea jamaa zake wa familia ya kifalme alipokuwa likizoni kutoka kwenye jeshi la wanamaji – na kufikia mwaka 1944, alipokuwa na miaka 18, ilikuwa wazi kwamba Elizabeth alikuwa anampenda.
Alikuwa akiweka picha yake katika chumba chake, na walikuwa wakiandikiana pia barua.
Bintimfalme huyo alijiunga na kikosi cha wafanyakazi wa ziada wasaidizi wa jeshi kwa jina Auxiliary Territorial Service (ATS) mwishoni mwa vita, ambapo alijifunza kuendesha na kukarabati lori.
Siku ya kumalizika kwa vita, ambayo hufahamika kama VE Day, alijiunga na jamaa wengine wa familia ya kifalme katika Buckingham Palace huku maelfu ya watu wakikusanyika katika barabara kuu ya kuelekea kasri hilo ambayo hufahamika kama The Mall kusherehekea kumalizika kwa vita Ulaya.
“Tuliwaomba ruhusa wazazi wetu tutoke nje kwenda kujionea wenyewe,” alikumbuka baadaye.
“Nakumbuka tulikuwa na wasiwasi sana kwamba tungetambuliwa (na watu). Nakumbuka milolongo mirefu ya watu tusiowafahamu wakishikana mikono na kutembea kuelekea Whitehall, sote tulijumuika nao na kutembea kama waliobebwa na wimbi la furaha na kupata nafuu.”
Baada ya vita, nia yake ya kutaka kuolewa na Prince Philip ilikabiliwa na changamoto kadha.
Mfalme hakutaka kumpoteza binti wake ambaye alimpenda sana na Philip alihitajika kuondoa pingamizi la ubaguzi katika familia ya kifalme ambayo haikuwapendelea watu wenye asili ya nje ya nchi.
Lakini matamanio ya wawili hao yalitimia na mnamo 20 Novemba 1947, walifunga ndoa katika kanisa la Westminster Abbey
Mtawala wa Edinburgh, cheo kipya cha Philip, alisalia kuwa mhudumu katika jeshi la wanamaji.
Kwa muda mfupi, alitumwa kuhudumu jeshini Malta, na huko kwa kiasi fulani walifurahia maisha ya kawaida.
Mtoto wao wa kwanza, Charles, alizaliwa 1948, akifuatwa na dadake, Anne, aliyezaliwa 1950.
Lakini Mfalme, baada ya kupata mfadhaiko sana na shinikizo wakati wa vita, alikuwa amezidiwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu, ambao ulitokana na kuwa mvutaji sigara sugu.
Januari 1952, Elizabeth, aliyekuwa na miaka 25 wakati huo, akiwa na Philip, walifunga safari ng’ambo.
Mfalme alikaidi ushauri wa madaktari na kwenda uwanja wa ndege kuwaaga.
Ilikuwa ni mara ya mwisho kwa Elizabeth kumuona babake akiwa hai.
Elizabeth alipata habari za kifo cha Mfalme akiwa katika mgahawa wa kitalii katika mbuga moja nchini Kenya na mara moja alirejea London akiwa sasa ndiye Malkia.Baadaye alikumbuka yaliyotokea.
“Kwa njia fulani, sikuwa na wakati wa kujifunza kazi. Babangu alifariki akiwa bado na umri mdogo, kwa hivyo lilikuwa jambo la ghafla sana na ilikulazimu kuitekeleza kazi vyema kadiri ya uwezo wako.”
Sherehe ya kutawazwa kwake ilikuwa ya kwanza ya aina yake kutangazwa moja kwa moja kwenye runinga Uingereza
Sherehe ya kutawazwa kwake Juni 1953 ilipeperushwa moja kwa moja kwenye runinga, licha ya pingamizi kutoka kwa Waziri Mkuu Winston Churchill.
Mamilioni ya watu walikusanyika kutazama kwenye runinga, wengi wao kwa mara ya kwanza, kumtazama Malkia Elizabeth II akila kiapo.
Huku Uingereza ikiwa bado inakabiliwa na kipindi cha kubana matumizi ya ugumu wa kiuchumi baada ya vita, wachanganuzi walitazama sherehe hiyo ya kumtawaza malkia kama mwanzo wa enzi mpya ya mtawala mwingine kwa jina Elizabeth.
Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vilikuwa vimeongeza kasi ya kufikisha kikomo himaya kuu ya Uingereza, na kufikia wakati Malkia alipoanza safari ndefu ya kuzuru mataifa ya Jumuiya ya Madola Novemba 1953, maeneo mengi ambayo zamani yalikuwa miliki ya Uingereza, ikiwemo India, yalikuwa yamejipatia uhuru.
Elizabeth aliibuka kuwa mfalme au malkia wa kwanza kuzuru Australia na New Zealand.
Ilikadiriwa kwamba karibu robo tatu ya raia wa Australia walijitokeza kumuona.
Katika miaka ya 1950, mataifa zaidi yaliitupa bendera ya Uingereza na koloni za zamani na tawala zake sasa zilikusanyika kwa pamoja na mkusanyiko wa mataifa yenye uhusiano wa pamoja, kwa hiari.
Wengi wa wanasiasa walihisi kwamba Jumuiya mpya ya Madola ingetoa ushindani kwa muungano uliokuwa unaibuka wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Ulaya na, kwa kiwango fulani, sera ya Uingereza iliitenga kutoka kwa Bara la Ulaya.
Makala haya kwa msaada wa mitandao mbalimbali